Trump: Mazoezi ya kijeshi na Korea Kusini yatakuwa makubwa zaidi

Rais wa Marekani Donald Trump ameikosoa China kwa kuhujumu jitihada zake na Korea Kaskazini, wakati kuna malalamiko kuhusu maendeleo ya kuharibu silaha za nyuklia za Korea Kaskazini.

Kupitia ujumbe wa Twitter alisema hakuna sababu ya kutoendelea tena na mazoezi ya kijeshi na Korea Kusini ambayo yamekuwa yakiikasirisha Korea Kaskazini.

Siku zilizopita waziri wake wa ulinzi alisema mazoezi ya kijeshi yanaweza kuendelea.

China imeikosoa Marekani kwa kuilaumu kuhusu uhusiano wake na Korea Kaskazini.

Mkutano kati ya Bw Trump na kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong-un mwezi Juni ulikamilika kwa ahadi kutoka Korea Kaskazini kufanya kazi katika kuharibu silaha za nyuklia kwenye rasi na Korea.

Baadaye Trump alitangaza kuwa hakukuwa tena na tisho kutoka Korea Kaskazini.

Lakini tangu wakati huo waangalizi wengi wanasema kuwa Korea Kaskazini haifanyi hima katika kuharibu maeneo yake ya kurushia makombora.

Kwa nini anailaumu China?

Kwenye matamshi yake kupitia Twitter, Bw Trump anasema Korea Kaskazini iko chini ya shinikizo kutoka China kwa sababu ya mvutano wa kibiashara kati ya Marekani na serikali ya China.

China ndiyo mshirika pekee wa Korea Kaskazini na inatajwa kuwa na ushawishi mkubwa kwenye maamuzi yake. China pia ndiye mshindani mkubwa wa Marekani na wa muda mrefu eneo hilo.

Marekani na China ziko kwenye mvutano mkuwa wa kibiashara na kila upande umeziwekea ushuru bidhaa za mwingine.

Hatua gani zimepigwa katika kuharibu silaha za nyuklia?

Tangu mkutano wa Juni, Korea Kaskazini imesitisha majaribio yake ya nyuklia, ikidai kuharibu kituo cha kufanyika majaribio ya nyuklia na ikarudisha mabaki ya wanajeshi wa Marekani waliouawa wakati wa vita vya Korea kati ya mwaka 1950-53.

Bw Trump ameilaumu Korea Kaskazini kwa kile amekitaja kuwa kutokuwepo hatua katika makubaliano yake ya kuharibu silaha za nyuklia.

Ripoti ya hivi majuzi ya Vox ilisema Korea Kaskazini ilijikokota kusonga mbele baada ya Trump kushindwa kutekeleza ahadi zake kwa Bw Kim, kuwa angeweka sahihi mukubaliano ya kumaliza vita vya Korea.

Baada ya ripoti ya Umoja wa Mataifa kupata kuwa Korea Kaskazini ilikuwa inandelea na mipango yake ya nyuklia, Marekani iliitaka jamii ya kimaifa kudumisha vikwazo vya kiuchumi na Korea Kaskazini.

Mazoezi ya kijeshi yatarudi?

Mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya Marekani na Korea yameikasirisha kwa siku nyingi Korea Kaskazini.

Kufuatia mkutano wa Juni Bw Trump alisimamisha mazoezi hayo ya kijeshi.

Katika ujumbe wake wa hivi majuzi, rais wa Marekani alisisitiza kuwa uhusiano wake na Kim ulibaki kuwa mzuri na hakukuwa na sababu ya kuanzisha tena mazoezi ya kijeshi na Korea Kaskazini.

Lakini aliongeza kuwa ikiwa yataanza yatakuwa makubwa kuliko yoyote yale.

Tangu kumalizika vita vya Korea, wakati Marekani ilishirikiana na Korea Kusini kuipiga vita Korea Kaskazini, Marekani imekuwa na wanajeshi wake nchini Korea Kusini.

Karibu wanajeshi 29,000 wa Marekani wako nchini Korea Kusini chini ya makubaliano ya ulinzi yaliyofikiwa mwaka 1953.