Afcon 2023: Kombe la mataifa Afrika au soka la vilabu - kipi muhimu zaidi?

Vilabu vikuu vya soka duniani vinajiandaa kuwakosa wachezaji muhimu wakati wa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2023). Je, mjadala kuhusu klabu na timu ya taifa una mashiko?

Nyota wa Afrika wakiwemo Mohamed Salah, Victor Osimhen na Achraf Hakimi watakuwa nchini Ivory Coast katika mashindano yatakayoanza Januari 13 na kumalizika tarehe 11 Februari.

Ingawa mashindano hayo yatafanyika wakati wa mapumziko ya msimu wa baridi katika baadhi ya ligi za Ulaya, lakini vilabu vitakabiliwa na wiki kadhaa bila wachezaji wao wa kikosi cha kwanza.

Pia Unaweza Kusoma

Je, wachezaji wanakabiliwa na mtanziko?

Kiungo wa kati wa Brentford, Frank Onyeka anajiandaa kwa Afcon yake ya pili akiwa na Nigeria, baada ya kucheza nchini Cameroon mapema 2022.

"Siku zote nitataka kuwakilisha nchi yangu kwenye mashindano makubwa. Ni heshima kuvaa shati la kijani na nyeupe, kwa hivyo ni jambo ambalo sina budi kulifanya," aliiambia BBC Sport Africa.

"Nilikuwa mvulana nikicheza katika mitaa ya Nigeria na sasa ninawakilisha Super Eagles kwenye Afcon.

"Ndoto imetimia. Baada ya kutazama magwiji wa Afcon miaka ya nyuma, sasa nitakuwa sehemu ya timu. Nayasubiri mashindano kwa hamu sana."

Onyeka 25 yuko katika kikosi cha kwanza cha Brentford msimu huu pamoja na Waafrika wenzake Bryan Mbeumo (Cameroon) na Yoane Wissa (DR Congo).

Kuhusu klabu anasema, "haitakuwa rahisi. Lakini najua timu iko imara. Mtu anapoondoka, kuna mtu mwingine huchukua nafasi yake."

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp hapo awali alikosoa muda wa michuano hiyo kwani inachezwa wakati msimu ukiendelea. Onyeka anasema kocha mkuu wa Bees, Thomas Frank amekuwa akiwatia moyo na kuwapa uhakika.

"Anafuraha kwangu kuiwakilisha nchi yangu kwenye hatua hii kubwa. Nina furaha sana kwamba yeye pia ni kocha wangu msaidizi, atawaacha wachezaji wake na kwenda Afcon," alisema.

Hata hivyo kurejea Ligi Kuu ya Uingereza ilikuwa "vigumu sana" kwa Onyeka baada ya Afcon iliyopita, ambapo Nigeria ilitoka katika hatua ya 16 bora.

"Unaporudi unakuta timu imetulia, wanacheza vizuri," anasema. "Kuingia kwenye timu tena inachukua muda mrefu.”

Afcon ifanyike lini?

Mwaka 2017 Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf) liliamua kuhamisha mashindano hayo kutoka Januari-Februari hadi Juni-Julai - mashindano ya 2019 nchini Misri yakiwa ya kwanza kufanyika wakati huo.

Mashindano ya 2021 yalipelekwa Januari na Februari 2022, ili kuepusha hali mbaya ya hali ya hewa katika taifa mwenyeji Cameroon na kwa sababu ya janga la Uviko-19.

Mabadiliko hayo yamezuia ukosoaji kutoka kwa baadhi ya watu.

Jay-Jay Okocha aliyeshinda Kombe la Mataifa ya Afrika akiwa na Nigeria mwaka 1994, anasema muda wa Afcon unaweza kuwa na athari kubwa kwa wachezaji kutokana na mwingiliano wa kalenda.

"Imekuwa vigumu sana kwa wachezaji wa Kiafrika kucheza Januari au kuanza msimu na mapumziko ya msimu wa baridi mapema sana," Okocha aliiambia BBC.

"Ikiwa wanaweza kuhamisha Kombe la Dunia hadi Disemba kwa sababu ya joto ili kuendana na mataifa yanayoshiriki, kwa nini hawawezi kufanya kitu kama hicho katika Kombe la Mataifa ya Afrika, na kufanya kazi pamoja ili isiathiri mtu yeyote?"

"Najua makocha wengi wanaokataa kusajili wachezaji wa Kiafrika kwa sababu ya Afcon kuwa Januari, lakini watasajili Wabrazil ambao wanakwenda kucheza Copa America majira ya joto. Sio sawa."

Hisia mchanganyiko za mashabiki

Ghana, kama timu nyingi zitakazoshiriki Kombe la Mataifa ya Afrika 2023, ina majina mengi ya nyota wanaocheza katika baadhi ya vilabu vikubwa barani Ulaya.

Kiungo wa kati wa Arsenal Thomas Partey, Mohammed Kudus wa West Ham na mshambuliaji wa Crystal Palace, Jordan Ayew - ni miongoni mwa wale watakaoziacha timu zao za Ligi Kuu ya Uingereza na kwenda Ivory Coast.

Issahaku Abdul-Mumen, rais wa klabu ya mashabiki wa West Ham, Ghana Hammers, anasema, ‘bila Kudus, Ghana inaweza isifike mbali. Lakini Kudus anacheza katika kila mechi ya West Ham sasa. Mimi ni shabiki mkubwa wa Afcon.

“Lakini Kudus kuondoka West Ham utakuwa ni wakati mbaya sana kwetu. Ni wakati wa huzuni kwangu kama shabiki wa West Ham lakini kama shabiki wa Ghana nitafurahi."

Makocha wanakabiliwa na nini?

Ikiwa mashabiki wa Hammers wana wasiwasi juu ya kumkosa Kudus, hawako peke yao.

Mkufunzi wa West Ham, David Moyes anasema timu yake "itamkosa mshambuliaji wake Mohammed Kudus. Ni mchezaji mzuri sana kufanya naye kazi na bila shaka pasi na mabao yake ni muhimu."

"Ni pigo kubwa (kumkosa) kwa sababu anafunga mabao na kutengeneza pasi. Itabidi tutafute njia nyingine."

Hata hivyo meneja wa timu ya taifa ya Kudus, kocha wa Black Stars, Chris Hughton, anaamini kuwa mvutano kati ya klabu dhidi ya nchi ni wa muda mrefu.

Anasema makocha kote Ulaya kwa sasa wamejipanga pale wachezaji wao watakapoondoka kwa ajili ya michuano ya Afrika, na Afcon si sababu tena ya kutowasajili nyota wa Afrika.

"Vilabu vingi na makocha wanakubali wanapomchukua mchezaji wa Kiafrika kuna uwezekano wa kumkosa kwa muda wakati wa Kombe la Mataifa ya Afrika," anasema kocha huyo mwenye umri wa miaka 65.

Mashindano ya Afcon 2025, ambayo yatafanyika nchini Morocco, yalitarajiwa kurudishwa mwezi Juni na Julai - lakini hilo litapelekea kuingiliana na Kombe la Dunia la timu 32.

Bila suluhu ya haraka, wachezaji nyota wa bara la Afrika - wanaweza kukumbwa na vuta nikuvute nyingine katika muda wa miezi 18 ijayo.

Pia Unaweza Kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi