Uchaguzi wa Marekani 2024: Ni lini tutajua nani ameshinda uchaguzi?

- Author, Sam Cabral
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Wapiga kura wa Marekani watapiga kura tarehe 5 Novemba kuchagua rais wao ajaye.
Matokeo ya uchaguzi wa Marekani wakati mwingine hutangazwa ndani ya saa chache baada ya vituo kufungwa. Na katika baadhi ya kinyang'anyiro cha urais mshindi alitangazwa usiku wa siku ya uchaguzi, au mapema asubuhi iliyofuata.
Mgombea wa chama cha Democratic, Kamala Harris, Makamu wa Rais wa sasa, na mgombea wa chama cha Republican, Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani, ushindani wao unakaribiana.
Ushindi mwembamba unaweza kupelekea kura kuhesabiwa upya. Katika jimbo la Pennsylvania, kwa mfano, kuhesabiwa upya kwa jimbo zima kutahitajika ikiwa kutakuwa na tofauti ya nusu ya asilimia kati ya kura zilizopigwa kwa mshindi na aliyeshindwa.
Changamoto za kisheria ni jambo jingine linaloweza kuchelewesha matokeo. Zaidi ya kesi 100 za kabla ya uchaguzi tayari zimewasilishwa na wanachama wa Republican, zikiwemo kuhusu ustahiki wa wapiga kura na usimamizi wa daftari la wapiga kura.
Matukio mengine ambayo yanaweza kusababisha ucheleweshaji ni pamoja na matatizo yoyote yanayohusiana na uchaguzi, hasa katika maeneo ya kupigia kura.
Chaguzi zilizopita
Uchaguzi wa 2020 ulifanyika Jumanne Novemba 3. Lakini Televisheni za Marekani hazikumtangaza Joe Biden kuwa mshindi hadi Jumamosi asubuhi ya Novemba 7, baada ya matokeo ya Pennsylvania kuwa wazi zaidi.
Mwaka 2016, Trump aliposhinda urais, alitangazwa mshindi siku moja baada ya uchaguzi.
Mwaka 2012, wakati Barack Obama aliposhinda muhula wa pili, ushindi wake ulionekana kabla ya saa sita usiku siku yenyewe ya kupiga kura.
Uchaguzi wa 2000 kati ya George W Bush na Al Gore ulikuwa tofauti. Kura zilipigwa tarehe 7 Novemba, Lakini kukawa na mchuano mkali huko Florida na kinyang'anyiro hicho hakikuamuliwa hadi Disemba 12.
Mahakama ya Juu ya Marekani ilipiga kura kusitisha mchakato wa kuhesabu kura upya kwa jimbo hilo, na Bush akawa mshindi na kumkabidhi White House.
Majimbo gani muhimu 2024?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kote Marekani, vituo vya kwanza vya kupigia kura vitafungwa saa 23:00 GMT siku ya Jumanne na vituo vya mwisho vitafungwa saa 06:00 GMT, siku ya Jumatano.
Kinyang'anyiro hiki kinatarajiwa kupata matokeo kutoka katika majimbo saba. Majimbo yenyewe ni Arizona, Georgia, Michigan, Nevada, North Carolina, Pennsylvania na Wisconsin.
Saa 00:00 GMT – vituo vitafungwa huko Georgia na majimbo mengine matano, na katika majimbo mengine mawili.
00:30 GMT, vituo vitafungwa katika majimbo matatu, ikijumuisha North Carolina. Matokeo ya mapema yakitoka North Carolina na Georgia, picha inaweza kuanza kuonesha ni mgombea gani anafanya vyema zaidi, lakini bado itakuwa mapema mno kujua mshindi.
01:00 GMT – vituo vitafungwa Pennsylvania, na katika majimbo mengine 15 na Mkoa wa Columbia, na pia Michigan na majimbo mengine manne. Afisa mkuu wa uchaguzi wa Georgia anakadiria kuwa takriban 75% ya kura zitahesabiwa kufikia wakati huo.
02:00 GMT - upigaji kura utaisha huko Arizona, Wisconsin na majimbo mengine 12. Vituo vyote vilivyosalia vitafungwa huko Michigan.
Michigan inaruhusu maafisa kuanza kuhesabu kura wiki moja kabla ya siku ya uchaguzi, lakini hawaruhusiwi kufichua matokeo hadi upigaji kura uishe.
Huko Pennsylvania na Wisconsin majimbo hayo hayaruhusu kuhesabu kura hadi kuanza kwa upigaji kura wa ana kwa ana, na hilo husababisha kuchelewea kwa matokeo kutoka katika majimbo hayo.
03:00 GMT - vituo hufungwa kote Nevada na majimbo mengine mawili. Kura za Nevada zinaweza kuchukua siku kuhesabiwa, kwa sababu jimbo hilo huruhusu kura za barua za posta kuhesabiwa hata kama zimetuma siku ya uchaguzi.
Kura za wasiohudhuria vituoni ambazo hutumwa kwa posta, zikiwemo kura za wanajeshi na Wamarekani wanaoishi ng'ambo, kwa kawaida ni miongoni mwa kura za mwisho kuhesabiwa.
Kura huhesabiwaje?
Kwa kawaida, kura zinazopigwa siku ya uchaguzi huhesabiwa kwanza, zikifuatiwa na kura za mapema na za posta, kisha zile ambazo zimepingwa, na mwisho kura za ng'ambo na za wanajeshi.
Maafisa wa uchaguzi wa eneo - ambao huteuliwa, wakati mwingine huchaguliwa – huthibitisha kura na mchakato wa kuhesabu.
Kuthibitisha kura ni pamoja na kulinganisha idadi ya kura na idadi ya wapiga kura walio hai. Kuchukua, kufunua na kuchunguza kila kura moja kama imechanika, ina doa au imeharibika. Pia kuweka kumbukumbu na kuchunguza ukiukaji wowote.
Kuhesabu kura kunahusisha kuiingiza kila moja kwenye skana za kielektroniki zinazoweka matokeo kwenye jedwali. Katika baadhi ya matukio hesabu za mikono au hesabu za mara mbili huhitajika.
Kila jimbo na eneo lina sheria kali kuhusu ni nani anayeweza kushiriki katika kuhesabu kura, ikijumuisha jinsi waangalizi wa vyama wanavyoweza kufuatilia na kuingilia kati katika kuhesabu kura.
Kura za wajumbe maalumu

Chanzo cha picha, Getty Images
Mara baada ya kila kura halali kujumuishwa katika matokeo ya mwisho, mfumo wa kura za wawakilishi maalumu wanaomchagua Rais huanza kutumika.
Katika kila jimbo kuna idadi tofauti za kura za wawakilishi hao. Kwa ujumla, wawakilishi maalumu hupiga kura zao zote kwa yeyote atakayeshinda kura nyingi.
Bunge jipya la Marekani litakutana tarehe 6 Januari kuhesabu kura za wawakilishi maalumu na kuthibitisha rais mpya.
Baada ya uchaguzi wa 2020, Trump alikataa kukubali kushindwa na kuwahimiza wafuasi kuandamana hadi Ikulu ya Marekani wakati Bunge likikutana ili kudhibitisha ushindi wa Biden.
Alimsihi makamu wake wa rais, Mike Pence, kukataa matokeo - lakini Pence hakukubaliana naye.
Hata baada ya ghasia kuvunjwa na wajumbe wa Congress kujipanga upya, Warepublican 147 walipiga kura bila kufaulu kutengua kupoteza kwa Trump.
Mageuzi ya uchaguzi tangu wakati huo yamefanya kuwa vigumu kwa wabunge kupinga matokeo yaliyoidhinishwa - yanayotumwa kwao kutoka katika majimbo. Pia mageuzi hayo yanasema makamu wa rais hana uwezo wa kukataa kura za uchaguzi.
Trump, mgombea wake mwenza JD Vance na viongozi wakuu wa chama cha Republican mjini Capitol Hill wamekataa mara kadhaa kusema watakubali matokeo iwapo atashindwa.
Rais mteule ataanza muhula wake wa uongozi baada ya kuapishwa Jumatatu, 20 Januari 2025, katika uwanja wa majengo ya Capitol ya Marekani.
Itakuwa ni mara ya 60 kuapishwa kwa rais katika historia ya Marekani.
Hafla hiyo itamshuhudia rais mpya akiapishwa kwa ahadi ya kuilinda Katiba na kisha kutoa hotuba yake ya kuapishwa.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












