Magufuli akutana na mkurugenzi wa Benki ya Dunia, kimya bado kuhusu msaada wa $50m

Magufuli alipokutana na Bi Bird miaka miwili iliyopita

Chanzo cha picha, IKULU, Tanzania

Maelezo ya picha, Magufuli alipokutana na Bi Bird miaka miwili iliyopita

Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli amekutana na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini humo kuzungumzia miradi mbalimbali inayofadhiliwa na benki hiyo.

Hata hivyo, utata bado unaendelea kuhusu msaada wa dola 50 milioni za Marekani ambazo benki hiyo ilikuwa inatarajiwa kutoa kwa taifa hilo.

Taarifa iliyotumwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu baada ya mkutano huo inaeleza kuwa Rais Magufuli na Bi Bella Bird walizungumzia miradi mbalimbali ambayo imo njiani, lakini mkazo kwenye taarifa hiyo umewekwa kwenye sekya ya elimu ya awali na ya sekondari.

Bi Bird amenukuliwa akisema kuwa kwa sasa wanakamilisha maandalizi ya ufadhili wa miradi mingine inayohusu sekta ya elimu hasa elimu ya awali na sekondari, itakayogharimu shilingi Trilioni 1.357, na kwamba maandalizi hayo yatakamilika mwezi ujao.

Bi Bird alipokutana na Rais Magufuli katika Ikulu jijini Dar es salaam Jumanne

Chanzo cha picha, IKULU, Tanzania

Maelezo ya picha, Bi Bird alipokutana na Rais Magufuli katika Ikulu jijini Dar es salaam Jumanne

Kwa jumla, miradi inayotekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia nchini Tanzania kwa mujibu wa Bi Bird imefikia thamani ya shilingi Trilioni 10.186.

Maendeleo ya miradi hiyo ni mazuri, taarifa hiyo imemnukuu Bi Bird.

"Kwa hiyo nimekutana na Mhe. Rais Magufuli kuzungumzia maendeleo ya miradi hiyo na kwa ujumla maendeleo ni mazuri," amesema Bi. Bella Bird, kwa mujibu wa benki hiyo.

Taarifa kuhusu msaada

Wiki iliyopita, Benki ya Dunia ilitoa taarifa ikisema imesikitishwa sana na marekebisho ya sheria yanayopendekezwa kufanywa kwenye Sheria ya Takwimu ya 2015.

Benki hiyo ilisema sheria hizo haziendani na viwango vya kimataifa vilivyowekwa kuhusu takwimu.

"Tumeifahamisha serikali ya Tanzania kwamba marekebisho hayo, iwapo yatatekelezwa, huenda yakaathiri sana kuandaliwa kwa takwimu rasmi na zisizo rasmi, ambazo huwa muhimu sana kwa ustawi wa taifa lolote lile," benki hiyo ilisema.

"Ni muhimu sana kwa Tanzania, sawa na taifa jingine lolote, kutumia sheria za takwimu kuhakikisha takwimu rasmi ni za kiwango cha juu zaidi na za kuaminika na pia kulinda uwazi na uwajibikaji katika matumizi yake, kuendeleza mjadala kwa manufaa ya raia."

Kutokana na hilo, benki hiyo imesema: "Benki ya Dunia inajadiliana na serikali kuhusu utoaji wa msaada zaidi katika kujenga mifumo ya takwimu endelevu unafaa kwa wakati huu."

Mkutano wa leo umefanyika kukiwa na utata kuhusu msaada wa $50m

Chanzo cha picha, IKULU, Tanzania

Maelezo ya picha, Mkutano wa leo umefanyika kukiwa na utata kuhusu msaada wa $50m

Ingawa benki hiyo ilisema mashauriano yanaendelea na kwamba wameeleza wasiwasi wake kuhusu sheria hiyo ya takwimu, hawakusema wazi kwamba wamesitisha mradi huo nambari P167066.

Kadhalika, kiasi hicho cha $50 milioni bado kimeorodheshwa kwenye tovuti ya benki hiyo kama msaada unaopangiwa kutolewa kwa Tanzania, ingawa mpango huo bado haujaidhinishwa, bado upo kwenye utaratibu.

Benki ya Dunia ilikuwa imetumia kiasi cha $ 63.18 milioni kama msaada kuimarisha uwezo wa mfumo wa takwimu wa serikali Tanzania kufikia Juni 30,2018 chini ya mradi ambao ulikuwa umeidhinishwa mwaka 2011.

Agosti, waliidhinisha kiasi kingine cha $ 8.56 milioni.