Tanzania na Burundi miongoni mwa nchi ambazo raia hawana furaha duniani kwa mujibu wa UN 2018

Mwanamke mwenye huzuni

Chanzo cha picha, AFP

Tanzania, Burundi na Rwanda zimeorodheshwa kuwa kati ya nchi zenye watu wasio na furaha duniani katika orodha ya kila mwaka ya Umoja wa Mataifa kuhusu viwango vya furaha duniani.

Burundi ndilo taifa ambalo wakazi wake hawana furaha zaidi duniani katika nafasi ya 156 ambapo imechukua nafasi hiyo kutoka kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) iliyokuwa inashikilia nafasi hiyo mwaka jana.

CAR ndiyo inayoifuata Burundi katika orodha ya mwaka huu.

Tanzania imeshika nafasi ya 153 sawa na mwaka jana huku Rwanda pia ikishikilia nafasi ya 151 sawa na mwaka jana kati ya mataifa 156.

Orodha ya mwaka jana hata hivyo ilishirikisha mataifa 155.

Taifa linaloongoza kwa furaha duniani mwaka huu ni Finland, kwa mujibu wa ripoti hiyo ya UN ambapo nchi hiyo imechukua nafasi hiyo kutoka kwa Norway.

Ripoti hiyo huangazia furaha waliyo nayo watu wa taifa furahi na chanzo cha furaha hiyo.

People enjoy a sunny day on the Esplanade in Helsinki, Finland, in May 2017

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mataifa ya Ulaya Kaskazini yanashikilia nafasi tano za juu katika orodha hiyo, Finland wakiongoza

Mataifa ya Ulaya Kaskazini yanashikilia nafasi tano za juu kwa kuwa na viwango vya juu vya raia walioridhika, huku nchi zilizoathiriwa na vita vya muda mrefu pamoja na nchi kadha za Afrika Kusini mwa Sahara zikiendelea kwa mara nyingine kushikilia nafasi tano za chini.

Burundi, taifa ambalo raia hawana furaha zaidi, lilitumbukia kwenye mzozo wa kisiasa baada ya Rais Pierre Nkurunziza kuamua kuwania tena urais kwa muhula wa tatu mwaka 2015. Mwaka huo kulitokea pia jaribio la mapinduzi ya serikali.

Orodha hiyo huaandaliwa kwa kuangazia pato la mtu kwa kila mwaka, miaka ambayo mtu anatarajiwa kuishi, kuwa na mtu wa kutegemea kwa usaidizi, dhana ya kuwepo uhuru wa kufanya maamuzi maishani, uhuru kutoka kwa ufisadi, na ukarimu miongoni mwa mengine.

Imetayarishwa na shirika la maendeleo endelevu, Sustainable Development Solutions Network (SDSN), ambalo lilianzishwa na Umoja wa Mataifa.

Mwaka 2017, hali ilikuwa hivi:

Maoni ya Watanzania kuhusu ripoti hii

tanzania
Maelezo ya picha, Wageni waliokuja kutembea Tanzania hawawezi kujua maisha yetu
tz
Maelezo ya picha, Tanzania imekuwa na amani miaka yote
tanzania
Maelezo ya picha, Musa anatamani kupata ufafanuzi zaidi maana alijiuliza sana

Mwaka huu, ripoti hiyo iliangazia pia takwimu kuhusu furaha ya wahamiaji katika mataifa wanamoishi ambapo Finland iliibuka kuwa nchi bora zaidi kwa wahamiaji kuishi.

line

Finland hufahamika sana kutokana na nini?

  • Raia wa Finland hupenda sana bafu ya mvuke, pengine kutokana na baridi kali nchini mwao. Taifa hilo bafu za mvuke 3.3 milioni za kutumiwa na raia 5.5 milioni.
  • Ndiyo nchi iliyo na bendi nyingi zaidi za muziki aina ya 'metal'. Bendi zao maarufu ni kama vile HIM, Nightwish na Children of Bodom
  • Kutoka Lapland, unaweza kuwaona kulungu wa nchi za baridi, Mwanga wa Kaskazin na iwapo una bahati utamuona Santa Claus
  • Taifa hilo ni maarufu duniani kwa vibonzo kama vile Moomins na app ya kuchezwa kwenye simu ya Angry Birds

"Nafikiri kila kitu hapa kimepangwa kuwawezesha watu wanafanikiwa, kuanzia kwa vyuo vikuu na mifumo ya uchukuzi ambayo hufanya kazi vyema sana," mwalimu Mmarekani Brianna Owens, anayeishi jiji la pili kwa ukubwa Finland, Espoo, aliambia Reuters.

line

Shirika hilo la UN liliorodheshwa nchi 156 kwa viwango vya furaha na 117 kwa furaha ya wahamiaji.

Norway, Denmark, Iceland na Uswizi ndizo nchi hizo nyingine zinazoshikilia nafasi tano za kwanza kwa furaha.

Uingereza na Marekani zinashikilia nafasi za 19 na 18 mtawalia.

Togo imeimarika zaidi mwaka huu kwa kupanda nafasi 17, nayo Venezuela ikashika zaidi - nafasi 20 - hadi 102.

'Wahamiaji wenye furaha'

Utafiti huo ulibaini kuwa mataifa 10 yenye furaha zaidi pia yanaongoza kwa wahamiaji wao kuridhika.

Finland, taifa la watu 5.5 milioni, lilikuwa na wahamiaji 300,000 mwaka 2016.

Ripoti hiyo ya UN huandaliwa pia kwa kuwahoji watu zaidi ya 1,000 katika zaidi ya nchi 150.

Ripoti hiyo hata hivyo huwa haielezi ni kwa nini nchi moja ina furaha zaidi kushinda nyingine.