Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Madaktari Kenya wakataa nyongeza ya mishahara ya serikali
Madaktari nchini Kenya wamekataa nyongeza ya karibuni zaidi iliyopendekezwa na serikali katika juhudi za kujaribu kumaliza mgomo wa madaktari na wahudumu wa afya ambao umedumu kwa mwezi mmoja sasa.
Mgomo huo umelemaza huduma katika hospitali na zahanati za umma.
Rais Uhuru Kenyatta alikutana na wawakilishi wa chama cha taifa cha madaktari hao Jumanne na kupendekeza nyongeza ya mshahara na marupurupu ya madaktarii kwa angalau $560 (£450).
Hilo lingesababisha madaktari wanaoanza kazi kulipwa takriban $2,000 kila mwezi.
Viongozi wa chama hicho, ambao walikuwa wameahidi kutangaza msimamo leo, walisema pendekezo la serikali linawafaa madaktari lakini kuna baadhi ya mambo ya kuwafaa wananchi ambayo yameachwa nje.
Madaktari wanaitaka serikali kutekeleza makubaliano ya mishahara na marupurupu yaliyotiwa saini mwaka 2013.
Kwenye makubaliano hayo, serikali iliahidi kuongeza idadi ya madaktari, kuongeza pesa za utafiti wa kimatibabu, dawa na vifaa na mitambo katika hospitali za umma.