Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Shule ya Moi Girls yafungwa Kenya baada ya tuhuma za kubakwa wasichana shuleni
Je watoto katika shule za Mabweni wako salama kiasi gani? Hilo ndilo suali kubwa wanaouliza Wakenya baada ya kuibuka tuhuma za kubakwa kwa wasichana katika shule moja mjini Nairobi.
Shutuma kali zimeibuka nchini Kenya katika mitandao ya kijamii huku masuali mengi yakiulizwa kuhusu usalama wa watoto wanaosoma katika shule za mabweni baada ya tuhuma kwamba wasichana kadhaa katika shule moja ya upili Nairobi Kenya walibakwa na mtu asiyejulikana ndani ya shule hiyo Jumamosi usiku.
Makundi ya kutetea haki za wanawake yanaandamana nje ya Shule Moi Girls Nairobi kuitaka serikali ichukuwe hatua za kisheria dhidi ya mwalimu mkuu wa shule hiyo.
Wazazi waliokuwa na ghadhabu waliwasili katika shule ya upili ya Moi mjini Nairobi Jumapili asubuhi kuwachukua watoto wao kufuatia agizo la wizara ya elimu nchini.
Akizungumza na waandishi habari alipoizuru shule hiyo, waziri wa elimu nchini Amina Mohammed amesema uchunguzi utaendelea, na kwamba watachunguza mapengo yoyote yaliopo na wayashughulikie.
'Nataka niwahakikishie kwamba tutaimarisha usalama shuleni, na tutahakikisha kwamba watoto wetu wanapokuja hapa, watasoma kama walivyokuja kusoma', amesema Waziri Amina.
Kuna mzozo kuhusu idadi kamili ya wasichana wanaotuhumiwa kubakwa, huku ripoti za kukinzana zikitaja mischana mmoja nyingine zikitaja wasichana watatu ndio waliobakwa katika mkasa huo.
Gazeti moja nchini linasema msichana mmoja aliyeathiriwa amemtaja mwanamume - aliyemueleza kwa rangi ya ngozi mwilini kuwa ni wa kahawia - aliwashambulia usiku.
Afisa mkuu wa polisi anayelisimamia eneo ambako shule hiyo iko, amethibitisha kuwa msichana wa kidato cha pili alibakwa katika choo kilichoko nje ya bweni, lakini hakuweza kuthibitisha tuhuma kuhusu waathiriwa wengine wawili.
Hii sio mara ya kwanza kwa shule hiyo ya Moi Girls kujipata matatani.
Idara ya upelelezi nchini sasa inchunguza tuhuma hizo na kwamba maafisa wa shule hiyo waliwataka wanafunzi wanyamaze wasiripoti kisa hicho cha ubakaji.
Kuna tuhuma pia kwamba mwanafunzi huyo wa kidato chapili aliambiwa ajioshe baada ya mkasa huo , na kwamba aliahidiwa kupewa ufadhili wa karo ya shule.
Kwa sasa shule hiyo ya Moi Girls imefungwa kwa angalau wiki moja kuruhusu uchunguzi ufanyike.