Uchaguzi DRC: Mamlaka zapiga marufuku mikutano ya vyama vyote ya kisiasa mjini Kinshasa

Mamlaka nchini Jamhuri wa Demokrasi ya Congo zimepiga marufuku mikutano yote ya kisiasa kwenye mji mkuu Kinshasa kwa wagombea wote wa urais siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa kihistoria nchini humo.
Gavana anayeegemea upande wa serikali wa mji wa Kinshasa Andre Kimpita, alisema kuwa hatua hiyo ya kupiga marufuku mikutano ya siasa imechukuliwa kwa sababu za kiusalama.

Tangazo hilo ambalo halikutarajiwa linakuja wakati mgombea mkuu wa upinzani Martin Fayulu alikuwa azindue kampeni yake ya kisiasa mjini Kinshasa.
Uchaguzi huu mkuu ambao utaandaliwa tarehe 23 mwezi huu ambao ni wa kumtafua mrithi wa Rais Joseph Kabila, umekuwa ukihairishwa kwa muda mrefu na itakuwa ndiyo mara ya kwanza kutakuwa na mabadiliko ya uongozi kwa njia ya amani nchini Jamhuri ya Demokrasi ya Congo.

Chanzo cha picha, PPRD
Chama tawala nchini DRC kimemteua Emmanuel Ramazani Shadary waziri wa zamani wa mashauri ya ndani na mwaminifu kwa Rais Joseph Kabila kuwa mgombea wake.
Mwezi uliopita viongozi wakuu wa upinzani nchini DRC walimchagua Bw Fayulu ambaye ni mfanyabiashara kama mgombea wao katika kinyang'anyiro cha Desemba 23.

Chanzo cha picha, FABRICE COFFRINI
Uteuzi wa mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 61 Martin Fayulu ulifanyika baada ya mazungumzo baina ya viongozi wakuu wa vyama saba vya upinzani yaliyofanyika mjini Geneva nchini Uswizi.
Hata hivyo upinzani uligawanyika siku chache baadaye kufuatia mwanasiasa mwingine wa upinzani Felix Tshisekedi kutangaza kuwa hamuungi mkono Fayulu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Tshekedi, kiongozi wa chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS) aliidhinishwa kuwa mgombea wa urais baada ya mazungumzo kati yake na mgombea wa chama cha UNC (Union for the Congolese Nation) Vital Kamerhe.
Mwafaka kati ya wawili hao uliafikiwa jijini Nairobi mnamo 23 Novemba.

Chanzo cha picha, Getty Images













