Uchaguzi DRC: Tarehe mpya ya kupiga kura ni Disemba 30

Wafuasi wa Fayulu

Mamlaka za uchaguzi nchini Jamuhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) imetangaza kuahirisha uchaguzi mkuu uliokuwa umepangiwa kufanyika Jumapili kwa wiki moja.

Uchaguzi huo sasa umepangiwa kufanyika Jumapili tarehe 30 Desemba badala ya tarehe 23 Desemba.

Tume hiyo imesema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na kuchelewa kwa shughuli ya kufikisha vifaa na mitambo ya kupigia kura vituoni.

Msemaji wa tume ya uchaguzi DRC CENI Jean-Pierre Kalamba likuwa awali ameiambia BBC kuwa maandalizi yalikuwa hayajakamilika.

Mapema leo tume hiyo ilikutana na wagombea wa urais na wawakilishi wao katika kile kilichoonekana kama kutaka kupata maafikiano.

Mashine hizi za kupigia kura zimekuwa vikipingwa na upinzani
Maelezo ya picha, Mashine hizi za kupigia kura zimekuwa vikipingwa na upinzani

Uchaguzi wa DRC umekuwa ukisogezwa mbele kwa zaidi ya miaka miwili sasa, huku rais anayemaliza muda wake Joseph Kabila akishutumiwa kwa kutoa visingizio kadhaa vya kuahirisha uchaguzi ili aendelee kusalia madarakani.

Wiki iliyopita ghala la tume ya uchaguzi liliopo jijini Kinshasa liliteketea kwa moto na kuunguza baadhi ya vifaa muhimu vya uchaguzi, hata hivyo, mamlaka ziliwahakikishia wananchi kuwa moto huo hautaathiri kufanyika kwa uchaguzi.

Mamlaka zilidai kuwa moto uliozuka kwenye ghala la tume ya uchaguzi hautazuia uchaguzi wa Disemba 23.

Chanzo cha picha, CENI

Maelezo ya picha, Mamlaka zilidai kuwa moto uliozuka kwenye ghala la tume ya uchaguzi hautazuia uchaguzi wa Disemba 23.

"Tumewaambia mafundi wetu ya kwamba wafanye juhudi zao zote ili uchaguzi ufanyike Disemba 23, lakini kila wakati tunaangalia wapi walipofika. Kama haiwezekani tunapanga kuongea na wanasiasa ili kuangalia namna gani tutaweza kuahirisha uchaguzi na kuongeza siku nne, saba au 14 na sioni wapi kuna ubaya wakati tunataka kufanya mambo kwenye utaratibu mzuri," alisema Kalamba Alhamisi.

Tangazo hilo la ghafla linatokea wakati polisi walimzuia mmojwapo wa wagombea wakuu wa upinzani wa kiti cha urais Martin Fayulu kuzindua kampeni zake katika mji mkuu wa nchi hiyo.

Wagombea wakuu wa urais DR Congo

Alipokuwa bado anazuiwa, Fayulu ameiambia BBC kuwa hatakubali uchaguzi uahirishwe hata kwa sekunde.

"Hatuwezi kukubali kukubali kuahirishwa kwa uchaguzi kwa namna yeyote ... (rais Joseph) Kabila amefahamu kuwa mimi naitwa mwanajeshi wa raia, ikiwa tarehe 23 hakuna uchaguzi kabila na mkuu wa tume huru ya uchaguzi wanapaswa kuondoka," amesema Fayulu.

Kama kweli uchaguzi utaahirishwa, kuna kila dalili ya kutokea kwa machafuko ya kisiasa na makabiliano kati ya raia na vyombo vya usalama.

Uchaguzi huu ukifanikiwa kufanyika itakuwa ndiyo mara ya kwanza kwa DRC kushuhudia mabadiliko ya uongozi kwa njia ya amani.

Kuzuiwa Kampeni

Polisi walilazimika kuwatawanya kwa mabomu ya machozi wafuasi wa upinzani baada ya kuzuia mkutano wao wa kampeni
Maelezo ya picha, Polisi walilazimika kuwatawanya kwa mabomu ya machozi wafuasi wa upinzani baada ya kuzuia mkutano wao wa kampeni

Mamlaka za jiji Kinshasa zilitangaza marufuku ya kufanyika kwa shughuli za kampeni kuanzia jana katika jiji hilo kuu la nchi ikiwa ni muda mchache tu kabla ya Fayulu kuzindua kampeni zake.

Licha ya tangazo hilo, maelfu ya wafuasi wa Fayulu walijitkeza kwenye uwanja ambao ulipangwa kufanyika kwa mkutano wao.

Hata hivyo, Fayulu alizuiwa na polisi takribani kilomita 50 mbali na uwanja huo na kumfanya kushindwa kufika na kuhutubia na kumwaga sera mbele ya wafuasi wake.

Vurugu
Maelezo ya picha, Vurumai zilizuka baada ya mkutano wa mgombea wa upinzani Martin Fayulu kuzuiliwa

Gavana anayeegemea upande wa serikali wa mji wa Kinshasa Andre Kimpita, alisema kuwa hatua hiyo ya kupiga marufuku mikutano ya siasa imechukuliwa kwa sababu za kiusalama.

Ebola DRC Darubini Kufikia: 22/07/2019

Waliofariki: 1649

Walioambukizwa: 849

Jumla ya visa vilivyothibitishwa: 2498

BBC

Hatua hiyo haikupokelewa vyema na wafuasi wa Fayulu ambao waliingia barabarani na kuandamana wakitishia vurumai iwapo Fayulu hatakabidhiwa mamlaka baada ya uchaguzi.

Polisi iliwalazimu kutumia nguvu ya ziada kuwatawanya wafuasi hao wa Fayulu kwa kuwarushia mabomu ya machozi.