Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mahamoud Ali Youssouf: Kutoka diplomasia ya Djibouti hadi uongozi wa AUC
Na Yusuph Mazimu
Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, ambao umekuwa ukifuatiliwa kwa karibu siku za hivi karibuni, umefanyika Ijuma hii na Mahamoud Ali Youssouf Ali Youssouf, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Djibouti kushinda.
Ulikuwa uchaguzi wenye ushindani, ambapo Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Djibouti Mohammed Ali Youssouf ameibuka mshindi dhidi ya Raila Odinga, waziri mkuu wa zamani wa Kenya na Richard Randriamandrato, waziri wa mambo ya nje wa zamani wa Madagascar.
Youssouf alishinda kwa kupata kura 33 katika raundi ya 7, ambayo alisalia kama mgombea pekee baada ya Raila kujiondoa katika raundi ya sita kufuatia kupitwa kura na Youssof katika raundi ya tatu, nne, tano na raundi hiyo ya sita.
Randriamandrato kutoka Madagascar, waziri mambo ya nje wa zamani alijiondoa katika raundi ya tatu.
Youssof sasa anakwenda kumrithi Moussa Faki Mahamat, kama mwenyekiti mpya wa Tume hiyo ya Umoja wa Mataifa kutoka Chad, mwanadiplomasia aliyechaguliwa kushika wadhifa huo tangu Machi 14, 2017.
Mahamoud Ali Youssouf ni nani?
Mahamoud Ali Youssouf, 58, ni waziri wa mambo ya nje wa nchi ndogo ya Djibouti, yenye umuhimu wake kimkakati katika Pembe ya Afrika.
Ni mwanadiplomasia na msomi mwenye taaluma ya uongozi wa biashara akisomea chuo kikuu cha Liverpool nchini Uingereza.
Kimataifa, Youssouf amekuwa akiongoza kama Mwenyekiti wa Kikao cha Kawaida cha 129 cha Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya nchi za kiarabu mnamo 2008.
Mbali na kushika ubalozi wa Djibouti nchini Misri kati ya mwaka 1997 na 2001, amekuwa waziri wa mambo ya nje wa Djibouti tangu 2005, akihudumu chini ya marais watatu.
Ndiye Waziri anayetajwa kushika wadhifa wa mambo ya nje kwa muda mrefu zaidi barani Afrika.
Kushika kwake wadhifa huo muhimu katika siasa kwa miongo miwili inakuonyesha ni mtu wa aina gani.
Ni mtu mwenye kuungwa mkono anayeonyesha dhamira ya kufanya kitu kwa taifa lake na bara la Afrika.
"Lengo langu kuu nikichaguliwa ni kukomesha kuenea" kwa virusi katika bara hilo, aliiambia AFP katika mahojiano mwezi uliopita.
Alisema kuwa kamati hiyo inahitaji marekebisho, na kuongeza kuwa mageuzi haya yaanze kwa uongozi na viongozi wakuu.
Mbali na kudumisha amani na usalama barani humo, alisema matarajio yake ni kukuza maendeleo ya kiuchumi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Anajivunia kuwa na uwezo wa kuzungumza lugha mbalimbali, na anaamini kwamba uwezo huu wa kuwasiliana unamwezesha kuwa daraja linalounganisha kaskazini na kusini, mashariki na magharibi.
Imehaririwa na Asha Juma