Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo Zimbabwe: China yasema haikuingilia kati kumuondoa Mugabe
Serikali ya China imepuuzilia mbali madai kwamba huenda ilihusika katika kumuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu wa Zimbabwe Robert Mugabe.
Maswali yameibuka kwamba huenda mshirika huyo wa muda mrefu wa Zimbabwe kibiashara alihusika baada ya kubainika kwamba Jenerali Constantino Chiwenga alizuru Beijing wiki iliyotangulia hatua ya jeshi la nchi hiyo kuingilia kati na kuchukua udhibiti wa serikali.
China ilikuwa tayari imesisitiza kwamba ziara ya Jen Chiwenga ilikuwa ya kawaida na haikuwa na uhusiano wowote na uamuzi aliouchukua siku chache baadaye.
Leo, wizara ya mambo ya nje ya China kupitia msemaji wake Geng Shuang imekariri kwmaba hakukuwa na jambo ambalo si la kawaida kuhusu ziara hiyo.
Amesema hayo alipokuwa anampongeza rais mpya wan chi hiyo Emmerson Mnangagwa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, ameambia kikao cha wanahabari:
"Ni ziara iliyopangwa muda mrefu na iliidhinishwa na aliyekuwa rais Mugabe. China imekuwa ikidumisha sera ya kutoingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine na hili halijabadilika."
Ameongeza:
"Tunaiunga mkono kwa dhati Zimbabwe ikifuata njia ambayo inaendana na hali ya kisiasa nchini humo na tunaamini kwamba chini ya uongozi wa Bw Mnangagwa, maendeleo ya taifa ya Zimbabwe yatapiga hatua zaidi."