Charlie Hebdo: Gazeti lililosababisha mashambulio ya kigaidi Ufaransa lachapisha tena vibonzo vya Mtume Mohammad.

Chanzo cha picha, EPA
Gazeti la Charlie Hebdo nchini Ufaransa kwa mara nyengine tena limechapisha vibonzo vya Mtume Mohammad ambavyo vilisababisha gazeti hilo kulengwa katika mashambulio baya la kigaidi 2015.
Uchapishaji huo unajiri siku moja kabla ya watu 14 kuwasilishwa mahakamani wakituhumiwa kwa kuwasaidia washambuliaji wawili waliohusika na shambulio hilo tarehe 7 mwezi Januari 2015.
Watu 12 waliuawa, akiwemo mchoraji maarufu wa vibonzo.
Watu watano walifariki katika shambulio jingine lililohusishwa na vibonzo hivyo mjini Paris siku kadhaa baadaye.
Mashambulio hayo yalikuwa wimbi la mashambulio ya Wanajihad.
Ukurasa wa mbele wa toleo jipya unaonyesha vibonzo 12 vya Mtume Mohammad, ambavyo vilichapishwa katika gazeti la Denmark kabla ya kuchapishwa katika gazeti la Charlie Hebdo.
Kibonzo kimoja kinamuonesha Mtume Mohammad amevalia bomu badala ya kitambaa cha kichwa wanachojifunga wanaume.
Kichwa kikuu cha gazeti hilo kilisema ''Yote hayo kwa hili''.
Katika Uhariri wake , gazeti hilo linasema kwamba mara kwa mara limekuwa likitakiwa kuchapisha vibonzo vya Mtume Mohammad tangu mauaji hayo ya 2015.
Tumekuwa tukikataa mara kwa mara kufanya hivyo, sio kwamba haturuhusiwi - sheria inaturuhusu kufanya hivyo -lakini kwasababu kulikuwa na sababu nzuri ya kufanya hivyo - sababu ambayo ina maana na ambayo inaleta kitu cha kujadili, ilisema.
Kwa kuchapisha tena vibonzi hivi katika wiki ya kesi ya shambulio la kigaidi la Januari 2015 inaonesha umuhimu wake kwetu.
Je ni nini kinachotarajiwa katika kesi hiyo
Watu 14 wanatuhumiwa kupata silaha na kuwasaidia washambuliaji wa afisi za gazeti la Charlie Hebdo mjini Paris, mbali na kushambulia duka moja la Wayahudi na afisa mmoja wa polisi.
Washukiwa watatu wanafanyiwa kesi bila wao wenyewe kuwepo kwasababu wanaaminika kutorokea Kaskazini mwa Syria na nchini Iraq.
Inaaminika kwamba kuna takriban watu 200 wanaodaiwa kuhusika na manusura wa shambulio hilo wanatarajiwa kutoa ushahidi, kulingana na ripoti za chombo cha habari cha Ufaransa RFI.
Kesi hiyo ilitarajiwa kuanza mnamo mwezi Machi lakini ikaahirishwa kwasababu ya mlipuko wa virusi vya corona , Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea hadi mwezi Novemba
Je ni nini kilichofanyika 2015?
Mnamo tarehe On 7 Januari, ndugu wawili Said na Cherif Kouachi walivamia ofisi za gaeti la Charlie Hebdo , na kuwafyatulia risasi kiholela waliokuwepo na kumuua muhariri Stephanie Charbonnier maarufu Charb , waandishi wawili wa safu, muhariri wa nakala, mgeni mmoja aliyekuwa akihudhuria mkutano na msimamizi.
Mlinzi wa muhariri na afisa wa polisi pia waliuawa.

Chanzo cha picha, EPA
Huku maafisa wa polisi wakijaribu kuwasaka ndugu hao wawili- ambao baadaye waliuawa - kisa chengine kilizuka mashariki mwa mji wa Paris.
Amedy Coulibaly, ambaye alikuwa mshirika wa ndugu wawili wa Kouachi , alimuua afisa wa polisi kabla ya kuwatekanyara watu kadhaa katika duka moja la Wayahudi.
Aliwaua wanaume wanne Wayahudi tarehe 9 Januari kabla ya kupigwa risasi na maafisa wa polisi.
Katika kanda ya video aliyoirekodi Coulibaly ilisema kwamba shambulio hilo limetekelezwa kwa jina la Islamic State.
Kwanini Gazeti la Charlie Hebdo lililengwa na magaidi?
Kejeli za gazeti la Charlie Hebdo ziikiwalenga watu wa mrengo wa kulia , na masuala ya Ukatoliki ,Uyahudi na Uislamu - zimezua utata kwa muda mrefu.
lakini ni jinsi lilivyomuangazia Mtume Mohammad ndiposa lilivutia vitisho vya kifo dhidi ya waandishi wake na shambulio la bomu la petroli katika ofisi zake 2011.
Charb alitetea sana vibonzo hivyo kama ishara ya uhuru wa kujielezea. Siwalaumu Waislamu kwa kutocheka michoro yetu, aliambia chombo cha habari cha AP mwaka 2012.
Naishi chini ya sheria za Ufaransa siishi chini ya sheria za Kuran.
Kufuatia shambulio hilo la 2015, maelfu ya watu waliandamana wakipinga shambulio hilo na alama ya reli #JeSuisCharlie (Mimi ni Charlie) ilianza kusambaa kote duniani.












