Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Daraja refu zaidi la kioo limefunguliwa China
Daraja refu zaidi duniani ambalo sakafu yake ni kioo limefunguliwa katika mji wa Zhangjiajie katika mkoa wa Hunan nchini China.
Daraja hilo ndilo la juu zaidi lenye sakafu ya kioo duniani na linaunganisha milima miwili ambayo hufahamika kama Milima ya Avatar. Filamu ya Avatar iliandaliwa katika milima hiyo.
Daraja kwa tarakimu
Ujenzi ulikamilika Desemba mwaka jana. Urefu wa daraja hilo ni 430m na liligharimu $3.4m (£2.6m).
Daraja hilo limewekwa 300m juu ya ardhi, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la Xinhua.
Sakafu yake imeundwa kwa vipande 90 vya vioo ambavyo vina tabaka tatu.
Kwa mujibu wa maafisa wa serikali, daraja hilo lenye upana wa mita 6, ambalo mchoro wake uliandaliwa na msanifu mijengo kutoka Israel Haim Dotan, tayari limeweka rekodi kadha za dunia katika usanifu mijengo na ujenzi.
Je, na usalama wake?
Hili ni suala kuu. Lakini maafisa wameandaa hafla za kudhihirisha uthabiti wake. Maafisa walituma watu wenye nyundo kujaribu kuvunja vioo. Pia magari yaliyojaa abiria yalipita juu yake mapema mwezi huu.
Mwandishi wa BBC Dan Simmons ni mmoja wa walioalikwa kujaribu kubaini iwapo vioo vya daraja hilo vinaweza kuvunjika.
Maafisa wanasema watu 8,000 wataruhusiwa kutumia daraja hilo kila siku.