Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tanzania: Uchunguzi kuhusu kuvamiwa kwa Clouds Media kuanzishwa
Waziri wa habari nchini Tanzania Nape Nnauye, ameanzisha uchunguzi kuhusu kisa ambapo kituo kimoja cha runinga kilivamiwa na afisa wa serikali.
Waziri huyo wa habari amechukua hatua hiyo mara baada ya mkurugenzi wa kituo hicho cha habari, Clouds Media Groups, Ruge Mutahaba kuambia wanahabari Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alivamia kituo hicho, akiwa na polisi wenye silaha.
Bw Nnauye ameunda kamati maalum ya kuchunguza kuhusu tukio hilo na akataka apewe matokeo ndani ya saa 24.
Kamera za CCTV katika kituo hicho zinamuonesha mtu anayedaiwa kuwa kamishna wa jiji la Dar es Salaam Paul Makonda, akiwa anasindikizwa na polisi waliojihami, akiingia studio za Clouds Media Group.
Rais John Magufuli amesema katika hotuba yake ya leo alipokuwa akizindua ujenzi wa barabara ya juu eneo la Ubungo, jijini Dar es Salaam kuwa Bw Makonda aendelea kuchapa kazi na kwamba yeye hafanyii kazi maneno ya kwenye mitandao kwa sababu yeye ndiye Rais wa nchi.
Dkt Magufuli amesema kuwa kuna baadhi ya watu wanaingilia majukumu yake wakati yeye ndiye mwenye uamuzi na kwamba hapangiwi kazi ya kufanya kwa sababu anajiamini.