Je,kesi za Bobi Wine na Kale Kayihura zina msukumo wa kisiasa?

Mahakama ya jeshi nchini Uganda imekumbwa na tuhuma za kufanya maamuzi yake kutokana na msukumo wa kisiasa mara baada ya wiki hii kusikiliza mashtaka ya mbunge ambaye pia mwanamuziki nchini Uganda Robert Kyagulanyi jina maarufu Bobi Wine.

Hii leo, mahakama hiyo ya jeshi pia imeanza kusikiliza kesi ya aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la polisi nchini Uganda IGP - Kale Kayihura. Kayihura anashtakiwa kwa kosa la kushindwa kulinda zana za kivita katika kipindi cha mwaka 2010 mpaka 2018 wakati ambapo anatuhumiwa kuidhinisha silaha zitolewe kwa watu wasiostahili na kuhatarisha usalama wa wananchi na mali zao.

Tuhuma hizo zilisababisha kiongozi huyo kuachishwa kazi na Rais Yoweri Mseveni mwezi machi mwa ka huu na baadae mwezi juni alishikiliwa na jeshi la Uganda mpaka leo hii alipopandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza kukabiliana na tuhuma hizo.

Kayihura anatarajiwa kurudi tena mahakamani tarehe 4 Septemba licha ya kwamba alikana mashtaka yote yanayomkabili.

Kwa upande wa mbunge asiye na chama Bobi Wine yeye alishtakiwa na jeshi kwa mashtaka ya kumiliki silaha kinyume cha sheria, mahakama hiyo baadae ilimuachia huru lakini alikamatwa tena na kufunguliwa mashtaka ya uhaini katika mahakama ya kiraia.

Tofauti kati ya mahakama ya kijeshi na kiraia ni ipi?

Tofauti ya msingi kati ya mahakama ya kijeshi na mahakama ya kiraia ipo katika utaratibu wa uendeshaji wa kesi.

Mahakama za jeshi kwa mataifa ya jumuiya ya madola kazi yake ni kuangalia makosa ya wanajeshi kwa kuhakikisha nidhamu inazingatiwa na kushughulikia mashitaka ya makosa ya kivita.

Katika mahakama ya kijeshi ,kesi zake huwa hazina uwazi na hata utoaji wa adhabu utegemea na utashi wao na sio demokrasia.

Watendaji wa kazi wa mahakama za kijeshi ni askari wenyewe tofauti na mahakama za kiraia.

Ronnie Mulindwa ambaye ni wakili nchini Uganda anasema hata kwa upande wa Uganda utaratibu ni huohuo kwamba mahakama ya kijeshi ni kwa ajili ya wanajeshi lakini raia anaweza kuhukumiwa na mahakama hiyo pale aendapo atakutwa na kesi ya kuwa na silaha za kijeshi au vitendea kazi vyovyote vya kijeshi kama sare .

Jambo ambalo kwa upande wake Bobi Wine ambaye si askari alishtakiwa kwa kosa hilo licha ya kwamba ushaidi waliodai kuwa nao ulikuwa unaleta mgongano.

Lakini vilevile hata kwa upande wa Kayihura yeye alikuwa askari polisi na hakuwa mwanajeshi.

Mchambuzi wa siasa za kimataifa na diplomasia ndugu Godluck Nyingo kutoka Tanzania amesema hata wa upande wa wanajeshi wenyewe hawawezi kushtakiwa katika mahakama za kiraia labda mpaka pale askari akivuliwa wadhifa wake wa askari ndipo anaweza kuhukumiwa katika mahakama ya kiraia.

Lakini pamoja na hayo kwa mujibu wa sheria za Uganda ibara ya 19 inasema mtu yeyote atakayekutwa na silaha za kijeshi basi kesi yake itasikilizwa na mahakama ya kijeshi.

Ingawa katika Ibara ya 120 ya nchini Uganda inasema haiwezi kushtaki raia katika mahakama ya kijeshi hivyo inaonekana wazi sheria yao wenyewe inakingana.