Ziara ya Theresa May ina umuhimu gani Afrika?

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May, anajiandaana kwa safari yake ya kwanza barani Afrika tangu aingie madarakani mwaka 2016.

Ziara yake Bi May itaanza Afrika Kusini siku ya jumanne kabla hajasafiri kwenda Nigeria na Kenya zikiwa miongoni mwa miradi wanayolenga kuinua utajiri wa Brexit.

Waziri mkuu anasema safari hii itakuwa ni ya mafanikio na vilevile inatoa fursa ya kipekee kwa Uingereza.

Bi.May aliongeza kusema kuwa Uingereza imetaka kusisitiza na kuimarisha uhusiano wake na washirika wake kabla hajaondoka madarakani mwaka 2019.

Bi May ataongozana na wafanyabiashara 29 wakubwa katika nchi zote tatu ambazo ni za jumuiya ya madola

Suala la usalama pia litakuwa miongoni mwa ajenda ambazo zinatarajiwa kujadiliwa kama vile suala la vitisho vya Boko Haram nchini Nigeria na ngome ya Uingereza ambayo iko nchini Kenya ambazo wanasaidiana kukabiliana na wanamgambo wa alshabab nchini Somalia.

Ratiba ya Waziri mkuu wa Uingereza

Jumanne;Bi.May atasafiri kwenda Afrika Kusini na kufikia mji wa Cape Town ambapo atakutana na vijana kabla hajawasilisha tamko rasmi juu ya biashara na namna ambavyo wawekezaji binafsi ambao unaweza kuletwa barani Afrika.

Baada ya mkutano huo anategemewa kukutana na rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa na baadae anatarajiwa kutembelea kisiwa cha Robben eneo ambalo Nelson Mandela alifungwa.

Jumatano;Bi May anatarajiwa kukutana na rais wa Nigeria Muhammadu Buhari katika mji mkuu wa Abuja kabla hajakutana na watumwa waliopo mjini Lagos.

Alhamisi -Nchini Kenya ,bi.May anategemea kukutana na rais Uhuru Kenyatta kabla ya kuwatembelea askari wa Uingereza na shule ya biashara .Na ziara yake itamalizika kwa kula chakula cha pamoja na rais Kenyatta.

Ziara ya bi.May mjini Nairobi itakuwa ni ugeni wa mara ya kwanza kwa waziri mkuu wa Uingereza tangu mwaka 1988 alipotembelea Margaret Thatcher.

Itakuwa mara ya kwanza kwa taifa la ukanda wa jangwa wa Afrika kutembelewa na kiongozi huyo tangu David Cameron alipohudhuria mazishi ya Mandela mwaka 2013.

Bi.May amesema mafanikio na ukukua wa biashara una maslahi kwa wote na ukiongeza manufaa ambayo yanaweza kupatikana kutokana na uhusiano huu kati ya serikali ,taasisi za kimataifa na biashara.

Msemaji wake aliongeza kwamba waziri mkuu atatumia ziara hii kutangaza msaada zaidi ili kuwezesha kukabiliana na hali ya kiusalama katika bara hili kwa sababu nchi haiwezi kuendelea kama itakuwa katika migogoro.

Katika ziara yake nchini Afrika ya Kusini Bi.May atawasilisha matokeo ya vita ya kwanza inayohusisha wakati mgumu ambao uliwahi kutokea majini.

Ziara ya Uingereza barani Afrika ina umuhimu gani?

Mchambuzi wa wa masuala ya sera za kigeni ,ndugu Heristides Kabendera kutoka chuo kikuu cha Kampala University jijini Dar es salaam anasema ziara hii ambayo inakuja yawezekana kwamba haina jipya zaidi ni kutegemea namna ambavyo mataifa ya Afrika yatakaupokea ujio huu.

Bwana Kabendera anasema inawezekana kuwa huu ni muendelezo tu wa itikadi zao za kutafuta masoko na malighafi na sasa ni wakati muafaka ambapo mataifa ya Afrika yanapaswa kujifunza kwamba ile zama ya kupokea misaada imekwisha hivyo kama tumeamua kuwa na uhusiano nao kibiashara basi tuone namna gani nzuri ambayo tunaweza kutumia fursa ili kujiletea maendeleo.

Mara nyingi mahusiano ya nchi tajiri na nchi maskini huwa ni ya unyonyaji, tofauti na uhusiano ambao labda walikuwa nao katika mataifa ya ulaya.

Na vilevile ukiangalia mataifa haya matatu (Kenya,Nigeria na Afrika Kusini )yana uchumi wa kati ambapo viongozi wake wakitumia fursa vizuri basi Afrika tunaweza kufaidika.

"Inabidi tuangalie wale wana nini na sisi tuna nini ,hatuhitaji miaka mia kujifunza ,miaka 60 inatutosha kujua mbinu zao,"bwana Kabendera alieleza.