Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Ukraine haitahudhuria mazungumzo ya Marekani na Urusi nchini Saudi Arabia, chanzo cha serikali kimeiambia BBC

Wakati huo huo, viongozi wa Ulaya wanajiandaa kwa mkutano wa dharura nchini Ufaransa huku bara hilo likijibu hatua za Marekani juu ya Ukraine.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa leo. Kwaheri

  2. Zelensky asisitiza kuwa "hatakubali" makubaliano yaliyofikiwa bila Ukraine

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesisitiza msimamo wake kwamba Ukraine haitakubali kamwe makubaliano ya amani yaliyojadiliwa kati ya Urusi na Marekani pekee, bila Ukraine kuwepo mezani.

    Zelensky alisikika akisema maneno hayo mara kwa mara huko Ulaya wiki hii - lakini sasa, akizungumza na hadhira ya Marekani, anazidi kufikisha ujumbe nyumbani.

    "Sitakubali kamwe maamuzi yoyote kati ya Marekani na Urusi kuhusu Ukraine," anasema.

    "Hivi ni vita nchini Ukraine dhidi yetu, na ni hasara kwetu kibinadamu," anaongeza.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio anatarajiwa kukutana na maafisa wa Urusi nchini Saudi Arabia lakini ujumbe wa Ukraine hautakuwepo.

  3. Zelensky atoa wito kwa jeshi la Ulaya huku kukiwa na hofu juu ya msimamo wa Marekani

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky hapo jana alitoa wito wa kuundwa kwa "jeshi la Ulaya" huku kukiwa na wasiwasi unaoongezeka kwamba huenda Marekani isitoe msaada tena katika bara hilo.

    Akizungumza katika Mkutano wa Usalama wa Munich siku ya Jumamosi, alisema hotuba ya Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance katika hafla hiyo ilionyesha wazi kwamba uhusiano wa zamani kati ya Ulaya na Marekani "unamalizika" na bara hilo "linahitaji kuzoea hali hiyo".

    Hata hivyo, Zelensky pia alisema Ukraine "haitakubali kamwe mikataba iliyofanywa nyuma ya migongo yetu bila ushiriki wetu" baada ya Trump na Rais wa Urusi Vladimir Putin kukubali kuanzisha mazungumzo ya amani.

    Viongozi wa Ulaya kutoka katika bara zima wameitetea Ukraine katika siku chache zilizopita, wakisema kwa uthabiti kwamba hakuna mazungumzo ya amani yanayoweza kufanyika bila Ukraine - au bila ushiriki wa Ulaya.

    Mapema wiki hii Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kuwa na mazungumzo marefu ya simu na kiongozi huyo wa Urusi na kuongeza kuwa mazungumzo ya kusitisha "vita vya kipuuzi" nchini Ukraine yataanza "mara moja".

    Trump kisha "alimjulisha" Zelensky juu ya mpango wake.

  4. Takriban 48 wamefariki dunia katika ajali ya mgodi wa Mali

    Takriban wachimbaji 48 wameuawa kufuatia kuanguka kwa mgodi wa dhahabu haramu uliotelekezwa huko Magharibi mwa Mali.

    Polisi wa eneo hilo wamethibitisha ajali hiyo ilisababishwa na maporomoko ya ardhi na waathiriwa wengi ni wanawake vijana akiwemo mmoja aliyebeba mtoto mgongoni.

    Mali ni mmoja wa wazalishaji wanaoongoza wa dhahabu barani Afrika lakini kama nchi nyingi za Afrika Magharibi, viongozi wana wakati mgumu kudhibiti shughuli za wachimbaji haramu.

    Mkuu wa shirika la mazingira la ndani alinukuliwa akisema kwamba 'kuna ugumu mwingi katika utafuta madini kwenye eneo kama hili, ".

    Ajali hiyo ilitokea katika eneo ambalo lilikuwa limetelekezwa, na hapo awali liliendeshwa na kampuni ya Wachina.

    Ajali za mgodi sio kawaida kwa Mali, mwaka mmoja uliopita tukio kama hilo lilitokea katika eneo hilo hilo ambalo lilisababisha vifo vya watu wapatao 70.

    Na mwezi uliopita, watu takriban 10 waliuawa na wengine kujeruhiwa, wengi wao wanawake katika ajali ya mgodi.

  5. Taarifa za Ukraine kutoka kwa timu ya Trump zawaacha washirika na wasiwasi

    Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, amewashangaza washirika wa Marekani kwa hotuba yake iliyoeleza kile ambacho wengi walikiona kama msururu wa makubaliano ambayo Ukraine ingepaswa kutia saini makubaliano yoyote ya amani na Urusi yaliyosimamiwa na Rais Trump.

    Hegseth alisema "haikuwa sawa" kufikiria kwamba Ukraine inaweza kurudisha eneo lake huru linalokaliwa na Urusi, kama ilivyo hitaji lake la kujiunga na uanachama wa Nato, akiongeza kuwa ni juu ya wanajeshi wa Ulaya na sio Marekani kudumisha amani.

    Wakosoaji, ikiwa ni pamoja na baadhi ya Warepublican mjini Washington, walikashifu hotuba hiyo, wakisema iliondoa nguvu zote za Ukraine kabla ya mazungumzo yoyote. Waliongeza kuwa, ilikuwa ni utiifu wa Marekani kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin.

    "Kwa hakika ni mbinu ya mazungumzo ya kufanya makubaliano makubwa sana hata kabla hayajaanza," alisema Waziri Mkuu wa zamani wa Uswidi Carl Bildt, ambaye ni mwenyekiti mwenza wa Baraza la Ulaya la Uhusiano wa Kigeni.

    Siku iliyofuata, Hegseth alirudia baadhi ya yale aliyokuwa amesema. Alifafanua kuwa chaguzi zote kwa kweli bado ziko mezani kwa Trump kutumia kama njia kati ya Putin na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

    "Anachoamua kuruhusu au kutoruhusu ni kwa kiongozi huru wa ulimwengu, Rais Trump," alisema Hegseth.

    Hata hivyo aliongeza kwamba amekuwa "akionyesha tu uhalisia" na kukataa wazo kwamba alikuwa ametoa makubaliano yoyote yasiyofaa kwa Moscow.

    Soma zaidi:

  6. Kumi na wanane wauawa katika kituo treni India

    Takriban watu 18 wamekufa na wengine 10 kujeruhiwa katika ajali iliyotokea kwenye kituo cha reli cha New Delhi.

    Maelfu ya watu waliripotiwa kujaa kwenye kituo cha treni Jumamosi usiku walipokuwa wakijaribu kupanda treni zilizochelewa.

    Wanne kati ya waathiriwa walikuwa watoto, huku 10 wakiwa wanawake, kulingana na orodha iliyotolewa na maafisa.

    Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alisema alikuwa pamoja "na wale wote ambao wamepoteza wapendwa wao" kupitia ujumbe wake wa X.

    Mkanyagano kwenye umati kunaripotiwa kutokea mara kwa mara nchini India ambapo kila wakati kuna msongamano ama kwenye hafla za kidini, sherehe na maeneo ya umma.

    Tukio hilo linatokea wiki kadhaa baada ya watu 30 kuuawa katika mkanyagano uliotokea alfajiri katika tamasha la kidini, Kumbh Mela, kaskazini mwa India, ambapo makumi ya mamilioni ya Wahindu walikuwa wamekusanyika kuoga katika maji matakatifu ya mto katika

    Pia unaweza kusoma:

  7. Viongozi wa Ulaya wako tayari kufanya mkutano wa dharura juu ya Ukraine

    Upande wa Trump ulisema viongozi wa Ulaya watashauriwa lakini hawatashiriki katika mazungumzo yoyote kati ya Marekani na Urusi kuhusu kumaliza vita.

    Viongozi wa Ulaya wanatazamiwa kukutana wiki ijayo kwa mkutano wa dharura kuhusu vita nchini Ukraine, kujibu wasiwasi wa kwamba Marekani inaendelea kuhusisha Urusi pekee katika mazungumzo ya amani hatua ambayo itafungia bara hilo nje.

    Sir Keir Starmer, ambaye anatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wa kilele huko Paris, alisema ni "kipindi nadra sana kwa usalama wetu wa kitaifa" na ni wazi Ulaya lazima ichukue jukumu kubwa katika Nato.

    Haya yanajiri baada ya mjumbe maalum wa Donald Trump nchini Ukraine kusema viongozi wa Ulaya watashauriwa lakini hawatashiriki katika mazungumzo yoyote kati ya Marekani na Urusi kuhusu kumaliza vita.

    Viongozi wakuu wa Ikulu ya White House, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, wanatarajiwa kukutana na wapatanishi wa Urusi nchini Saudi Arabia katika siku zijazo.

    Maafisa wa Marekani walisema kuwa Ukraine pia ilialikwa - ingawa Rais Volodymyr Zelensky anasema nchi yake haijapokea mwaliko kama huo.

    Katika matamshi ambayo huenda yakazua wasiwasi nchini Ukraine na miongoni mwa washirika wa Ulaya, mjumbe maalum Keith Kellogg alisema mazungumzo ya awali yameshindwa kwa sababu pande nyingi zilihusika.

    "Inaweza kuwa kama chaki ubaoni, inaweza kupakwa kidogo, lakini ninasema kitu ambacho ni kweli kabisa," alisema Jumamosi.

    Ulaya inasalia kuandamwa na makubaliano ya Minsk, mapatano yaliyofeli ya kusitisha mapigano kati ya Ukraine na Urusi yaliyofikiwa mwaka 2015.

    Mazungumzo hayo ambayo yalisimamiwa na Ufaransa na Ujerumani yalitaka kukomesha mapigano katika eneo la Donbas mashariki mwa Ukraine.

    Kinachofahamika ni kuwa, Sir Keir ameonekana kuwa na jukumu lake la kuzileta Marekani na Ulaya pamoja ili kuhakikisha kunakuwepo na mwelekeo mmoja wa kuhakikisha upatikanaji wa amani nchini Ukraine.

    Soma zaidi:

  8. Viongozi watoa maoni mseto baada ya Raila Odinga kushindwa UAC

    Viongozi nchini Kenya wamezungumzia uchaguzi wa AUC na kuonyesha hisia mseto huku mgombea wa uenyeketi kutoka nchini humo Raila Odinga akishindwa na mgombea wa Djibouti Mahamoud Ali Youssouf.

    Kiongozi wa taifa nchini Kenya William Ruto, ameandika kwenye mtandao wa X na kuonyesha shukrani zake kwa uongozi wa bara Afrika.

    "Asanteni kwa kusikiliza maono na vipaumbele vya mheshima @RailaOdinga kwa Umoja wa Afrika na kwa kumpa fursa ya kushirikisha ndoto yake ya mabadiliko katika bara hili.

    Kwa waheshimiwa Mahmoud Youssouf na Selma Haddadi, mwenyekiti na naibu mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika, ninawapa pongezi zangu za dhati.

    Bunge la AU limewaamini, na Kenya inaahidi kutoa ushirikiano wake kamili kwenu munapoongoza Tume ya Muungano wa Afrika hadi kiwango kingine.

    Uchaguzi huu haukuhusu watu au mataifa, ulikuwa juu ya mustakabali wa Afrika. Siku za baadaye ni zenye matumaini na umoja, tutaendelea kushirikiana kwa Afrika yenye umoja, mafanikio, na ushawishi mkubwa kimataifa.

    Naibu Rais wa Kenya Kithure Kindiki aliandika kwenye mtandao wa X akisema, Rais Ruto, mgombea wetu Raila Odinga na timu yake ya kampeni walijitahidi kwa kila namna. Kwa bahati mbaya, tumeshindwa. Tunasalia kuwa taifa lenye furaha kwamba tulikaribia sana. Leo haikuwa siku yetu ila iko siku itafika. Asante kwa marafiki wote wa Kenya ambao walisimama na sisi kwa wakati stahiki.

    Pia amesisitiza juu ya haja ya kutathmini upya kilichokoseka ili kisijirudie katika siku za usoni.

    Wakili mwandamizi Ahmednasir Abdullahi amempongeza Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kwa kazi nzuri aliyoipigania hadi mwisho.

    "Mheshimiwa Raila na Kenya wamejitahidi kadiri ya uwezo wao ... lakini Djibouti na mgombea wake walikuwa maarufu zaidi katika bara lote ... pongezi," alisema kwenye mtandao wa X.

    Gavana wa Mombasa Abdulssemad Nassir alisema Raila amekuwa akitafuta kitu kikubwa kuliko yeye mwenyewe - huduma, uadilifu, na utafutaji usio na kikomo wa mustakabali bora wa baadaye wa Kenya na Afrika.

    Alisema wakati matokeo ya uchaguzi ni yale ambayo nchi ilitarajia, naibu huyo wa chama cha ODM alisema haipunguzi thamani ya uongozi wa Raila au heshima aliyonayo katika bara hili.

    "Hii haikuwa tu juu ya nafasi aliogombea; ilikuwa juu ya maono ya umoja wa Afrika, maendeleo, na ustawi. Ustadi alionao Baba unaendelea kuhamasisha, na ushawishi wake unasalia kuwa imara kama zamani," aliandika kwenye mtandao wa X.

    Mshauri mwandamizi wa Baraza la Washauri wa Uchumi katika Ikulu, Moses Kuria, alisema Afrika imepoteza fursa ya kufaidika na uongozi wenye maono wa Raila.

    "Ni Afrika ambayo imepoteza sio Baba. Changamoto zilizo mbele ni kubwa kwa Afrika. Ni Afrika ambayo imekosa uongozi uliokomaa. Kama nchi tutakuwa naye wenyewe Baba yetu na kufaidika na kile Afrika imepoteza," alisema.

    Soma zaidi:

  9. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 16/02/2025