Uchaguzi DRC 2018: Majengo ya tume ya uchaguzi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yateketea

Chanzo cha picha, CENI
Majengo yanayotumiwa na tume ya taifa ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yameshika moto na kuteketea mjini Kinsasa.
Moto huo ulizuka mwendo wa saa nane usiku wa manane na kuzua taharuki ikizingatiwa kwamba ni siku 10 zilizosalia kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika nchini humo.
Moshi mweusi ulitanda angani na uliweza kuonekana kutoka mbali asubuhi kulipopambazuka, shirika la AFP limeripoti.
Moto huo unadaiwa kuathiri majengo ambayo yamekuwa yakitumiwa kuhifadhi vifaa vya uchaguzi.
Chanzo cha moto huo bado hakijabainika.

Chanzo cha picha, CENI
Waziri wa mambo ya ndani Henri Mova Sakanyi amesema uharibifu uliotokea ni mkubwa mno.
Duru zinasema kulikuwa na mashine takriban 7,000 za kupitia kura ziliharibiwa.

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images
"Tunatumai kwamba kisa hiki hakitavuruga mchakato wa uchaguzi. Uchunguzi unaendelea," Jean Pierre Kalamba, msemaji wa tume ya uchaguzi (CENI) amenukuliwa na vyombo vya habari.
Kampeni za uchaguzi huo zimekumbwa na ghasia katika baadhi ya maeneo nchini humo.
Jumatano, watu watatu waliuawakatika makabiliano kati ya polisi na wafuasi wa upinzani katika mkutano wa kampeni uliokuwa unafanyika mashariki mwa nchi hiyo.

Chanzo cha picha, CENI
Ghasia zilizuka katika mji wa Kalemie, ulio ufukweni katika Ziwa Tanganyika wakati wa mkutano wa kampeni wa Martin Fayulu.
Watu wawili walioshuhudia, wamenukuliwa na AFP wakisema risasi zilifyatuliwa baada ya Bw Fayulu kuwasili na kuanza kuelekea eneo la mkutano.

Chanzo cha picha, FABRICE COFFRINI
Fayulu aliwatuhumu polisi kwa kuchangia ghasia hizo, pamoja na "magenge ya vijana wenyewe silaha" aliosema walikuwa wamevalia mavazi ya PPRD, akirejelea chama tawala nchini humo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Jumanne, wafuasi wawili wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Fayulu waliuawa na wengine 43 kujeruhiwa katika machafuko yaliyotokea katika mkutano wa kampeni jijini Lubumbashi, jiji la pili kwa ukubwa DRC.
Fayulu, 62, mbunge ambaye hakuwa maarufu sana, alipata umaarufu baada ya kuidhinishwa na muungano wa upinzani kuwa mgombea wa pamoja.
Felix Tshisekedi hata hivyo alijiondoa kwenye muungano huo akiwa pamoja na Vital Kamerhe na wawili hao wanawania kwa pamoja, Tshisekedi akiwa mgombea urais kwa ahadi kuwa Bw Kamerhe atakuwa waziri mkuu wakishinda.
Uchaguzi nchini DR Congo utafanyika 23 Desemba.












