Dkt Anthony Mwandulami: Mtanzania anayejijengea kaburi lake la kifahari Njombe kusini mwa Tanzania

Umewahi kujiuliza utazikwa wapi baada ya kufa? Mwanamume mmoja nchini Tanzania ameamua hataki utata kuhusu hatima yake baada ya kufa.
Dkt Anthony Mwandulami mkaazi wa Njombe nyanda za juu Kusini mwa Tanzania ameshaanza kujijengea kaburi lake tayari. Mwandulami ambaye pia ni mganga wa tiba asilia, anasema kaburi hilo ambalo amekuwa akilijenga kwa takriban miaka minane sasa.
Alimwambia mwandishi wa BBC David Nkya kwamba sababu kuu inayomfanya kujijengea kaburi hilo ni kuihifadhi historia yake baada ya kifo.
Kaburi hili si tu limeleta mshangao kwa wakazi wa eneo la Njombe, lakini pia linawashtua wengi nchini kote.
Lina urefu wa mita kumi na mbili kwenda chini na limejengwa kwa mfumo wa jengo la ghorofa.
Haya ndio makazi ya kudumu ya Antony Mwandulami baada ya kufa.
Lakini Waafrika wengi hawana tabia ya kufikiria watazikwa wapi ukiachilia mbali kujijengea makaburi wangali wako hai, kulikoni kwa Mwandulami?

"Kaburi hili nimeamua kulijenga, nimeona si vizuri sana kutokana na shughuli zangu nilizozifanya hapa Tanzania na nilivyowasaidia Watanzania, halafu nikapotea tu. Na wakati huo huo nimeona nina uwezo wa kujitengenezea sehemu ya kuhifadhi mwili wangu. Nikaona bora nitengeneze. Kaburi hili nimeliandaa kwa ajili ya kupumzisha mimi na wake zangu," anasema.
"Ni muhimu sana kwa sababu siwezi kusahaulika na wajukuu zangu pamoja na watakaozaliwa na familia yangu watakuja kujua kwamba huyu ni nani na alifanya nini kwenye familia yetu.

Mwandulami anasema ndani ya kaburi hili, atazikwa yeye pamoja na wake zake watatu.
Haya ni makubaliano ambayo wamejiwekea tayari na wake zake. Mke wake mkubwa juu ya suala hili?
"Mimi naona ni vizuri amefanya jambo la maana sana, kutengeneza makao yake. Tumelipokea vizuri, tumefurahi. Kwa sababu ameshatengeneza sehemu nzuri anapolala yeye na sisi wake zake tunalala hapo hapo," anasema mkewe kwa jina Damian.
Amechimba chini mita 12 na chini kabisa ndiko kunakopatikana makaburi yenyewe. Mwili wake utakaushwa kabla ya kuhifadhiwa, anasema.
Utamaduni wa kujijengea kaburi kama hili kabla hujafa ni kitu kigeni kabisa hapa. Lakini kwa mujibu wa Mwandulami, kaburi lake hili linatarajia kugharimu takriban dola 500,000 ambazo ni sawa na Sh1 bilioni mpaka kukamilika kwake.

Na kwa viwango vya chini vya maisha kijijini humo, fedha anazotumia ni nyingi sana.
Wanakijiji wenzake wameshangazwa na hatua hiyo.
Ujenzi bado unaendelea. Licha ya maandalizi haya yote, swali ambalo huenda hata wewe unajiuliza, je ni nini hatma ya ujenzi hasa iwapo kifo chake kitasababisha mwili wake usionekane?













