Karl Patterson Schmidt: Mtaalamu wa nyoka aliyeandika safari ya kifo chake Marekani

A boomslang snake

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Boomslang akikuuma sehemu kubwa ya damu hupoteza uwezo wake wa kuganda

Mnamo Septemba 1957, mkurugenzi wa kituo cha kuwahifadhi wanyama cha Lincoln Park Zoo mjini Chicago aliagiza nyoka mmoja atumwe kwenye Makumbusho ya Historia ya Maumbile atambuliwe ni wa aina gani.

Nyoka huyo mwenye urefu wa sentimita 76 alifaa akaguliwe na Karl Patterson Schmidt, mtaalamu maarufu wa nyoka aliyekuwa amefanya kazi katika makumbusho hayo kwa miaka 33.

Alikuwa mtaalamu wa nyoka wanaokaa kwenye matumbawe na alikuwa amejikusanyia mkusanyiko mkubwa sana wa nyoka kutoka kila pembe ya dunia kufikia wakati wa kustaaf wake kama Mhifadhi Mkuu wa Viumbe mwaka 1955.

Kwa hivyo, aliamua kuikumbatia kazi hiyo na kumkagua vyema ili kumtambua.

Kung'atwa na nyoka

Nyoka huyo alikuwa na michoro ya rangi za kupendeza kwenye ngozi yake na kichwa chake kilikuwa na umbile sawa na la nyoka wa kijani anayeishi mitini Afrika Kusini ambaye hufahamika kama Boomsland, Schmidt aliandika.

Lakini alishangazwa na hali kwamba gamba lake la kwenye mkundu, ambalo hufunika sehemu ya kuendea haja, halikuwa limegawanyika.

Hatua aliyoichukua baada ya hapo ilimgharimu maisha yake; alimnyanyua nyoka huyo ili kumtazama kwa makini.

A venomous Boomslang snake lurks inside David Jones' 'snake house' at the Chameleon Village Reptile Conservation Park on July 12, 2010 in Johannesburg, South Africa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Nyoka aliyemuua mtaalamu huyo baadaye ilibainika kwamba alikuwa aina ya Boomslang, kama huyu aliyeko pichani

Schmidt alipomuinua nyoka huyo, alimshambulia na kumuuma kidole cha gumba cha mkono wake wa kushoto, na kumuacha na vidonda viwili vidogo, vilivyokuwa vinavuja damu kidogo.

Schmidt alianza kuinyonya damu kutoka kwenye kidole chake cha gumba badala ya kutafuta usaidizi wa kimatibabu.

Badala ya kwenda hospitalini, alianza kuandika kuhusu athari za sumu hiyo kwenye mwili wake.

Chini ya saa 24 baadaye, alikuwa ameshafariki.

Siku ya mwisho ya Schmidt

Schmidt pengine alidhani, kama wataalamu wenzake wa wakati huo, kwamba nyoka aina ya Boomslang ambao huwa na meno karibu na mkundu wao hawawezi kutoa sumu ya kutosha kuwaua binadamu.

Kwa hivyo, badala ya kuwa na wasiwasi, alikwenda zake nyumbani na kuanza kuandika athari za sumu hiyo kwenye mwili wake.

Alidhani angepona.

Science Friday, kipindi cha redio ya PRI nchini Marekani, kilitoa video ya "Diary of a Snakebite Death" (Shajara ya Kifo kutokana na Kuumwa na Nyoka), ikieleza kwa kina saa za mwisho za Schmidt duniani, kupitia kuangalia aliyoyaandika kwenye shajara yake.

Chicago Field Museum of Natural History

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Schmidt alikuwa na mkusanyiko mkubwa sana wa nyoka wa aina mbalimbali Chicago

"4:30 - 5:30 PM nahisi kichefuchefu sana, lakini sitapiki. Wakati wa safari kwenda Homewood, nimetumia treni.

5:30 - 6:30 PM kibaridi kikali na kutetemeka, na baadaye kupata homa kali 101.7 [38.7 ºC]. Kutokwa na damu mdomoni, jambo lililoanza mwendo wa saa 5:30, sana kutoka kwenye ufizi.

8:30 PM nimekula vipande viwili vya mkate wa tosti wenye maziwa.

9:00 to 12:20 A.M. nililala vyema. Nilikwenda haja saa 12:20 AM zaidi nikawa natokwa na damu, lakini kiasi kidogo. Nilikunywa gilasi ya maji saa 4:30 AM, lakini baadaye nikaanza kuhisi kichefuchefu na kutapika sana, nilitapika chakula nilichokuwa nimekila kikiwa bado hakijameng'enywa. Nilipata nafuu kidogo na kulala hadi 6:30 AM"

Kukataa msaada

Schmidt aliulizwa saa chache kabla ya kifo chake kama alihitaji usaidizi wa kimatibabu.

Lakini alikataa, akisema hakutaka kuingilia dalili alizokuwa akizihisi, ambazo alikuwa akiziandika kwenye shajara yake.

Badala yake, akiongozwa na hamu yake ya sayansi, aliendelea kuandika matukio kwenye kitabu chake baada ya kula kiamsha kinywa.

"Septemba 26. 6:30 AM. Kiwango cha joto 98.2 (36.7 ºC). Nilikula chakula cha nafaka na mayai ya kuvukizwa, na sosi ya tufaha pamoja na kahawa kama kiamsha kinywa. Sikutoa mkojo hata kidogo lakini nilivuja damu kiasi kidogo kila baada ya saa tatu hivi. Naoendelea kutokwa na damu mdomoni na puani, lakini si sana."

"Sana", Science Friday wanasema lilikuwa neno la mwisho kwa Schmidt kuandika kwenye shajara yake.

Chicago Daily Tribune front page on 3 October 1957

Chanzo cha picha, Chicago Daily Tribune

Maelezo ya picha, Schmidt's unusual death was the headline of the Chicago Daily Tribune on 3 October 1957

Mwendo wa kula chakula cha mchana saa 1.30 pm, alitapika na akamwita mke wake.

Usaidizi ulipofika, alikuwa amepoteza fahamu na alikuwa na atatokwa na jasho sana.

Daktari aliitwa na juhudi za kujaribu kuokoa maisha yake zikaanza, alipokuwa anapelekwa hospitalini.

Kufikia saa tisa alasiri, 3 p.m. Schmidt alithibitishwa kufariki, kutokana na "kulemaa kwa mfumo wake wa kupumua".

Uchunguzi wa maiti yake ulibaini kwamba matatizo ya kupumua yaliyotokana na damu kuingia kwenye mapafu yake.

Alifariki kutokana na kuvuja damu kwenye macho yake, mapafu, figo, moyo na ubongo.

Sumu hatari

Uchunguziwa kisayansi uliofanywa kwa miongo miwili baada ya kifo cha Schmidt, ulibaini kwamba nyoka aina ya Boomslang ni miongoni mwa nyoka wenye sumu kali zaidi Afrika.

Ukiumwa na nyoka huyo, sumu yake inaweza kusababisha kuganda vya damu na kuwa chembe ndogo ndogo, na sehemu iliyosalia ya damu kupoteza uwezo wake wa kuganda.

Hivyo, mwathiriwa huvuja damu hadi kufa.

Nyoka huyo ambaye hupatikana kwenye miti huwa maeneo ya kusini na kati Afrika na anapokomaa anaweza kuwa na urefu wa 100-160 cm, baadhi hufikia urefu wa 183 cm.

Nyoka ha huwala vinyonga, mijusi, vyura na wakati mwingine wanyama wengine wadogo, ndege na mayai.

Taarifa ya Chicago Daily Tribune mnamo 3/10/1957

Chanzo cha picha, Chicago Daily Tribune

Maelezo ya picha, Schmidt aliamini sumu hiyo haingemuua, gazeti la The Chicago Daily Tribune liliandika

Lakini huchukuliwa kama nyoka mwenye woga sana, na mara nyingi hukimbia kiumbe yeyote ambaye ni mkubwa kuliko wanyama aliozoea kuwala.

Juhudi za Schmidt za kutaka kumkagua nyoka huyo kwa makini bila kutafakari sana, kama ilivyoelezwa nammoja wa walioshuhudia, huenda ndiyo sababu iliyomfanya nyoka huyo kumuuma.

Inaaminika kwmaba Schmidt na wenzake hawakuamini kwamba sumu ya nyoka huyo ingekuwa hatari kiasi cha kumuua, mwanzo kutokana na hali kwamba ni nyoka mdogo sana.

Pili, ni jino moja tu ambalo liliingia kabisa ndani ya ngozi yake, kiasi cha 3 mm hivi. Na isitoshe, mwathiriwa alionekana mwenye afya.

Lakini wengine wameeleza kwamba Schmidt huenda alifahamu kwamba wakati huo hakukuwa na dawa yoyote ya kumaliza sumu ya nyoka aina ya Boomslang na kwamba tumaini lake wakati huo lilikuwa tu apate nafuu bila usaidizi wowote.

Licha ya kilichokuwa kikitokea akilini mwake baada ya kuumwa, Schmidt ni wazi kwamba hakubadilisha mtazamo wake na kujitolea kwa kazi yake, aliandika mwandaaji wa vipindi wa Science Friday, Tom McNamara.

Badala yake "alijitumbukiza kwenye ulimwengu wa mambo yasiyofahamika sana".