Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mo Dewji: Utata waibuliwa juu ya picha za gari alilotekewa bilionea Mohammed Dewji
Utata mkubwa umeibuka juu ya uhalisia wa picha ya gari linalodaiwa kuhusika katika tukio la kutekwa kwa bilionea Mohammed Dewji nchini Tanzania.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, Inspekta Jenerali (IGP) Saimon Sirro amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Ijumaa kuwa wamelitambua gari aina ya Toyota Surf lenye namba za usajili wa kigeni kuhusika kwenye mkasa huo.
IGP Sirro alionesha picha za gari hiyo alizodai zimepatikana kutoka kwenye kamera ya kunasa matukio (CCTV) ya hoteli ya Colosseum.
Dewji maarufu kama Mo alitekwa na watu wasiojulikana alfajiri ya siku ya Alhamisi, Octoba 11 punde tu aliposhuka kwenye gari yake akieleka mazozini katika hoteli moja ya kifahari.
Hata hivyo, punde tu baada ya picha hiyo kutua mitandaoni, baadhi ya watu wakaanza kuonesha mashaka yao juu ya uhalisia wake.
Mwanamziki maarufu wa Bongo Flavour, Mwana FA ambaye pia hufanya mazoezi katika hoteli hiyo, kupitia ukurasa wake wa Twitter ameeleza mashaka yake akisema picha hiyo haioneshi gari hilo likiwa katika hoteli ya Colosseum.
Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani kupitia chama cha upinzani Chadema Godbless Lema ambaye majuzi alidai kuwekwa wazi kwa picha za CCTV za tukio hilo nae kupitia ukurasa wake wa Twitter alihoji kama kweli picha hiyo ilichukuliwa katika hoteli ya Colloseum na iwapo kweli ni ya CCTV.
Mtu mwengine aliyehoji maswali kama hayo ni Afisa Usalama wa zamani nchini Tanzania na mwandishi wamakala mwenye maskani yake nchini Uingereza, Evarist Chahali. Chahali amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais John Magufuli, na katika hili amekwenda mbali na kudai polisi wamedanganya.
Chahali pia aliweka picha ya CCTV ikimuonesha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alipovamia ofisi za Clouds TV mwezi Machi 2017 na kulinganisha na za gari hilo, akisema ya Makonda ni halisi na ya gari ni feki.
Awali IGP Sirro alisema wamebaini nambari ya usajili wa gari hilo ni AGX 404 MC, limeingia nchini kutoka nchi jirani likiendesha na Obasanjo Zacharias Junior na mpaka sasa bado lipo Tanzania.
"Tumefuatilia na watu wetu wamekwenda mpaka mpakani na wameweza kuona lilipita tarehe 1 Septemba 2018. Tumepata maelezo ya kutosha ambayo siwezi kuyasema," amesema.
Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe ametumia ukurasa wake wa twitter kuonesha kutokubaliana kwake na kauli hiyo.
Pia Zitto amedai kuwa anaamini polisi wanajua mahali Mo alipo.
Kuna watu ambao wanahoji juu ya pembe (angle) ambayo picha hiyo imepigwa. Kawaida, wanasema, kamera za CCTV kuwa juu na picha zake huchukuliwa kwa pembe ya juu (oblique angle) lakini picha hiyo ya gari iliyotolewa na polisi pembe yake ni ya usawa wa kati (horizontal) kama zilivyo picha nyengine za kawaida.
Kwamujibu wa kamanda Sirro mpaka sasa hawajajua Mo amefichwa wapi na uchunguzi bado unaendelea juu ya tukio hilo.
Sirro pia amekataa kukubali au kukanusha iwapo waliotekeleza uteakaji huo ni wazungu wawili kama ilivyodaiwa awali na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda na kamanda wa polisi wa kanda maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa.