Mo Dewji: Tunayoyafahamu kufikia sasa kuhusu kutekwa kwa bilionea Mtanzania Mohamed Dewji

Muda wa kusoma: Dakika 7

Ni zaidi ya wiki moja sasa tangu bilionea wa umri mdogo zaidi barani Afrika Mohamed Dewji, 43, kutekwa nyara na watu wasiojulikana jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini Tanzania Simon Sirro amesema bado hawajui alipo Mo Dewji lakini wamefanikiwa kupata maelezo kuhusu gari lililotumiwa na watekaji nyara hao ambalo amesema lilitoka moja ya nchi jirani na kuingia Tanzania tarehe 1 Septemba mwaka huu.

Amesema wamebaini kuwa waliomteka walikuwa na bastola ambazo ni za kufyatua risasi za ukubwa wa 9mm.

Kufikia sasa bado hakuna taarifa za alipo wala wahusika wakuu katika utekaji nyara wake kukamatwa.

Hapa, tunaangazia mambo ambayo yanafahamika kufikia sasa kuhusu kutekwa kwa tajiri huyo ambaye hufahamika na wengi kama Mo Dewji.

Mo Dewji alivyotekwa

Ailikuwa ni Alhamisi tarehe 11 Oktoba na Mo alikuwa amekwenda kwenye kituo cha mazoezi ya Colosseum eneo la Oyster Bay, Dar es Salaam mwendo wa saa kumi na moja alfajiri.

Mfanyabiashara huyo alikuwa hana walinzi wowote na hata gari alilokuwa analitumia alikuwa anaendesha mwenyewe.

Watu wawili wasiofahamika ambao wanasemekana kuwa sio raia wa Tanzania (Wazungu), waliokuwa wameziba nyuso zao wakati walipofika kumteka katika hotelini.

Walioshuhudia walisema kuwa waliona risasi ikipigwa juu na akikamatwa kupelekwa katika gari la watekaji nyara hao na likaondoka.

Polisi wanadai kuwa Mo Dewji alitekwa na Wazungu wawili katika tukio ambalo lilihusisha magari mawili, jingine likiwa ndani na jingine nje ya uzio wa hoteli hiyo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema: "Asubuhi ya leo Wazungu wawili walikuwa na gari aina ya Surf. Kulikuwa na magari mawili, moja lilikuwa ndani na lingine nje, gari la ndani liliwasha taa ghafla na lile lililokuwa nje likaingia na kwenda kupaki karibu na gari la Mo Dewji lililokuwa limepaki."

"Na Mo akiwa ndani ya gari hilo Wazungu wawili wakatoka na kumbana Mo Dewji baada ya kutoka ndani ya gari lake na kisha kumpakia katika gari lao aina ya Surf kisha wakaondoka naye kusikojulikana."

Gazeti la Mwananchi limekuwa likimnukuu dereva mmoja wa magari ya teksi ya Uber aliyedai kushuhudia tukio hilo anayesema alisema aliwaona watekaji wanne walioficha nyuso ambao walimnyakua Mo kutoka ndani ya hoteli.

Walimtoa nje kabla ya kupiga risasi juu na kutokomea naye.

Gari moja lililotumiwa na watekaji, aina ya Toyota Surf, linadaiwa kuwa na nambari ya usajili AGX 404 MC, na dereva aliyeingia nalo Tanzania ni Obasanjo Zacharias Junior.

Kamanda Sirro amesema kwa kutumia kanda za kamera za CCTV polisi wamebaini kwamba gari hilo aina ya Surf baada ya kutoka hoteli ya Colosseum, lilipita barabara za Haile Sellasie, Ally Hassan Mwinyi, Maandazi, Mwai Kibaki na kisha likapotelea kwenye eneo la Mlalakuwa karibu na mzunguko wa Kawe.

Operesheni ya kumtafuta, na utata

Punde baada ya taarifa za kutekwa kwake, polisi walitangaza kuchukua hatua za kumtafuta kuhakikisha anapatikana akiwa hai.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda ni miongoni mwa waliozungumza na wanahabari siku hiyo kuhusu kutoweka kwa Mo, lakini badala ya taarifa yake kueleweka vilivyo, ikawa kwamba anadaiwa kusema Mo alikuwa amepatikana.

Ilimlazimu kukanusha hizo.

Bw makonda alikuwa amewaambia wanahabari kwamba habari sahihi au ambazo wengi wanazisubiri ni kwamba "Mo amepatikana, na wahalifu wametiwa mikononi mwa vyombo vyetu vya dola."

Wengi walichukulia hilo kuwa tangazo la kupatikana kwa Mo Dewji.

"Ninayo matumaini ya weledi na ukubwa wa jeshi letu la polisi na vyombo vyengine tutahakikisha ndugu tumepata akiwa salama," alisema.

Kamanda wa polisi wa kanda maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa naye alilazimika kupuuzilia mbali taarifa kwamba Mo Dewji alikuwa amepatikana eneo la Coco Beach.

"Zipo taarifa mtaani kwamba ameshapatikana, wengine wanadai kwamba amepatikana kule Coco Beach lakini taarifa kutoka meza yangu hii, na taarifa ambazo sasa ni taarifa rasmi, bado hajapatikana wala wahusika bado hawajakamatwa.

"Jeshi la polisi linaendelea na operesheni kali kufuatia tukio hilo, mikoa yote mitatu tunaendelea na ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha kwamba tukio hili ambalo ni la aina yake na ambalo limefanywa na raia wa kigeni halipati nafasi ya kuchafua taswira nzuri ya Tanzania kwa maana ya mahali ambapo wahalifu, vinaendelea kukemewa kwa pamoja.

"Mahali ambapo watu wameendelea kuita ni kisiwa cha amani."

Kukamatwa kwa watuhumiwa, na Haji Manara

Kufikia mwisho wa siku ya kwanza ya kutoweka kwa Mo, Bw Mambosasa alisema watuhumiwa waliokuwa wanashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo walikuwa wamefikia 12.

Siku iliyofuata, Msemaji wa Simba Haji Manara alikamatwa pia na kuzuiliwa kwa kile polisi walisema ni kutokana na kusambaza taarifa za tukio hilo la kutekwa kwa Mo kwenye mitandao kwa madai ya kutumwa na familia, bila kutumwa na familia hiyo.

"Hajatumwa na familia hivyo tunamshikilia," alisema Mambosasa wakati huo.

Jumanne wiki hii, Manara aliandika kwenye Instagram: Alhamdulillah.... kila jambo huja na sababu yake, na mitihani ya kilimwengu tumeumbiwa sisi binaadamu, naendelea kuwasihi tuviache vyombo vinavyohusika vitimize wajibu wao, kubwa tuendeleze dua na sala kwaajili ya kiongozi wetu InshaAllah.."

Jumamosi, waziri Lugola aliambia wanahabari kwamba watu 20 walikuwa wamekamatwa kuhusiana na kisa hicho na akawahakikishia Watanzania kwamba Jeshi la polisi nchini linaendelea kufanya kazi katika kuchunguza visa vya utekaji nyara.

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini Tanzania Simon Sirro Ijumaa alisema kufikia wakati huo ni watu wanane waliokuwa wanazuiliwa na polisi kuhusiana na kisa cha kutekwa kwa Mo.

Amesema watu wengine takriban 26 ambao walikuwa wanahojiwa wameachiliwa huru.

Miongoni mwa wale ambao bado wanazuiliwa kuna kapteni mmoja wa boti.

Zawadi ya Sh1 bilioni imezaa matunda?

Jumatatu wiki hii, familia ya Mohammed Dewji ambayo ilikuwa kimya siku za kwanza kwanza baada ya kutekwa kwake livunja ukimya na kusema watatoa kitita cha Sh1 bilioni kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazopelekea kupatikana kwa bilionea huyo.

Katika mkutano na waandishi wa habari, ami wa Mo, Azim Dewji alisema familia itazichukulia taarifa hizo kuwa kama za siri na pesa hiyo itakuwa zawadi kwa atakayezitoa.

"Familia inashukuru sana watu wote kwa kuendelea kututia nguvu na kumuombea kijana wetu Mohammed apatikane. Tunafarijika na ushirikiano na mshikamano wenu," alisema Dewji.

Familia hiyo iliwataka walio na habari kuwasiliana na mwanafamilia Murtaza Dewji kwa namba za simu au kutuma taarifa kupitia anwani ya barua pepe ya [email protected]

Lakini kufikia Jumatano, taarifa zilizokeza kwamba hakuna maelezo yoyote ambayo yemewasilishwa kwa familia hiyo.

"Hakuna tulichopata mpaka sasa ndugu yangu, familia bado tupo katika kipindi kigumu sana, nafikiri mzidi kutuombea jamani," alisema Azim Dewji, ambaye ni msemaji wa familia hiyo, amenukuliwa na Mwananchi.

"Samahani sana, nisingependa kulizungumzia hili mpaka nikae na familia. Baada ya hapo tunaweza kukutana na ninyi wiki ijayo labda tunaweza kuwaeleza kitu."

Magufuli amesema nini?

Rais John Magufuli hajatoa taarifa yoyote rasmi kuhusiana na kisa hicho cha utekaji nyara kufikia sasa.

Waziri wa mambo ya ndani nchini Tanzania Kangi Lugola anaonekana kuwa afisa wa ngazi ya juu zaidi anayehusika kuzungumzia utekaji huo.

Waziri mwingine, Januari Makamba, anayehusika na Muungano na Mazingira Tanzania, alikuwa siku ya kwanza ametoa tamko kupitia ukurasa wake wa Twitter na kusema alikuwa amezungumza na baba mzazi wa Mo ambaye amethibitisha kuwa mfanyabiashara huyo ametekwa.

"Nimetikiswa sana. Naamini polisi watatoa taarifa kamili. Mohammed ana familia na watoto wadogo. Tumuombee yeye na familia yake. Tusaidie kutoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwake," aliandika.

Maswali yanayogonga vichwa kuhusu utekaji wa Mo Dewji

Kuna maswali kadhaa ambayo yamekuwa yakijitokeza ambayo majibu yake yanaweza kutoa mwangaza wa kulielewa tukio lenyewe na pengine kupelekea kupatikana kwa tajiri huyo.

Kwa nini akatekwa? Baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa vimenukuu vyanzo kutoka jeshi la polisi Tanzania kuwa yawezekana kuwa Mo ametekwa kwa sababu za kifedha, ikihisiwa watekaji watadai kikombozi ili wamuachie huru.

Kutokana na utajiri alio nao (ambapo jarida la biashara la Forbes linakisia kuwa unafikia dola bilioni 1.5) ni jambo ambalo linayumkinika.

Nani walimteka? Hiki kimeendelea kuwa kitendawili kikubwa ikizingatiwa kuwa tajiri huyo hajawahi kuwa na rekodi ya 'kukwanguana' na watu kibiashara au kisiasa. Tangu alipostaafu ubunge Mo Dewji aliamua kukaa mbali na siasa na amekuwa makini kutoa kauli za kuunga mkono au kupinga maoni ama kundi lolote la siasa.

Hali kwamba inadaiwa magari mawili yalihusika, na wazungu pia, na ukubwa wake kwa sifa, ni wazi kwamba wahusika si watu wadogo.

Kamanda Mambosasa pia ameibua maswali manne ambayo yanaonesha utata mkubwa wa namna tukio hilo lilivyotekelezwa.

Aliambia Mwananchi kwamba maswali hayo ni.

1. "Hebu tujiulize kamera (iliyopo katika hoteli ya Colosseum) nayo imeshindwa kutupatia kila kitu kuna upande tumeshindwa kuupata vizuri tunajiuliza ilikwepeshwa makusudi?"

2. Kwa nini walinzi wa hoteli ambayo Mo alitekwa hawakuwahoji wahalifu ambao walifika kabla ya Mo kutaka kujua kwanini hawakushuka kwenye gari walilokuwemo.

3. "Tunaambiwa wakati zoezi linafanyika hakukupigwa yowe wala majibizano ya risasi ina maana hawa waliokuwa hapa walilichukuliaje tukio hili?"

4. Hakuna aliyeandika gari zinazoingia katika hoteli hiyo, "kwa hiyo hebu tufanye uchunguzi."

Godbless Lema kuhusu CCTV na usaidizi kutoka nje

Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani Godbless Lema Jumatano litaka jeshi la polisi kutoa picha za CCTV kwa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ambazo zinaonyesha tukio la kutekwa kwa bilionea Mohamed Dewji.

Mwanasiasa huyo alitoa wito pia kwa serikali kuomba kupokea msaada kutoka kwa wananchi na kutoka kwa mataifa ya nje.

"Baada ya kugundua kuwa waliomteka Mo ni wazungu wawili na wameonekana kwenye mkanda wa CCTV, na si polisi wanataka wananchi watoe ushirikiano? Chamuhimu una zitoa picha za video, hao wazungu tuwaone. Swali kwa nini wanaficha hizo picha za CCTV? Kwanini hata kwa (Tundu) Lissu kamera ilichukuliwa?," alihoji Lema.

"Ndio nasema serikali kujivua lawama kwenye maswala yote kwamba haihusiki ilete Scotland yard ama ilete mashirika mengine ya kiupelelezi duniani yaje yachunguze swala hili."

Hata hivyo, serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola imesema haitaomba usaidizi wa kiupelelezi juu ya mkasa wa kutoweka kwa Mo na mikasa mingine ikisema vyombo vya ulinzi vya ndani vinaweza kuitatua mikasa hiyo.

Mo Dewji ni nani?

Kwa mujibu wa jarida maarufu la masuala ya fedha la Forbes, ana utajiri wa dola bilioni 1.5.

Mo mwenye umri wa miaka 43 ndiye tajiri namba moja Afrika Mashariki, na pia miongoni ma matajiri wa umri mdogo zaidi Afrika.

Mohammed Dewji ni afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya METL iliyoanzishwa na baba yake miaka ya 1970.

METL ina viwanda vya kutengeneza nguo na bidhaa nyingine za matumizi ya binadamu vikiwamo vyakula, sabuni na vinywaji. Pia ina mapato yanayozidi Dola 1.4 milioni za Marekani (Sh2.5 trilioni) kwa mwaka.

Katika kampuni hiyo, ambayo imekuwa na ushindani dhidi ya kampuni kubwa nyingine kama Said Salim Bakhresa, Dewji anamiliki asilimia 75 ya hisa zote.

Kwa mujibu wa tovuti yake, METL inaendesha shughuli za uagizaji na usafirishaji bidhaa kutoka na kwenda nje, uzalishaji unaohusisha nguo, vinywaji na vyakula, usagaji nafaka, nishati na petroli na utengenezaji baiskeli.

Pia inahusika na huduma za simu, fedha, kilimo na pia ina kitengo cha kontena kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

METL ina shughuli zake katika nchi sita barani Afrika na ina malengo ya kujipanua zaidi katika maeneo zaidi.

Dewji ni mtanzania pekee aliyesaini mkataba mwaka 2016 wa kutoa kwa wahitaji nusu ya mali yake.

Mo Dewji Foundation ndio asasi ambayo aliianzisha ili kutekeleza nia yake hiyo na kazi yake kubwa ni kusaidia watanzania wasiojiweza kwa upande wa afya,elimu na maendeleo jamii.

Mbali na biashara na shughuli za jamii Mo Dewji amewahi kuwa mwanasiasa na mwaka 2005 mpaka 2015,Mohamed Dewji alikuwa mbunge wa Singida Mjini.

Dewji pia ni mpenzi wa michezo na amewekeza katika klabu ya mpira ya Simba ya Tanzania.