Uchaguzi wa Marekani 2024: Ijue familia ya Donald Trump

    • Author, Ana Faguy
    • Nafasi, BBC News, Washington
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Kabla ya siasa, Donald Trump alijenga himaya yake kwa biashara ya mamilioni ya pesa.

Jina lake sasa - ni sawa na Chama cha Republican, na watu mbalimbali wa familia ya Trump sasa wana ushawishi.

Hawa ni baadhi ya wana familia mashuhuri.

Donald Trump Jr

Donald Trump Jr, mtoto mkubwa wa Trump, yupo karibu zaidi na Baba yake tangu aondoke Ikulu ya White House.

Alikuwa maarufu katika vyombo vya habari wakati wa uteuzi wa mgombea mwenza wa Trump JD Vance ambaye, alisema. "Ni chaguo zuri." Katika Kongamano la Kitaifa la Republican (RNC).

Donald Trump Jr hapo awali alimuoa Vanessa Trump, ambaye wamepata watoto watano. Sasa amechumbiwa Kimberly Guilfoyle.

Pia unaweza kusoma

Eric Trump

Eric Trump, ni mtoto wa tatu wa Trump, amemshauri babake kuhusu masuala muhimu, kulingana na ripoti.

Haonekani sana kama kaka yake mkubwa na yuko zaidi katika biashara ya familia ya Trump.

Ivanka Trump and Jared Kushner

Ivanka Trump na Jared Kushne walikuwa ni wanafamilia wenye ushawishi mkubwa wakati wa muhula wa kwanza wa Trump katika Ikulu ya White House.

Wawili hao wameoana tangu 2009 na wana watoto watatu.

Wakati Trump akiwa madarakani, Ivanka alijitokeza mara nyingi kwa niaba ya baba yake na utawala wake.

Kushner alishikilia nafasi ya mshauri mkuu wa Ikulu ya White House kutoka 2017 hadi 2021.

Tiffany Trump

Mtoto wa nne wa rais na mtoto wa pekee wa Trump aliyezaa na mke wake wa pili, Marla Maples.

Hajaingia kwenye siasa katika kampeni za babake wala wakati akiwa Ikulu ya White House.

Ameolewa na Michael Boulos tangu 2022.

Kimberly Guilfoyle

Kimberly Guilfoyle na Donald Trump Jr wamekuwa pamoja kwa miaka sita na ni wachumba tangu 2020.

Alikuwa mtangazaji wa Fox News kutoka 2006 hadi 2018, kabla ya kuondoka na kuwa mwanachama wa kamati ya kumuunga mkono Trump (pro-Trump super PAC.)

Ni mfuasi mkubwa wa Trump, haswa katika vipindi vya runinga.

Aliolewa na Gavana wa California Gavin Newsom mapema miaka ya 2000.

Lara Trump

Ameolewa na Eric, ndiye nyota anayechipukia wa familia, haswa tangu aanze kuhudumu kama mwenyekiti mwenza wa Kamati ya Kitaifa ya Republican mapema mwaka huu. Ana watoto wawili na Eric.

Julai, alitoa hotuba kwenye mkusanyiko wa watu kuhusu baba-mkwe wake.

"Familia yetu inakabiliwa na vitisho vya kuuawa... hakuna kitu kigumu kama binti-mkwe kutazama mtu akijaribu kumuua mtu unayempenda," alisema.

Melania Trump

Mke wa Rais Melania Trump ameolewa na Trump tangu 2005.

Alionekana sana wakati wa muhula wa kwanza wa Trump, lakini amejitokeza mara chache hadharani tangu wakati huo.

Julai, alihudhuria mkutano wa chama, siku chache tu baada ya jaribio la mauji dhidi ya mume wake.

Anaunga mkono uamuzi wa kuavya mimba. Msimamo wake ni tofauti na ule wa mume wake ambaye amejipatia sifa kwa kusaidia kupindua sheria ya Roe v Wade, na kukandamiza haki ya kikatiba ya kutoa mimba.

Barron Trump, 18, ndiye mtoto wake wa pekee na Trump.

Barron Trump

Barron Trump kwa kiasi kikubwa amekaa nje ya siasa.

Mei, iliripotiwa kuwa angekuwa miongoni mwa wajumbe kutoka jimbo la Florida wanaohudhuria kongamano la Julai, lakini siku moja baadaye mama yake alisema amekataa ofa hiyo.

Alihitimu Oxbridge Academy huko Palm Beach, Florida, mwezi Mei na baba yake anasema sasa anasomea Biashara katika Chuo Kikuu cha New York.

Kai Trump

Kai Trump ndiye mjukuu mkubwa wa Trump na bintiye Donald Trump Jr na mkewe wa zamani Vanessa Trump.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 17 ni mcheza gofu na alizungumza kwenye mkutano kuhusu Trump alivyo kama babu.

“Kwangu mimi ni babu wa kawaida tu. Anatupa peremende na soda,” alisema.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla