Serikali ya Nigeria imepiga marufuku utengenezaji na uingizaji wa dawa ya codeine

Serikali ya Nigeria imepiga marufuku mara moja utengenezaji na uingizaji wa dawa ya codeine inayotumika kutengeneza dawa za kukohoa.

Wizara ya afya Nigeria imechukua hatua hiyo baada ya uchunguzi wa kitengo kipya cha uchunguzi cha BBC, Africa Eye kubaini kuwa maafisa katika kampuni kubwa za dawa nchini wanahusika katika soko haramu la uuzaji wa dawa hiyo ya Codeine.

Waziri wa afya nchini ametaka dawa hiyo iondolewe katika soko nchini.

Rais wa bunge la Seneti na mkewe rais wa Nigeria, Aisha Buhari, wameelezea wasiwasi kuhusu ongezeko la matumizi ya dawa ya Codeine nchini.

Siku ya Jumatatu Kampuni ya Nigeria inasema imesitisha usambazaji wa dawa ya kukohoa baada ya uchunguzi wa BBC kuhusu kuhusika kwakwe katika uraibu mkubwa wa dawa hiyo nchini.

Emzor Pharmaceuticals imemtimua mkurugenzi wa kampuni hiyo aliyenaswa na mwandishi habari katika kamera ya siri akiuza chupa 60 za dawa hiyo.

Dawa ya kifua ya codeine inasababisha kiwango kikubwa cha uraibu miongoni mamilioni ya vijana nchini Nigeria.

Kampuni hiyo imeahidi uchunguzi 'kamili na wa kina' wa ndani.

Mkurugenzi huyo wa kampuni ya Emzor alinaswa katika kanda ya video kwa siti akijigamba kwamba anaweza kuuza maboxi milioni moja kwa wiki moja katika soko haramu.

Bunge la Seneti Nigeria linakadiria kuwa watu hunywa takriban chupa milioni 3 za dawa hiyo ya Codeine kwa siku moja katika majimbo mawili pekee nchini Kano na Jigawa.

Katika ripoti maalum ya uchunguzi iliyofanywa na BBC Africa, imegundua kuwa baadhi ya wauzaji wa dawa za binadamu huhusika katika biashara hii.

Katika mitaa ya ndani ya Kano kaskazini mwa Nigeria - makundi ya vijana wanashikilia chupa zenye dawa nzito ya maji yenye sukari - ni dawa ya kukohoa codeine.

Dawa hiyo nzito ya maji yenye ladha ya tamu inalewesha na kukupa uraibu.

Hii ni taswira iliyo ya kawaida kote nchini. Uraibu wa dawa hii yenye nguvu umefikia viwango ambavyo havikutarajiwa.

Madhara ya Codeine ki Afya

  • Ni rahisi mtu kuwa mraibu.
  • Inalewesha na mtu huhisi roho kwenda mbio.
  • Mtu hujihisi kisunzi au kizungu zungu.
  • Kuchanganyikiwa akili.
  • Kupungika na pumzi/hewa ya kupumua.

Kenya yapiga marufuku uuzaji holela wa Codeine:

Nchini Kenya hususan katika eneo la kaskazini mashariki Serikali tayari imetoa onyo kuhusu matumizi mabaya ya dawa ya Codeini.

Matumizi ya kupindukia ya dawa hiyo yana madhara mabaya kwa ubongo na huenda ikasababisha mtu kurukwana akili au kuugua matatizo ya akili.

Kwa sasa Kenya imepiga marufuku uuzaji wa dawa hiyo baada ya utafiti uliyofanywa na bodi ya kudhibiti uzajiwa wa madawa nchini Kenya kubaini dawa hiyo inatumiwa vibaya.

Dkt Anthony Martin Kiprotich ni afisa mkuu wa kitengo cha biashara ya kimataifa katika bodi hiyo.

'Matumizi ya dawa hiyo yaliongezeka sana mwaka jana kwa zaidi ya 100%, na kutokana na ripoti ya utafiti tumesitisha matumizi yake kwasababu dawa hiyo ilikuwa inauzwa kwa urahisi madukani bila ya maagizo ya daktari,' amesema Dkt Kiprotich.

Uchunguzi wa bodi hiyo ya uuzaji dawa nchini Kenya (PPB) umebaini ongezeko kubwa la dawa hiyo ya Codeine, na nyingine kadhaa za kupunguza kikohozi zilizo na Codeine.

Na katika baadhi ya visa imegunduliwa kwamba raia huzitumia dawa hizo wakati wa kutafuna majani ya miraa, kama kiburudisho au kileo.

Dkt Anthony Toroitich, anaeleza kwamba kiwango cha mililita 171 000 za dawa zilizo na Codeini ziliuzwa nchini katika muda wa miezi 11.