Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
MV Nyerere: Kenyatta atoa Sh125m kwa Watanzania kama rambirambi mkasa wa kivuko, mhandisi amkosoa Magufuli
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametoa Sh125 milioni kwa mwenzake wa Tanzania Dkt John Magufuli kama rambirambi kufuatia mkasa wa kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere mwezi jana.
Watu 228 walifariki na wengine wengi kujeruhiwa katika mkasa huo uliotokea tarehe 20 kivuko cha MV Nyerere kilipokuwa safariki kuelekea kisiwa cha Ukara kutoka kisiwa cha Ukerewe.
Mchango huo wa Rais Kenyatta umewasilishwa kwa Rais Magufuli na balozi wa Kenya nchini tanzania Dkt Dan Kazungu aliyekutana na kufanya mazungumzo naye ikulu Dar es Salaam.
Rais Magufuli amemshukuru rais Kenyatta na akaahidi kwamba fedha zilizotolewa na Rais Kenyatta zitatumiwa kuwasaidia wananchi wa visiwa vya Ukerewe, ikiwa ni pamoja na kuchangia kujenga hospitali ya hadhi ya wilaya.
Adokeza kwamba huenda wodi moja katika hospitali hiyo ikapewa jina la kiongozi huyo wa Kenya.
"Mwambie Mhe. Rais kuwa nashukuru sana, tulipanga fedha tulizopata tjenge wodi za wagonjwa lakini sasa tumeamua tujenge hospitali kubwa yenye hadhi ya wilaya," amesema Rais Maufuli.
"Na kwa mchango huu, tunaweza kuamua wodi moja tukaiita Wodi ya Kenyatta."
Mhandisi atofautiana na Magufuli
Hayo yamejiri huku Mhandisi wa Kivuko cha MV Nyerere, Alphonse Agustine Charahani aliyekaa majini kwa zaidi ya saa 48, akizungumza na wanahabari na kusema nahodha aliyekuwa zamu kivuko hicho kilipopinduka ni msomi na mtaalamu mzoefu na si kibarua kama inavyodaiwa.
Kwa mujibu wa gazeti la kibinafsi la Mwananchi, mhandisi amesema, nahodha huyo Abel Constatine Mahatine ambaye pia alifariki, alikuwa mhitimu na alikuwa amefanya shughuli hiyo kwa zaidi ya miaka 10.
"Hayo madai kwamba marehemu alikuwa 'deiwaka', nimekuja kuyasikia hapa nje. Kwa nini watu wasijiulize kwamba 'deiwaka' angepataje fursa ya kupeleka chombo kama kile kwa muda mrefu kiasi hicho?"
Kauli yake inaonekana kutofautiana na tamko la Rais Magufuli baada ya ajali hiyo, ambapo alisema kwenye hotuba ya moja kwa moja kwa taifa kwamba alikuwa amefahamishwa kwamba nahodha aliyefaa kuwa kazini alimwachia zamu ya kuendesha chombo hicho mtu ambaye hakuwa amepata mafunzo ya kazi hiyo.
Rais Magufuli alisema kuwa nahodha huyo alikuwa tayari amekamatwa na polisi nakwamba wote waliohusika na shughuli za kivuko hicho wangekamatwa ili kuhojiwa.
Mhandisi amesema hana sababu maalum ya kuikacha kazi ya uhandisi majini.
"Hii ni ajali kama nyingine na siwezi kusema kwamba nimeacha kuwa mhandisi, hii ni mipango ya Mungu ukizingatia maili chache zilizokuwa zimebaki kabla ya kivuko kutia nanga," amesema, na kuongeza kwamba ilikuwa ni mwujiza kwake kuokolewa.
Kuhusu chanzo cha ajali, ameambia Mwananchi kwamba anaamini ulikuwa mkosi tu.
"Siwezi kusema moja kwa moja kwamba ninajua sababu ya kuzama kwa MV Nyerere lakini tu nahisi ni bahati mbaya baada ya nahodha kupotea kidogo na kutoka kwenye mstari. Nadhani katika kushtuka kwake ndipo aligeuza kivuko ghafla na kusababisha uzito kuelekea upande mmoja. Sina uhakika lakini," amesema Alphonse.