Chama cha Upinzani MDC Alliance kinasema Chamisa amemshinda Mnangagwa

Wafuasi wa mgombea wa Upinzani Nelson Chamis

Chanzo cha picha, AFP

Upinzani nchini Zimbabwe unasema kuwa mgombea wake wa urais Nelson Chamisa, ameshinda uchaguzi mkuu wa Jumatatu.

Chama cha upinzani cha MDC kinasema kuwa chama tawala cha Zanu-PF kinajaribu kufanya udanganyifu ili kumruhusu Emmerson Mnangagwa kushinda , na kucheleweshwa kutolewa kwa matokeo hakutakubalika.

Tume ya uchaguzi nchini humo imesema kuwa hakuna udanganyifu na inahitaji muda ili kuhesabu kura hizo.

Uchaguzi huo ni wa kwanza tangu rais wa zamani Robert Mugabe kuondolewa kwa nguvu madarakani.

Akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari mjini Harare, Tendai Biti wa chama cha MDC Alliance amesema kuwa kuna jaribio la wazi linalofanywa na Zanu-Pf kuingilia chaguo la wananchi.

Zanu-Pf ambacho kimekuwa madarakani tangu 1980 kimeshutumiwa kufanya udanganyifu katika miaka ya nyuma ili kumweka Mugabe madarakani.

Hatahivyo msemaji wa chama amesema kuwa hajui kile bwana Tendai Biti anachozungumzia .

Shuguli ya kuhesabu kura inaendelea katika maeneo mbali mbali nchini Zimbabw

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Shuguli ya kuhesabu kura inaendelea katika maeneo mbali mbali nchini Zimbabwe huku matokeo ya mwanzo yakianza kutolewa

Awali wagombea wakuu katika uchaguzi wa Zimbabwe walituma ujumbe wao wa twitter kila mmoja akionyesha matumaini yake ya kupata ushindi.

Rais Emmerson Mnangagwa, ambae alichukua mamlaka baada ya kuondolewa madarakani kwa Robert Mugabe, alisema kuwa anapokea taarifa "nzuri sana" kuhusu kura za uchaguzi.

Wakati shughuli ya kuhesabu kura ikiendelea kote nchini Zimbabwe waandishi wa BBC walioko mjini Harare wanasema hali ya maisha imerejea kuwa ya kawaida huku wafanyabiashara wa mitaani na wenye maduka wakirejea kazini.

Rais Emmerson Mnangagwa (kushoto) pamoja na Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe , Nelson Chamisa (kulia)
Maelezo ya picha, Rais Emmerson Mnangagwa (kushoto) pamoja na Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe , Nelson Chamisa (kulia) kwa pamoja wametangaza kuwa watashinda uchaguzi

Lakini kuna hali ya ukimya huku watu wakisubiri matokeo katika uchaguzi huo wenye upinzani mkali.

Maafisa wanahesabu kura kwa mikono na kuzihakiki.

Bado hata hivyo viongozi waliotangazwa wazi kupata ushindi licha ya kwamba vyombo vya habari vya ndani ya nchi vinatuma matokeo kutoka vituo mbali mbali vya uchaguzi kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii.

Rais Emmerson Mnangagwa ametuma ujumbe wa Twitter akiwataka watu kusubiri matangazo rasmi kutoka kwa Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe (Zec).

Shuguli ya kuhesabu kura inaendelea katika maeneo mbali mbali nchini Zimbabw

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Shuguli ya kuhesabu kura inaendelea katika maeneo mbali mbali nchini Zimbabwe huku matokeo ya mwanzo yakianza kutolewa

Matokeo ya awali kutoka maeneo ya vijijini yanatarajiwa kuupatia ushindi upinzani, licha ya kwamba kwa kawaida maeneo hayo yamekuwa yakikiunga mkono chama tawala cha Zanu-PF.

Asilimia 75% ya wapigakura walijitokeza ushiriki uchaguzi huo mkuu wa kwanza kufanyika nchini Zimbabwe tangu kung'olewa madarakani kwa mtawala wa muda mrefu Robert Mugabe , maafisa wanasema.

Matokeo ya uchaguzi yanatazamiwa kuwa ya mchuano mkali baina ya rais aliyepo madarakani Emmerson Mnangagwa na hasimu wake mkuu, Nelson Chamisa.

Baadhi ya raia wa Zimbabwe waliojitokeza kushiriki uchaguzi mkuu
Maelezo ya picha, Baadhi ya raia wa Zimbabwe waliojitokeza kupiga kura ... 75% ya raia wa Zimbabwe walishiriki uchaguzi huo mkuu

Wachunguzi wa Kimataifa wa uchaguzi wa wameusifu uchaguzi huo na kuutaja kama fursa kwa Zimbabwe wa kuondokana na utawala wa mabavu uliopita.

Kisheria , Zec ina hadi siku tano za kutangaza matokeo rasmi baada ya , lakini katika enzi hii ya mitandao ya kijamii na taarifa gushi wengi wanatarajia Zec itatangaza matokeo yake mapema zaidi.

Lakini atakayeshindwa atakubali? hili litakuwa ni mtihani kwa demokrasia mya ya Zimbabwe kwani miaka ya nyuma vipindi vya baada ya uchaguzi vimekuwa vikitawaliwa na vurugu na ghasia.

Uchaguzi wa marudio utafanyika tarehe 8 Septemba ikiwa hakuna mgombea kati ya wagombea 23 atakaepata ushindi wa zaidiya 50% ya kura.

Tunayo yafahamu kwa sasa kuhusu uchaguzi mkuu wa Zimabwe kwa sasa:

  • Matokeo ya awali yameanza kutolewa.
  • Hakuna aliyetangazwa wazi kuwa mshindi licha ya kwamba vyombo vya habari vya ndani ya nchi vinatuma matokeo kutoka vituo mbali mbali vya uchaguzi kwenye kurasa zao za mitandao. ya kijamii.
  • Rais Emmerson Mnangagwa pamoja na Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe , Nelson Chamisa kwa pamoja wametangaza kuwa watashinda uchaguzi huo kupitia kurasa za Twitter.
  • Hali ya maisha imerejea kuwa ya kawaida huku wafanyabiashara wa mitaani na wenye maduka wakirejea kazini.
  • Uchaguzi wa marudio utafanyika tarehe 8 Septemba ikiwa hakuna mgombea kati ya wagombea 23 atakaepata ushindi wa zaidiya 50% ya kura kulingana na sheria za uchaguzi.
  • Asilimia 75% ya wapigakura walijitokeza ushiriki uchaguzi huo mkuu wa kwanza kufanyika tangu kung'olewa madarakani kwa Robert Mugabe.