Kwanini papa hushambulia wanadamu?

Chanzo cha picha, getty images
- Author, Richard Gray
- Nafasi, BBC
Mashambulizi ya papa ni matukio ya nadra sana. Lakini yanapotokea, yanaweza kuwa mabaya. Swali ni; kwa nini papa hushambulia watu?
Kulikuwa na takribani watu 83 duniani kote walioshambuliwa na papa mwaka 2009. Ni takwimu ambazo zimesalia katika kiwango hicho kwa muongo mmoja uliopita.
Idadi ya mashambulizi kwa wastani kati ya 2013-2017, ilikuwa ni 84. Mwaka 2023, kulikuwa na matukio 69 ya watu kushambuliwa na papa ghafla na mashambulizi 22 baada ya kuwachokoza, kulingana na Jalada la Kimataifa la Mashambulizi ya Papa katika Makumbusho ya Florida ya Historia ya Maliasili.
Kumi na nne ya mashambulizi haya yalisababisha vifo na kumi kati ya hayo yalihesabiwa kuwa ni mashambulizi ya ghafla.
End of Pia unaweza kusoma
Mashambuliz ya Papa yameongezeka?

Chanzo cha picha, Getty Images
Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha mashambulizi ya papa katika sehemu fulani za dunia yanaonekana kuongezeka.
Mashariki mwa Marekani na kusini mwa Australia wameona viwango vya mashambulizi ya papa yameongezeka karibu mara mbili katika miaka 20 iliyopita, wakati Hawaii pia imeshuhudia ongezeko kubwa.
"Kushambuliwa na papa kuna uhusiano mkubwa na na idadi ya watu na idadi ya papa katika maji kwa wakati mmoja," anasema Gavin Naylor, mkurugenzi wa Mpango wa Florida wa Utafiti wa papa, ambao hurikodi Mashambulizi ya Papa.
"Kadiri papa na watu wanavyozidi kuwa mahali pamoja, ndivyo uwezekano wa kukumbana huongezeka."
Idadi kubwa ya watu katika pwani ya kusini ya Australia na pwani ya mashariki ya Marekani, inamaanisha kuna idadi kubwa ya watu katika maji
Katika msimu wa vuli wa 2019, Massachusetts ilipata shambulio lake la kwanza baya la papa baada ya kupita miaka 82 na kuongezeka idadi ya kuonekana papa kumesababisha kufungwa kwa ufuo huo.
New York pia ilishuhudia idadi kubwa ya mashambuliz ya papa 2022 - mashambulizi 12 ya kushtukiza kwa mujibu wa Jalada la Kimataifa la Mashambulizi ya Papa.
Sababu ni nini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hilo limetokana na uwepo wa papa wachanga, waliothibitishwa 2016 ambao wamefanya makazi katika ghuba ya Great South, kati ya kisiwa cha Long na kisiwa cha Fire Island.
Inaaminika papa wachanga - wasio na uzoefu wanavutwa kwenye eneo hilo na mawimbi na wingi wa samaki, na kuufanya uwezekano wa kukutana na binadamu kuwa mkubwa wakati wa kuogelea.
Lakini hakuna ushahidi kwamba papa wanawinda wanadamu, kulingana na wanasayansi wanaowachunguza.
Papa weupe kwa mfano katika bahari ya Kaskazini ya Atlantiki, hufanya safari za msimu kwa kuhama maelfu ya maili hadi kwenye maji yenye joto zaidi kusini wakati wa miezi ya baridi kali.
Baadhi ya watu katika kipindi hicho hufanya safari baharini kwa miezi kadhaa, maelfu ya maili na kupiga mbizi hadi kina cha mita 1,000 kutafuta samaki. Hukutana nao.
"Sisi ni kama soseji ndogo zinazoelea majini," anasema Naylor. “Lichaya kuwa ni mlo rahisi kwa papa, lakini papa hawapendi sana kuwinda wanadamu. Kwa ujumla papa hupuuza watu.”
Naylor anaamini takwimu rasmi juu ya mashambulizi hazijuulikani. Kwani ripoti nyingi hutoka katika nchi zilizoendelea zenye idadi kubwa ya watu na vyombo vya habari vinavyofanya kazi sana.
Mashambulizi kwenye visiwa vya mbali au katika jamii ambazo hazijaendelea huenda hayaripotiwi.
Florida ndio ina idadi kubwa zaidi ya mashambulizi ya papa ulimwenguni. Kesi 16 zilitokea 2023, sawa na 44% ya jumla ya kesi za Marekani na 23% kote ulimwenguni.
Kulingana na Naylor, labda ni idadi kubwa ya watu katika maji ambapo papa wanaishi, na pia kuongezeka ripoti za mashambulizi ya papa kutokana na mitandao ya kijamii na habari za mtandaoni.
2020, kulikuwa na mashambulio 57 dhidi ya watu yaliyoripotiwa ulimwenguni na 73 mwaka 2021. Mwaka 2015, idadi hiyo ilikuwa 98.
Papa hushambulia mara nyingi karibu na kusini-mashariki mwa Marekani, wakihamia pwani ya Florida kutokana na kuongezeka joto la baharini ambalo limesababisha mawindo kuondoka.
Tabia za Papa

Chanzo cha picha, Getty Images
"Kuna aina 530 tofauti za papa,” anasema Blake Chapman, mwanabiolojia wa baharini ambaye amechunguza mifumo ya hisia wa papa na aliandika kitabu kuhusu shambulio la papa kwa wanadamu.
"Aina tofauti za papa zina tofautiana kulingana na baiolojia yao ya hisia, jinsi wanavyotenda, motisha zao na makazi wanayoishi."
Papa dume, kwa mfano, huwa na tabia ya kuwinda kwenye maji yasiyo na kina kirefu, ambayo huwafanya wasitegemee uwezo wao wa kuona na zaidi hutegemea kunusa na mapokezi ya hisia, ambayo huwaruhusu kutambua mawindo yao.
"Papa wakubwa weupe, mara nyingi huwinda katika maji safi sana na hutumia maono yao zaidi na macho yao ni bora zaidi," anasema Chapman.
Chpman anaamini, kando na kuongezeka kwa idadi ya watu katika ukanda wa pwani, uharibifu wa baharini, mabadiliko ya ubora wa maji, mabadiliko ya hali ya hewa na mabadiliko ya tabia za mawindo - kunasababisha papa kukusanyika kwa idadi kubwa katika maeneo yenye joto zaidi.
Mwaka 1992, kulikuwa na msururu wa papa kushambulia kwenye ufuo wa Recife, Brazili - eneo ambalo halikuwa na mashambulizi yoyote kwa muongo mzima uliopita.
Chapman anaamini ujenzi wa bandari kubwa ya kibiashara katika eneo hilo uliharibu maeneo makubwa ya miamba na mikoko, na kuwahamisha viumbe kama vile papa, ambao walihamia maeneo mapya kutafuta mawindo.
"Ikiwa wanyama hawa wanakimbiza samaki, na nyayo nyeupe ya mguu kutoka kwa mtu anayepiga teke maji huonekana – inaweza kumfanya papa kuirukia ghafla," anasema Naylor.
Jinsi ya Kujikinga

Chanzo cha picha, getty images
Lakini hali sio ya Kutisha. Huko Australia, kiwango cha shambulio la papa ni saw na 0.5 kwa kila watu milioni moja, huko Marekani ni chini ya mashambulizi 0.2 kwa watu milioni.
Kwa wale ambao wanaogopa na wanataka kujua jinsi ya kujikinga na papa, unashauriwa kumpiga papa anaekushambulia kwenye shavu lake au kumchoma machoni.
Kuogelea kwa vikundi na kukaa karibu na ufuo hupunguza hatari ya kushambuliwa. Kuvaa mavazi meusi na kuepuka kuvaa vito pia husaidia kupunguza uwezekano wa kuvutia macho ya papa.
Pia katika baadhi za fukwe, kuna mifumo iliyowekwa ya kutoa taarifa papa anapokaribia – inatumika hasa katika fukwe za Magharibi mwa Australia.
Mbinu nyingine inayojaribiwa huko Cape Town, Afrika Kusini, ni kebo ya sumaku-umeme ambayo inalenga kuwazuia papa wasikaribie maeneo yanayotumiwa na waogeleaji. Wanasayansi pia wamekuwa wakijaribu kizuizi cha sumakuumeme kama njia mbadala ya nyavu za papa.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












