Bobi Wine: Mbunge na mwanamuziki nyota aachiliwa huru kwa dhamana Uganda

Muda wa kusoma: Dakika 4

Mwanamuziki mwanasiasa Bobi Wine ambaye amekuwa akizuiliwa kwa karibu wiki mbili nchini Uganda pamoja na wanasiasa wengine 32 wa upinzani wameachiliwa huru kwa dhamana na Mahakama Kuu mjini Gulu, kaskazini mwa nchi hiyo.

Mbunge huyo wa Kyadondo Mashariki ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi amepewa dhamana pamoja na wabunge wengine watatu, na watuhumiwa wengine wanane.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuhusika katika kurushia mawe magari ya msafara wa Rais Yoweri Museveni wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Arua.

Kassiano Wadri aliyeshinda ubunge Arua ni miongoni mwa wabunge waliokuwazuiliwa.

Bw Wadri ameachiliwa kwa dhamana lakini akazuiwa kuzuru eneo bunge lake kwa miezi mitatu bila idhini ya mahakama.

Maombi ya dhamana ya washukiwa wengine 21 walioshtakiwa pamoja na Bobi Wine yatasikilizwa na mahakama baadaye leo.

Awali, taarifa zilikuwa zimesema kuwa wakili wa kimataifa aliyekuwa amepewa kazi ya kumwakilisha, Bobi Wine, amezuiwa kuingia nchini humo.

Gazeti la kibinafsi la the Monitor nchini humo limeripoti kuwa Robert Amsterdam ameorodheshwa kama mtu asiyetakikana nchini Uganda na serikali ya nchi hiyo.

Alikuwa miongoni mwa mawakili waliokuwa wameorodheshwa kumtetea Bw Kyagulanyi katika kesi ambapo ameshtakiwa uhaini.

Gazeti la kibinafsi la the Monitor nchini humo limeripoti kuwa Robert Amsterdam ameorodheshwa kama mtu asiyetakikana nchini Uganda na serikali ya nchi hiyo.

Alikuwa miongoni mwa mawakili waliokuwa wameorodheshwa kumtetea Bw Kyagulanyi katika kesi ambapo ameshtakiwa uhaini.

Jukumu la Bw Amsterdam lilikuwa kufanya masuala ya kiufundi, kutoa ushauri na pia kusaidia katika kufanya utafiti.

Wakili huyo ni raia wa Canada lakini huendesha shughuli zake kupitia kampuni ya Amsterdam & Partners iliyo na afisi Washington na London.

Raia wa Uganda wamepokeaje kuachiwa kwa Bobi Wine?

Wengi wameonekana kupokea taarifa za kuachiliwa kwa Bobi Wine kwa furaha kubwa.

'Kwa kweli inaleta furaha, hiyo ni ishara tosha kwamba huenda akachiliwa huru kabisa na akiachiliwa huru basi ina maana ataweza kuendelea kutupigania haki zetu sisi ki urahisi kuliko akiwa ndani. Mara nyingi watu ndio huwa wana nguvu, watu mukiwa wengi munasikika zaidi kuliko mtu ukiwa mmoja' alisema mkaazi mwanamke mmoja mkaazi wa Kampala.

'Mimi naskia vizuri kwani amepitia wakati mgumu sana na kipindi kigumu mfano ukienda mita aya Kamoja, watu wengi wanafurahia Bobi Wine kuwa huru, yaani kila mtu anafurahi' amesema mkaazi mwingine baada ya taarifa za kuachiwa kwa Bobi Wine kusambaa katika vyombo vya habari.

Mkewe Wine, Barbie, aliweka ujumbe huu leo kuadhimisha miaka 7 ya ndoa yao terehe iliyoangukia siku sawa na kuachiliwa kwa mbunge huyo wa Kyadondo.

Bobi Wine amekuwa akizuiliwa rumande katika gereza la Gulu pamoja na watuhumiwa wengine 33, miongoni mwao wabunge.

Maafisa wakuu wa serikali Uganda kufikia sasa bado hawajazungumzia taarifa hizo.

Bw Medard Sseggona, mmoja wa mawakili Kyagulanyi amesema hatua ya kumzuia Bw Amsterdam kuingia nchini humo si ya busara, na inaweza tu kuashiria kwamba serikali imeanzakuingiwa na wasiwasi.

Bw Amsterdam katika makala iliyochapishwa kwenye vyombo vya habari Uingereza Jumamosi alikuwa amezungumzia kukamatwa na kuzuiliwa kwa wabunge Uganda na kimya cha jamii ya kimataifa.

Kwenye gazeti la The Guardian, alitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuwawekea vikwazo watu wanaohusika katika ukiukaji wa haki za kibinadamu nchini Uganda.

"Vikwazo kama hivi vinaweza kufanikiwa vyema katika kuzuia ukiukaji wa haki za kibinadamu siku za usoni, na kuzuia madhara zaidi kwa raia wasio na hatia," aliandika.

Mlinzi kukamatwa

Gazeti la serikali la Vision siku ya Jumamosi liliripoti kuwa mlinzi wa Bobi Wine Eddy Ssebuufu alikuwa amekamatwa, lakini polisi na jeshi wote walijitenga na taarifa hizo.

Dereva wa mbunge huyo alifariki baada ya kupigwa risasi wakati wa rabsha zilizozuka wakati wa kampeni.

Bw Bobi Wine alisema waliomuua dereva wake walikusudia kumuua yeye mwenyewe.

Mbunge huyo alikuwa amezuiliwa katika mahakama ya kijeshi ambapo alikuwa ameshtakiwa kosa la kuwa na silaha kinyume cha sheria lakini mashtaka hayo yanaondolewa Alhamisi.

Alikamatwa muda mfupi baadaye na kufunguliwa mashtaka katika mahakama ya kiraia.

Bobi Wine ni nani hasa?

Nyota huyu wa mtindo wa Afrobeats aliingia katika taaluma ya muziki katika miaka ya 2000, na anaelezea kipaji chake kuwa ni cha kuelimisha na kuburudisha. Mojawapo ya vibao vyake vya awali Kadingo, inahusu usafi wa mwili.

Alizaliwa 12 Februari 1982, Bobi Wine na alikuwa na miaka minne pekee Museveni alipoingia madarakani mwaka 1986.

Jina lake rasmi Wine, ni Robert Kyagulanyi Ssentamu.

Alilelewa katika mtaa duni wa Kamwokya kaskazini mashariki mwa Kampala na alianza kujihusisha katika muziki mapema miaka ya 2000.

Nyimbo zake za mtindo wa dansi za 'Akagoma' na 'Funtula' zilikuwa maarufu sana miongoni mwa vijana.

Ana shahada ya muziki, dansi na uigizaji kutoka Chuo Kikuu cha Makerere ambapo alihitimu mwaka 2003.

Aprili 2018 alifuzu na stashahada ya masuala ya kisheria kutoka Kituo cha Maendeleo ya Sheria, Kampala.

Alichaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi mdogo baada ya kusimama kama mgombea huru mwaka 2017 wilayani Kyadondo mashariki, Uganda ya kati.

Aliwashinda wagombea kutoka chama tawala National Resistance Movement (NRM) na chama kikuu cha upinzani Democratic Change (FDC).

Baada ya kutangazwa mshindi, aliahidi kuangazia zaidi kuwaunganisha raia.

"Jambo langu la kwanza ninalotaka kufanya ni kufanikisha maridhiano kati ya viongozi wa Kyadondo Mashariki...Ninataka siasa zitulete pamoja... jinsi muziki ufanyavyo."