Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, Harry Kane ataisumbua tena Arsenal katika Ligi ya Mabingwa?
Huenda Arsenal walifurahia kutimka Harry Kane alipoondoka Tottenham na kwenda Bayern Munich majira ya joto.
Lakini anarejea Kaskazini mwa London akijaribu kuwaondoa vijana hao wa Mikel Arteta katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
The Gunners wanawakaribisha Bayern katika mechi ya Jumanne ya robo fainali ya kwanza.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 amefunga mabao mengi zaidi katika Ligi ya Uingereza dhidi ya Arsenal kuliko mchezaji mwingine yeyote - amefunga mara 14.
Kane amevunja rekodi nchini Ujerumani kwa kufunga mabao 38 katika mechi 37 za kwanza.
Anakaribia kupata Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya, kama mfungaji bora anavyozawadiwa katika ligi zote za Ulaya na kiatu ambacho hajawahi kukipata hapo awali. Kwa sasa ana mabao 32.
Nahodha huyo wa Uingereza ni mchezaji wa nne kufikisha magoli hayo katika ligi ya Bundesliga, nyuma ya wachezaji magwiji wa Bayern, Gerd Muller na Robert Lewandowski, ambao walifikia magoli hayo mara tatu kila mmoja, na Dieter Muller wa Cologne.
Rekodi ya mabao mengi 41 katika ligi ya Bundesliga iliwekwa na Lewandowski akichezea Bayern mwaka 2020-21, rekodi ambayo Kane atahitaji mabao 10 katika mechi zake sita za mwisho ili kuivunja.
"Atashinda Kiatu cha Dhahabu mwaka huu na hilo litaongeza mtazamo kwamba, ni mshambuliaji mzuri," alisema mwandishi wa habari wa soka barani Ulaya Guillem Balague kwenye BBC Radio 5.
"Amezoea haraka sana na anajaribu kujifunza Kijerumani na anafanya vizuri uwanjani. Huku watoto wake wanne na mke wake wakiwa pamoja nae."
Zaidi ya hayo, hakuna aliyefunga mabao mengi katika Ligi ya Mabingwa msimu huu kuliko mabao sita ya Kane.
Mashindano hayo yanaweza kuwa nafasi nzuri zaidi kwa Kane kushinda taji lake kuu la kwanza la mashindano hayo. Ikumbukwe hakushinda taji lolote katika muongo mmoja akiwa katika kikosi cha kwanza cha Tottenham.
Alihamia Bayarn ambayo ilikuwa imeshinda mfululizo mataji 11 ya Bundesliga lakini sasa wako pointi 16 nyuma ya vinara Bayer Leverkusen, zikiwa zimesalia mechi sita.
Iwapo Leverkusen wataifunga Werder Bremen siku ya Jumapili - itakuwa mara ya kwanza tangu Aprili 2013 kwa Bayern kutokuwa mabingwa wa Ujerumani.
Na ushindi wa Leverkusen utathibitishwa zaidi siku ya Jumamosi ikiwa vijana wa Thomas Tuchel watafungwa na wakiwa nyumbani.
"Kama Kane angekuwa na mataji mengi angeonekana kama mchezaji wa tofauti zaidi kwa kila mtu," anasema Balague.
"Bila shaka sasa, yuko kwenye klabu kubwa, akijaribu kushinda mambo mengi katika klabu hiyo na anafanya vyema."
Mwandishi wa kandanda barani Ulaya Mina Rzouki anasema: "Bayern wamekuwa na wakati mgumu msimu huu lakini amekuja na kuipeleka mbele. Itakuwa ajabu sana ikiwa hatashinda chochote."