Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Putin anaweza kulipiza kisasi uasi wa kiongozi wa Wagner - Mkuu wa CIA
Rais wa Urusi Vladimir Putin anajaribu kupoteza muda anapotafuta jinsi ya kukabiliana na Yevgeny Prighozin, anasema mkurugenzi wa CIA.
Bw Prigozhin ni mkuu wa kundi la mamluki la Wagner ambaye aliongoza uasi nchini Urusi mwezi mmoja uliopita.
Uasi huo ulifichua udhaifu mkubwa katika mfumo wa mamlaka aliyojenga Putin, mkuu wa CIA William Burns alisema.
Aliliambia Baraza la Usalama la Aspen kwamba kiongozi wa Urusi bado anaweza kutaka kulipiza kisasi dhidi ya Bw Prigozhin.
"Tunachokiona ni mchezo mgumu sana," mkuu wa CIA alisema Alhamisi.
Bw Prigozhin amezunguka lakini alikuwa katika mji mkuu wa Belarus wa Minsk hivi majuzi na Urusi, alisema alipoulizwa kuhusu video ya hivi karibuni inayomuonesha mkuu wa Wagner huko Belarus.
Bw Putin huenda anajaribu kuvuta muda anapotafuta namna bora ya kukabiliana na kiongozi wa kundi la Wagner, Bw Burns aliongeza.
Kundi hilo la mamluki bado lina thamani kwa uongozi wa Urusi katika maeneo kama vile Afrika, Libya na Syria na hivyo basi kulikuwa na uwezekano kwamba Bw Putin angejaribu kulitenganisha kundi hilo na kiongozi wake.
Naye mkuu wa CIA alisema kuwa Bw Putin anaweza kusubiri kulipiza kisasi.
"Putin ni mtu ambaye kwa ujumla anadhani kulipiza kisasi ni jambo bora zaidi," Bw Burns alisema. "Kwa uzoefu wangu, Putin ni mtu wa kulipa kisasi kwa hivyo nitashangaa ikiwa Prigozhin ataepuka kuadhibiwa zaidi."
Mapema mwezi huu, Rais wa Marekani Joe Biden alisema kuna hatari kwamba kiongozi wa Wagner anaweza kupewa sumu.
"Kama ningekuwa yeye ningekuwa mwangalifu nilichokula. Ningeweka macho yangu kwenye menyu yangu," rais alidakia.
Mkurugenzi wa CIA aliunga mkono wazo hilo akisema: "Kama ningekuwa Prigozhin, sitamfukuza mwonjaji wangu wa chakula."
Shirika la ujasusi lilikuwa linafahamu kuhusu uasi huo, Bw Burns alisema, akithibitisha ripoti za awali.
Jenerali mkuu wa jeshi la Urusi, Sergei Surovikin, ambaye aliripotiwa kujua mapema kuhusu uasi wa Wagner, pia hana "uhuru wa kutembea" kwa sasa, mkuu wa CIA aliongeza.
Uasi huo ulikuwa ni shambulio la moja kwa moja ambalo Bw Putin amewahi kuona katika miaka yake 23 madarakani, ikiwa ni pamoja na kupinga moja kwa moja uhalali wa Kremlin kwa vita vya Ukraine, huku Bw Prigozhin akisema kuwa yamejengwa juu ya uongo, Bw Burns alisema.
Aliongeza kuwa cha kushangaza zaidi ni kwamba kiongozi wa Urusi alihisi kulazimishwa kufanya makubaliano na mtu ambaye aliwahi kuwa mhudumu wake, mkuu wa CIA alisema.
Bw Prigozhin mara nyingi hujulikana kama "mpishi wa Putin" kwani alipata umaarufu baada ya kutoa huduma za upishi kwa Bw Putin na wanajeshi kabla ya kuanzisha kundi la Wagner.
Saa 36 za uasi huo zitakuwa zimewaacha wengi nchini humo na swali la "ikiwa mfalme hakuwa na nguo au angalau kwa nini inamchukua muda mrefu sana kuvalia", Bw Burns alisema.
Hili lingeibua maswali mazito zaidi kwa wasomi wa Urusi kuhusu uamuzi wa Bw Putin, ambao umekuwapo tangu uamuzi wake wa kuzindua uvamizi kamili wa Ukraine mnamo Februari 2022.
Iwapo Ukraine itapiga hatua zaidi katika uwanja wa vita basi hilo linaweza kusababisha Warusi zaidi kutilia maanani ukosoaji wa Bw Prigozhin wa vita hivyo, alisema.