Wauaji wa mwanariadha wa Uganda wahukumiwa kifungo cha miaka 35

Chanzo cha picha, Reuters
Kenya imewahukumu wanaume wawili kifungo cha miaka 35 kila mmoja kwa mauaji ya mwanariadha wa Uganda Benjamin Kiplagat mwishoni mwa mwaka jana.
Mkimbiaji huyo wa mbio za kuruka viunzi kwenye Olimpiki aliuawa kwa kuchomwa kisu mkesha wa Mwaka Mpya katika mji wa Eldoret, unaojulikana kama kituo kikuu cha mafunzo kwa wanariadha.
"Matendo yako yalikuwa ya kikatili kwa mtu asiyeweza kujitetea ambaye ulikatisha maisha yake," Jaji Reuben Nyakundi aliambia Peter Ushuru Khalumi na David Ekai Lokere wakati wa kusikizwa kwa hukumu katika Mahakama Kuu ya Eldoret.
Mauaji ya Kiplagat yalishtua watu nchini Kenya, ambayo imeshuhudia mauaji ya wanariadha wengine kadhaa katika miaka ya hivi karibuni.
Tangazo
Hakimu alisema kuwa Khalumi na Lokere walimfuata Kiplagat aliyekuwa ndani ya gari lake, na kisha picha za CCTV zilionyesha kuwa walimuua kimakusudi katika hatua iliyopangwa. Sababu haswa ya mauaji hayo haikujulikana lakini wakati wa kukamatwa polisi walikuwa wamesema ni wizi.
Mnamo Jumatatu, katika ombi la hisia kwa mahakama, mamake mwanariadha huyo alimtaka Hakimu Nyakundi atoe kifungo cha maisha.
















