Maprofesa waliotekwa na Taliban waoneshwa kwenye video

Timothy Weekes

Chanzo cha picha, Via AP

Maelezo ya picha, Timothy Weekes alitoa wito kwa Bw Trump kumsaidia

Wapiganaji wa Taliban wametoa kanda ya video inayowaonesha mateka wawili - Mmarekani na raia wa Australia - ambao walitekwa na wanamgambo hao nchini Afghanistan mwaka jana.

Mmarekani Kevin King na raia wa Australia Timothy Weekes walikuwa maprofesa katika chuo kikuu cha Wamarekani cha Afghanistan mjini Kabul.

Walitekwa mwezi Agosti wakiwa kwenye magari yao nje ya chuo hicho na wapiganaji waliokuwa wamevalia sare za wanajeshi wa serikali.

Baadaye mwezi huo, wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan walijaribu kuwakomboa lakini wakashindwa, Pentagon ilisema.

Kwenye video hiyo ambayo inadaiwa kupigwa mnamo 1 Januari na kupakiwa mtandaoni, wanaume hao wanasema wamo buheri wa afya.

Lakini wanamuomba Rais mteule wa Marekani Donald Trump kujitolea kuwabadilisha na wafungwa wa Taliban ndipo waachiliwe huru.

Wanasema watauawa iwapo Marekani haitashiriki kwenye mazungumzo ya kuwaachilia huru.

Kevin King

Chanzo cha picha, Via AP

Maelezo ya picha, Kevin King pia alioneshwa
Afghanistan

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Marekani walijaribu kuwaokoa Septemba mwaka jana lakini wakafeli