Jamii zinazokula panya kama kitoweo Pwani ya Kenya

Panya

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Panya
    • Author, John Nene
    • Nafasi, BBC Swahili

Baadhi ya Jamii ya Wa mijikenda wanaoishi Pwani ya Kenya wanaamini kwamba kula nyama ya panya kutakuepusha na visirani pamoja na mikosi.

Mzee Vue Taura, mwenyeji wa kijiji cha Mbudzi katika eneo la Kilifi, nchini Kenya, anasema nyama ya panya ni kitoweo kitamu na muhimu sana wakaazi wa kijiji hicho.

Anasema nyama ya panya inawakinga dhidi ya wachawi na majini.

"Panya ni kama sumu kwa majini kwa sababu hawawezi kukukaribia. Majini ni kama pepo na yanasumbua sana ukitumiwa unaweza kuenda hospitali lakini usipate tiba.

Wachawi pia tunajiepusha nao kwa kutumia panya."

Mzee Taura anasema mambo hayo yamekuwepo tangu enzi ya mababu zao na wao pia wanaendeleza utamaduni huo.

''Sisi pia tuliyakuta na wala sio ushirikina, ni mambo ambayo yanafanyika."

Miongoni mwa jamii ya mijikenda wanaokula nyama ya panya ni wakauma, wachonyi, wagiriama na wakambe.

Wenyeji wa kijiji cha Mbudzi wakielezea umuhimu wa kula nya ya panya
Maelezo ya picha, Wenyeji wa kijiji cha Mbudzi wakielezea umuhimu wa kula nya ya panya

Mama Eunice, mmoja wa wakaazi wa kijiji cha Mbudzi anaunga mkono kauli ya mzee Taura.

Anasema kuwa yeye binafsi amekula nyama ya panya tangu akiwa mdogo hadi sasa ana miaka 65.

Mama Eunice anasema,''Nyama ya panya inatukinga na magonjwa mengi sikumbuki mara ya mwisho nimeenda hospitali''.

Kwa mujibu wa wakaazi wa kijiji cha Mbudzi, panya wanaoliwa ni wale wana wasumbua watu majumbani na wale wanaoharibu mimea shambani.

Shingila Mbitsi ni mtegaji panya.

Kama kazi nyingine yoyote, imemsaidia kujikimu kimaisha na pia kusomesha watoto wake.

Mwindaji panya
Maelezo ya picha, Shingila Mbitsi ni mtegaji panya

Anasema amejifunza kazi hiyo kutoka kwa babu yake.

''Babu yangu alikua anawinda panya anawaleta kwa wingi, wengine tulikuwa tunakula na wengine anauza ili apate pesa ya matumizi."

Shingila anasema kuwa anakumbana na changamoto nyingi katika kazi yake ya utegaji panya hasa wakati kuna chakula cha kutosha shambani.

"Wakati wa ukame ndio ninapata wengi kwa sababu wanajitokeza kutafuta chakula.

Ukiweka mahindi katika mtego wanajileta wenyewe na kuingia. Wakati mwingine naweza kupata zaidi ya panya thelathini''.

Shangilia anasema yeye na wenzake huwatega panya usiku. Mtegaji anaweza kukaa kichakani usiku wote hadi asubuhi.''Msimu uliyo na panya wengi ni mwezi wa Disemba."

Pia anasema mvua ni adui mkubwa kwa wategaji panya kwa sababu wakati huo hawatoki katika maficho yao.