Ugiriki yasema moto uliozuka na kuleta maafa makubwa ulisababishwa kwa maksudi

Mji wa Mati ndio ulioathirika zaidi
Maelezo ya picha, Mji wa Mati ndio ulioathirika zaidi

Serikali ya Ugiriki imesema kwamba inaamini moto mkubwa ulizuka na kuleta maafa makubwa umesababishwa kwa makusudi.

Naibu waziri wa ulinzi wa wananchi Nikos Toskas amesema kuna ushahidi mkubwa unaoonyesha uwezekano wa kosa hilo la jinai na kwamba uchunguzi unatakiwa kuanza mara moja.

Hapo awali waziri huyu wa ulinzi alieleza kuwa majengo yaliyokuwa yamejengwa pasipo kuzingatia utaratibu yalikuwa yamezuia njia za dharura za kutokea.

Brian O'Callaghan na mkewe Zoe Holohan walikufa katika moto huo wakisheherekea ndoa yao
Maelezo ya picha, Brian O'Callaghan na mkewe Zoe Holohan walikufa katika moto huo wakisheherekea ndoa yao

Wakati huo huo baadhi ya watu walioponea kuungua katika kisa hicho wamewatupia lawama maafisa wa uokoaji na kusema kwamba shughuli za uokoaji zilikuwa zikifanywa Taratibu.

Miongoni mwa watu ambao mpaka sasa hawajulikani walipo mara baada ya kutokea kwa kisa hicho cha moto ni mapacha wa kike wenye miaka tisa Vassiliki na Sofia Filippopoulou, ambao kwa mara ya mwisho walikua na babu yao katika eneo la Mati wakati moto huo unatokea.

Satelite ya umoja wa ulaya ikionyesha namna makazi ya watu yalivyoharibiwa
Maelezo ya picha, Satelite ya umoja wa ulaya ikionyesha namna makazi ya watu yalivyoharibiwa

Mpaka kufikia sasa watu takribani 83 wamefariki huku makumi ya watu wakiwa hawajulikani walipo na majeruhi 11 kati ya 60 waliojeruhiwa wanapatiwa matibabu ya karibu kutokana na hali yao kuwa mbaya zaidi.