Ligi Kuu England: Wachezaji kutoka Afrika watafanya nini msimu huu?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Ian Williams
- Nafasi, BBC Sport Africa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Baada ya kipindi chenye shughuli nyingi cha michuano ya Ulaya, Copa America na Olimpiki, sasa mashabiki wa soka barani Afrika kwa mara nyingine tena wanaelekeza macho yao kwenye Ligi Kuu ya England.
Msimu mpya utaanza Ijumaa pale Manchester United watakapowakaribisha Fulham huko Old Trafford.
Mshambuliaji wa Senegal Iliman Ndaiye, winga wa Ghana Ibrahim Osman na mlinzi wa Morocco Chadi Riad ni miongoni mwa wachezaji wapya wa Afrika waliojiunga na ligi inayofuatiliwa zaidi duniani.
BBC Sport Africa inajadili baadhi ya maswali makubwa ambayo yatajibiwa katika kipindi cha miezi tisa ijayo.
Salah atafanya nini chini ya kocha mpya?
Mohamed Salah ni moja ya wachezaji bora kutoka Afrika kuwahi kuingia katika Ligi Kuu ya England. Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Misri, hakuwa katika ubora wake katika msimu uliopita, aliporomoka mwishoni mwa msimu huku Liverpool ikishindwa kutwaa taji la ligi hiyo.
Mabao yake 18 katika Ligi Kuu ya England - matano kati ya hayo yalitokana na mikwaju ya penati – ni kiwango cha chini kabisa ya magoli tangu ajiunge na Liverpool mwaka 2017, ingawa pia alitoa pasi za magoli 10.
Jeraha lilimfanya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 kukosa mechi nyingi za Kombe la Mataifa ya Afrika 2023, pamoja na mechi kadhaa za nyumbani, na tatizo lilionekana kuzidi mwezi Aprili pale alipoingia katika mzozo na kocha Jurgen Klopp .
Kikosi hicho cha Anfield bado hakijafanya usajili mpya chini ya kocha mpya Arne Slot. Hivyo Salah anabaki kuwa mchezaji wao muhimu. Je, Liverpool itaongeza mkataba wa Mfalme huyo wa Misri hadi Mei ijayo? Hilo bado halijafahamika.
Minteh ana thamani ya pauni milioni 30?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Moja ya uhamisho wa kustaajabisha wa majira ya kiangazi, ni wa winga wa Gambia, Yankuba Minteh, ambaye msimu uliopita alichezea timu ya Feyenoord ya Netherlands chini ya kocha Slot.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 alijiunga na Newcastle akitokea Odense ya Denmark mwezi Juni mwaka jana kwa ada ya pauni milioni 5, lakini ghafla akatolewa kwa mkopo.
Baada ya mabao 10 katika mechi 27 za ligi ya Eredivisie, Everton, Lyon na Borussia Dortmund zote zilionyesha nia ya kumtaka, lakini Brighton ndiyo iliyolipa pauni milioni 30 kumnunua mchezaji huyo.
Kocha Tom Saintfiet, aliyemchezesha Minteh katika mechi yake ya kwanza ya kimataifa akiwa na umri wa miaka 18, ameimbia BBC Sport Africa kuwa:
"Huu ni msimu wake wa kujifunza kwa kiwango cha juu na kama (Brighton) watamuunga mkono na kumpa muda na kumwacha akue, nina uhakika baadaye katika msimu ataimarika na kuonyesha uwezo wake halisi."
Saintfiet anamtaja Minteh kama mwenye "kipaji cha kuvutia, kasi kubwa, kupiga chenga pamoja na uwezo wa kufunga mabao.”
Nao mashabiki wa Brighton wana matumaini atafanya vyema.
Partey ana umuhimu gani kwa Arsenal?
Wakati Arsenal ilipotumia pauni milioni 45, kumnunua Thomas Partey mwezi Oktoba 2020, kulikuwa na matumaini angeongeza nguvu na utulivu kwenye safu yao ya kiungo.
Lakini baada ya kucheza mechi 95 za Ligi Kuu England, kwa misimu minne, mchango wa Mghana huyo umekuwa mdogo kwa sababu ya majeraha kadhaa.
"Sina hakika kuwa Partey ndiye jina la kwanza kwenye jedwali la timu," anasema mchambuzi wa soka James Cook na mwendesha wa kipindi cha mtandaoni cha Same Old Arsenal.
"Amepoa sana, hayuko imara kama alivyokuwa huko nyuma. Na hilo linaleta wasiwasi sana."
Msimu uliopita Mike Arteta alimwanzisha Partey, 31, katika mechi tano za mwisho kuwania taji la ligi. Licha ya kushindwa kulitwaa lakini walishinda michezo yote mitano.
"Nadhani Arteta alikuwa akitaka kuimarisha safu ya kiungo," anasema Cook, ambaye anaamini klabu hiyo inahitaji kujiimarisha eneo hilo.
"Huwezi tu kumtegemea Partey kuwa sawa katika kipindi chote cha msimu."
Akiwa amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake, ikiwa anaweza kuisaidia Arsenal kushinda taji la kwanza ndani ya miaka 21 basi itakuwa njia nzuri ya kusema ‘kwaheri.’
Huu ndio msimu wa Sarr kung'ara?
Mkufunzi wa Tottenham, Ange Postecoglou alipoanza ukufunzi wake msimu uliopita, ilidhihirika kuwa kiungo wa kati wa Senegal, Pape Sarr alikuwa sehemu muhimu ya timu hiyo.
Licha ya jeraha na mapumziko ya katikati ya msimu kwa ajili ya Afcon, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 alianza katika mechi 27 za Ligi Kuu ya England msimu wa 2023-24.
"Alipoamua kujiunga na Tottenham, wengi walikuwa na shaka kuhusu umbile lake na mahitaji ya Ligi Kuu," anasema Babacar Ndaiye Faye wa BBC Afrique.
“Lakini msimu wake wa kwanza chini ya Postecoglou ulimtuliza kila mtu. Ikiwa Sarr anaweza kujiamini, Spurs watakuwa na mchezaji mzuri."
Waafrika katika timu zilizopanda

Chanzo cha picha, Getty Images
Msimu uliopita ilikuwa ni mara ya pili tangu Ligi Kuu ilipoanza mwaka 1992, ambapo timu zote tatu zilizopanda daraja zilishuka tena.
Ipswich Town, Leicester City na Southampton zitakuwa na matumaini ya kupata mafanikio baada ya Burnley, Luton na Sheffield United zote kufeli.
Leicester wanategemea zaidi wachezaji wa Kiafrika ndani ya kikosi chao, watakuwa na furaha kumpa kiungo mzoefu wa Nigeria Wilfred Ndidi mkataba mpya .
Nyota wa Zambia, Patson Daka na mshambuliaji wa Ghana Abdul Fatawu walikuwa washambuliaji wa kikosi cha kwanza msimu uliopita, lakini waliweza tu kufunga mabao 13 kwa jumla katika ligi ya Championship.
Ipswich, imerejea kwenye ligi kuu baada ya kukosekana kwa miaka 22, chini ya nahodha wao na kiungo wa kati wa Misri, Sam Morsy, na beki wa DR Congo Axel Tuanzebe, wote watakuwa sehemu ya kikosi chao.
Vipaji vya Southampton kutoka Afrika vitakuwepo uwanjani, kiungo mshambuliaji kutoka Nigeria Joe Aribo anatarajiwa kuwemo katika kikosi.
Mkufunzi wa Saints Russell Martin hivi karibuni alimwita mshambulizi wa Super Eagles, Paul Onuachu, ambaye alitumia msimu uliopita kwa mkopo huko Trabzonspor, kuwa "mchezaji wa kipee" baada ya maandalizi ya msimu mpya.
Winga wa Ghana, Kamaldeen Sulemana bado hajang'ara katika kipindi cha miezi 18 klabuni hapo na ameondolewa kwenye mechi ya ufunguzi kutokana na jeraha.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












