Daraja refu zaidi la kioo limefunguliwa China

Daraja la Zhangjiajie, China

Chanzo cha picha, AP

Maelezo ya picha, Daraja hilo la kioo linapatikana katika mkoa wa Hunan

Daraja refu zaidi duniani ambalo sakafu yake ni kioo limefunguliwa katika mji wa Zhangjiajie katika mkoa wa Hunan nchini China.

Daraja hilo ndilo la juu zaidi lenye sakafu ya kioo duniani na linaunganisha milima miwili ambayo hufahamika kama Milima ya Avatar. Filamu ya Avatar iliandaliwa katika milima hiyo.

Wale wenye ujasiri wataweza kutazama mandhari ya kuvutia

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wale wenye ujasiri wataweza kutazama mandhari ya kuvutia

Daraja kwa tarakimu

Ujenzi ulikamilika Desemba mwaka jana. Urefu wa daraja hilo ni 430m na liligharimu $3.4m (£2.6m).

Daraja hilo limewekwa 300m juu ya ardhi, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la Xinhua.

Sakafu yake imeundwa kwa vipande 90 vya vioo ambavyo vina tabaka tatu.

Kwa mujibu wa maafisa wa serikali, daraja hilo lenye upana wa mita 6, ambalo mchoro wake uliandaliwa na msanifu mijengo kutoka Israel Haim Dotan, tayari limeweka rekodi kadha za dunia katika usanifu mijengo na ujenzi.

Muonekano wa daraja hilo

Chanzo cha picha, Reuters

Je, na usalama wake?

Hili ni suala kuu. Lakini maafisa wameandaa hafla za kudhihirisha uthabiti wake. Maafisa walituma watu wenye nyundo kujaribu kuvunja vioo. Pia magari yaliyojaa abiria yalipita juu yake mapema mwezi huu.

Mwandishi wa BBC Dan Simmons ni mmoja wa walioalikwa kujaribu kubaini iwapo vioo vya daraja hilo vinaweza kuvunjika.

Maelezo ya video, Dan Simmons tests the world's longest glass-bottomed bridge
Maafisa walituma watu na nyundo makusudi

Chanzo cha picha, AP

Maelezo ya picha, Maafisa walituma watu na nyundo makusudi
Magari yaliyojaa watu pia yalipita juu

Chanzo cha picha, AP

Maelezo ya picha, Magari yaliyojaa watu pia yalipita juu

Maafisa wanasema watu 8,000 wataruhusiwa kutumia daraja hilo kila siku.