David Maligana: Nilianza kwa kuchimba makaburi, sasa najivunia kuhifadhi maiti

David Maligana, maarufu kama Mgogo anajivunia kazi yake
Maelezo ya picha, David Maligana, maarufu kama Mgogo anajivunia kazi yake

David James Maligana ni Mfanyakazi katika chumba cha kuhifadhia maiti, kwa zaidi ya miaka kumi sasa, ambayo pia imebadili maisha yake.

Uwezo wake wa kuuandaa mwili wa marehemu, umempa umaarufu kiasi cha kumfanya marehemu kuonekana kama mtu aliyelala usingizi tu, pale anapoagwa na ndugu zake tayari kwa mazishi.

Kazi hii alianza mwaka 2003, akiwa ni mtumishi wa Manispaa ya Dodoma, katika kitengo cha Afya, Kinga na Uuguzi akifanya kazi ya kuchukua uchafu mitaani na kupeleka kutupwa katika maeneo maalumu.

''Ndio tulikuwa tukihusika na kuchukua miili ya marehemu kwenye hospitali ya mkoa wa Dodoma na ile ya Milembe na kuchimba makaburi na kwenda kuistiri Ipagala'' Anasema Maligana.

Katika harakati za kutafuta maisha, mwaka 2005 alifika katika kisiwa cha Ukerewe mkoani Mwanza, huko ambako ndiko safari ya kazi yake hiyo ilipoanzia.

Baada ya kupata taarifa za kufariki kwa mfanyakazi wa chumba cha maiti katika hospitali ya Ukerewe, Maligana anasema alijaribu bahati yake, na kwenda kutafuta kazi hapo na baada ya kuhojiwa kwa muda kama ana uwezo wa kumudu kazi hiyo, mwishowe alifanikiwa kuipata.

Anasema mwaka 2008 aliajiriwa rasmi na kukaa katika hospitali hiyo kabla ya mwaka 2013 kuhamia katika hospitali ya Sekou Toure mjini Mwanza.

Amepitia changamoto nyingi, mwenyewe anasema alifanya kazi muda mrefu kama kibarua na kwamba jamii pia haikumchukulia kama mtu wa kawaida.

Hata hivyo anasema licha ya kufanya kazi katika mazingira ya kutisha, hajawahi kupata changamoto yoyote inayohusiana na imani za kishirikina.

wahudumu wa vyumba vya kuhifadhia maiti

''Binafsi nina zaidi ya miaka kumi, kwenye kazi hii na nimefanya kazi katika maeneo mbalimbali, nimewahi kuitwa kufanya uchunguzi, kwenye miili ya watu waliozikwa, wengine ndio kwanza walikuwa na majuma mawili tu, wengine moja pamoja na miili ya aina mbalimbali mengine imeuawa ama kutupwa tu, lakini sijawahi kukutana na changamoto hizo,,'' amesema Maligana.

Aidha anasema changamoto nyingi pia alizipata kabla ya kupata mafunzo ya kazi yake hiyo, yaliyomfanya kufanya kazi yake kwa ufanisi.

Licha ya wengi kuwa na zana potofu na Wafanyakazi wa Chumba cha maiti, David James Maligana amekuwa akipata faraja kutoka kwa familia yake, hususan mkewe ambaye anamuunga mkono sana.

Mkewe Martha David anasema awali alivyosikia kazi ya mume wake aliogopa lakini sasa amezoea, anaona ni ya kawaida kama nyingine.

"Jamii ili nishawishi kuachana na mume wangu kutokana na kazi yake kuwa mbaya na kwamba inaleta madhara katika ukoo..'' Amesema Martha

Amewashauri wanawake wengine kutowanyanyapaa waume zao kutokana na kazi zao ambazo pengine hazithaminiki katika jamii.