Shambulio la Chui India: Mtoto mchanga amejeruhiwa baada ya kunyakuliwa na chui mjini Gujarat

Chanzo cha picha, Bhargav Parikh
Mtoto mchanga wa miezi minne anatibiwa kwa majeraha katika jimbo la magharibi mwa India la Gujarat baada ya chui kumnyakuakutoka mikoni mwa mama yake.
Mama huyo alikuwa amembeba mtoto wake huku akiwa ameketi nyuma ya mumewe ndani ya gari wakati waliposhambuliwa na chui huyo.
Kilio cha baba yake cha kuomba msaada kilisikika kwa wanakijiji kilichopo jirani ambao walikimbia na kumuondoa mnyama huyo.
"Walianza kupiga kelele ambazo zilimtisha chui na akaamua kumdondosha mtoto huyo ," Afisa wa msitu aliieleza idhaa ya BBC Gujarati.
Shabulio hilo lilitokea katika eneo lenye misitu mikubwa ambalo huwa kwa kawaida linalindwa na walinzi.
" Tulikimbia haraka mara baada ya kubaini kisa hicho na tukaita gari la wagonjwa ," Afisa wa misitu, ambaye alikuwa zamu wakati huo alisema.
Mama mtoto pia alijeruhiwa na yuko hospitali na mwanae, aliongeza afisa huyo.

Chanzo cha picha, Bhargav Parikh
Dkt Rajeev Deveshwar amesema mtoto na mama yake wako "thabiti na wanaendelea vizuri".
Mahesh Pandya, mwanamazingira katika eneo hilo ameiambia BBC Gujarati kwamba matukio kama hili hutokea kwasababu binadamu huingia katika "maeneo yanayokaliwa na wanyama kwa miaka mingi".
Visa vya mizozo baina ya binadamu na wanyama vimekuwa vikiongezeka nchini India, ambako kupungua kwa makao ya wanyama mara kwa mara huwafanya tembo, chui na duma kuvamia maeneo ya makazi ya watu.
Inakadiriwa kuwa Kuna chui kati ya 12,000 hadi 14,000 nchini India na kwa wastani chui mmoja huuawa kila siku.
Mwaka jana iliwachukua maafisa wa wanyamapori nchini India karibu saa 36 kumkamata chui ambae alionekana ndani ya kiwanda cha magari
Wafanyakazi wa kiwanda hicho walikuwa wameondoshwa na kiwanda kikafungwa kwa muda wakati waokoaji walipokuwa wakijaribu kumkamata mnyama huyo baada ya msako mkubwa.
Mnamo mwaka 2016, chui mmoja aliingia katika shule kwenye mji wa India wa Bangalore na kuwajeruhi watu sita waliokuwa wakijaribu kumkamata.
Ilichukua saa 10 kumkamata na kumtuliza mnyama huyo.













