Samaki wanaoishi ziwa Victoria wamo hatarini kuangamia

Wavuvi wa samaki ziwani

Utafiti mpya unaonyesha kwamba robo tatu ya aina zote za viumbe hai waishio kwenye maji yasiyo ya chumvi katika Ziwa Victoria lililopo Afrika Mashariki wamo hatarini ya kuangamia kutokana na uchafuzi wa mazingira na uvuvi uliopindukia.

Hiyo inatishia maisha ya takriban watu milioni 42 wanaoishi Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi.

Wahifadhi wa Mazingira wanatoa wito kwa matumizi bora ya ardhi na maji ya ziwa hilo kubwa zaidi za Afrika.

Utafiti huo wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Uasilia (IUCN) unaonesha asilimia 20 ya aina zote za viumbehai waliozingatiwa kwenye utafiti huo walibainishwa kuwa kwenye hatari ya kuangamia.

"Aina nyingi za viumbehai wanaoishi kwenye Bonde la Ziwa Victoria wako kwenye hatari kubwa, hasa kutokana na uchafuzi wa mazingira, matumizi ya rasilimali za kibiolojia (uvuvi uliopita kiasi), kilimo na viumbehai vamizi," ripoti ya shirika hilo inasema.

"Hatari hizi zimepelekea kiasi cha asilimia 19.7 ya aina za viumbehai wanaoishi kwenye maji baridi kwenye ukanda huu kutathiminiwa kama viumbehai walioko hatarini, na kiasi kikubwa cha kutisha, yaani asilimia 76 ya viumbehai wanaoishi kwenye maji yasiyo ya chumvi wanaopatikana katika ukanda huo pekee, kutathminiwa kama viumbehai walioko hatarini zaidi."

Ziwa Victoria

Samaki ndio walio kwenye hatari kubwa zaidi ambapo hatari inayowakabili ni kiasi cha asilimia 55.1 ya aina ya viumbehai wote waliotathminiwa.

Wanafuatiwa na kundi la konokono (yaani asilimia 25.5), dekapoda (asilimia 8.3), mimea (asilimia 9.0) na viumbe hai vinavyojulikana kisayansi kama odonata (asilimia 1.9).

Shirika hilo linasema kuna upungufu wa ufahamu wa kutosha kuhusu aina za viumbehai wanaoishi kwenye maji baridi kwa ajili ya kuwezesha maamuzi muafaka kuhusu mazingira na maendeleo kwenye bonde la ziwa.

IUCN wanasema kuendelea kupungua kwa viumbehai wanaoishi kwenye maji baridi kunaathiri maisha ya jamii masikini katika vijiji vilivyoko kando kando ya bonde hilo.

Samaki

"Samaki wa maji yasiyo ya chumvi ni muhimu sana kwa chakula (kwa binadamu na wanyama), na shughuli za uvuvi katika ziwa Victoria usaidia maisha ya kaya za mamilioni ya watu wanaoishi kando kando ya bonde hilo," ripoti ya shirika hilo inasema.

„Mimea inayopatikana ziwani ina matumizi mengi, ikiwa ni pamoja na dawa, chakula, ujenzi na kutengeneza bidhaa za mikono ambazo ni rasilimali muhimu kwa jamii hizi hasa kwa vile jamii nyingi hazipati wala hazimudu bidhaa ghali za sokoni."

Samaki wa maji baridi kwenye ukanda huo wanaathirika sana na mabadiliko ya tabianchi, kwa kuhisi haraka mabadiliko, kuwa kwenye hali ya kukumbana na mabadiliko, na kuwa na uwezo mdogo wa kumudu mazingira yanapobadilika.

Maafisa wa IUCN wamependekeza mbinu za usimamizi zinazowajumuisha wadau wote katikabonde la ziwa hilo pamoja na taratibu za maji ya kinga ya uhai wa viumbe zitumiwe kuhakikisha kuwa mifumo ya ikolojia kwenye maji baridi inaendelea kutoamaji, bidhaa na huduma kwa mifumo mingine ya ikolojia kwa uendelevu, na wakati huo huo ikiendelea kusaidia viumbehai.

"Hali hii itasaidia kudumisha faida za kijamii na kiuchumi za bonde hili," shirika hilo linasema.

Presentational grey line

Upekee wa Bonde la Ziwa Victoria

Victoria

Bonde la Ziwa Victoria linatambulika kimataifa kwa kuwa na idadi na aina nyingi za viumbehai tofauti wanaoishi kwenye maji yasiyo ya chumvi na wanaopatikana katika bonde hilo pekee, ambao wana umuhimu mkubwa kwa maisha ya wenyeji na kwa uchumi wa taifa katika bonde hilo.

  • Bonde hilo linahifadhi aina nyingi za viumbehai wakaao kwenye maji yasiyo ya chumvi, ambao wanachangia kuwepo kwa aina nyingi ya mifumo ya ikolojia.
  • Utafiti wa shirika la IUCN uligundua kati ya viumbe wa maji safi 601 waliochunguzwa, viumbehai 204 ni wa asili ya ziwa hilo (sawa na asilimia 31.3)
  • Kiwango hiki cha uasilia ni cha juu miongoni mwa samaki ambapo asilimia 78.2 waligunduliwa kuwa wa asili ya ziwa hilo.
  • Bonde la Ziwa Victoria hujumuisha ziwa hilo na maeneo yenye mito inayomwaga maji ndani ya ziwa hilo. Ziwa Victoria ni ziwa lenye maji yasiyo ya chumvi la pili kwa ukubwa wa eneo duniani ambapo ukubwa wake ni kilomita mraba 68,800. Ziwa Victoria linapatikana Kenya, Tanzania na Uganda.
  • Eneo lote la bonde ni la kilomita mraba 193,000 na hushirikisha mito na maziwa yanayopatikana Rwanda na Burundi.
  • Wakazi wa mataifa yenye bonde la ziwa hilo ni asilimia 30 ya wakazi wa mataifa hayo matano, jumla ya watu 42 milioni.
Presentational grey line