Kwa nini Israel imeugawa Ukanda wa Gaza kwa sehemu mbili?

"Sasa kuna Gaza upande wa kaskazini na Gaza upande wa kusini," msemaji wa jeshi la Israel, Daniel Hagari, alisema Jumapili usiku.

Kauli ya Hagari iliambatana na usiku wa mashambulizi makali ya Israel na kuzima intaneti huko Gaza, aliripoti Rushdi Abualouf, mwandishi wa habari wa BBC akiwa Gaza.

Mkurugenzi wa hospitali ya Al-Shifa katika jiji hilo aliripoti watu walikuwa wakisafirisha miili kwa punda na kwa magari yao wenyewe kwa sababu huduma ya magari ya wagonjwa zilikuwa hazifanyi kazi.

Jeshi la Israel linasisitiza kuwa Hamas inatumia hospitali kaskazini mwa Gaza kwa "madhumuni ya kijeshi," jambo ambalo mkurugenzi wa hospitali ya Al-Shifa anakanusha, akieleza hospitali hiyo iko wazi kwa ukaguzi wa Umoja wa Mataifa.

Hadi kufikia Jumatatu, idadi ya waliofariki Gaza tangu Israel ilipoanza kulipua eneo hilo kwa mabomu imefikia 10,022, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas.

Israel kwenye barabara kuu

Vifaru vya Israel vimeonekana kwenye barabara kuu ya Saladin ya Ukanda wa Gaza, ambayo inaunganisha kaskazini na kusini mwa eneo hilo.

Inaonekana wazi kuligawa eneo la kusini na kaskazini kilikuwa kipaumbele cha Israel, anasema mwandishi wa BBC wa masuala ya kidiplomasia Paul Adams.

Mapigano makali yameripotiwa katika maeneo ya wazi kati ya barabara kuu ya Saladin na pwani. Majengo kadhaa katika eneo hilo, kama vile Hospitali ya Friendship ya Uturuki ilishambuliwa.

Majengo mengine kama vile Chuo Kikuu cha Al-Azhar, chenye majengo mapya ya kifahari yanayofadhiliwa na Morocco na Saudi Arabia, yameharibiwa kabisa na milipuko ya mabomu ya mwishoni mwa wiki.

Kadhalika, njia nyingine inayounganisha kaskazini na kusini - barabara ya Al Rashid, ilikuwa imejaa magari ya kivita ya Israel mwishoni mwa wiki iliyopita, Adams anasema.

Mashambulizi kote Gaza

Licha ya wito wa mara kwa mara wa Israel kuwataka raia wa kaskazini mwa Gaza kuhamia kusini, Israel inaendelea kushambulia maeneo yote. Jumamosi Israel ilishambulia kambi ya wakimbizi ya Maghazi, iliyoko katikati mwa Gaza.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alitangaza hivi karibuni kwamba mashambulizi ya vikosi vyake yanaendelea katika Mji wa Gaza, ambao umezingirwa kabisa.

Israel inaendelea kuwahimiza zaidi ya raia 300,000 kaskazini mwa Gaza kuondoka, lakini wale ambao hawataki au hawawezi kuondoka wamejikuta katikati ya vita vikali.

Maumivu ya familia za mateka

Kivuko cha mpaka cha Rafah kati ya Gaza na Misri kilifunguliwa tena Jumatatu hii kwa raia wa kigeni au raia wa nchi mbili na kwa waliojeruhiwa vibaya.

Rafah imekuwa kivuko pekee cha wazi cha kuingia na kutoka Gaza tangu Hamas iliposhambulia Israel tarehe 7 Oktoba na jeshi la Israel kuanza mashambulizi yake ya kulipiza kisasi.

Kwa upande mwingine, wito unaendelea nchini Israel kwa serikali kufanikisha kuachiliwa kwa mateka zaidi ya 240 - miongoni mwao wanawake, watoto na wazee - ambao kikundi cha Kiislamu kiliwakamata katika uvamizi wake wa awali, ambao ulisababisha zaidi ya Waisraeli 1,400 kuuawa.

Adva Adar, ambaye bibi yake mwenye umri wa miaka 85 alitekwa nyara na Hamas, aliiambia BBC ana uhakika mashambulizi ya Israel yanalenga kuwakomboa mateka.

"Ikiwa wanafanya uvamizi wa ardhini huko Gaza, basi wanafanya hivyo kwa sababu inaweza kusaidia kuwarudisha mateka," anasema kwa simu kutoka Israel.

"Kama siamini, siwezi kuwa na matumaini. Na ikiwa siwezi kuwa na matumaini, sina sababu ya kuamka asubuhi. Ninahitaji kuamini kwamba atarudi," alihitimisha.

Blinken na ujumbe wake

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amerejea Mashariki ya Kati. Jumatatu hii alikuwa mjini Ankara, mji mkuu wa Uturuki, akizungumza na viongozi wa Uturuki.

Afisa huyo wa Marekani ametoa ujumbe ambao umma wake wa Marekani unataka kusikia. Alimhakikishia kiongozi wa Mamlaka ya Palestina, Rais Mahmoud Abbas, kwamba baada ya vita, serikali yake inapaswa kuchukua mamlaka huko Gaza.

Pia alilaani ghasia za walowezi katika Ukingo wa Magharibi, na kusema anataka kupunguza majeruhi ya raia wa Palestina huko Gaza na kuboresha hali ya maisha.

Pia aliiambia Israel unapokuwa na uungwaji mkono wa 100%, wa kijeshi na kidiplomasia, lazima ufanye kwa mujibu wa sheria za kimataifa.