Chelimo Njoroge: Mama anayetoa maziwa ya kutosha watoto 50 na mengine kuogesha

- Author, Saida Swaleh
- Nafasi, BBC News, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Chelimo Njoroge anakumbuka wakati friji yake ilijaa kupita kiasi. "Nilijaza friji kubwa. Kisha friji ya kawaida. Halafu nikaanza kutumia friji ya dada yangu," anasema huku akicheka. Mama huyo mwenye umri wa miaka 36 na watoto wawili kutoka Nairobi aligundua kuwa alikuwa "mzalishaji mkubwa kupita kiasi" wa maziwa ya mama. Hata baada ya kumnyonyesha mtoto wake, bado alikuwa akizalisha lita nyingi zaidi kila wiki. Kwa hivyo, badala ya kuacha yapotee, alianza kuyatoa kama msaada kwa wamama wengine wenye uhitaji.
Kwa karibu mwaka mmoja, Chelimo amekuwa akiwasaidia wengine kimya kimya, akitoa maziwa yake ya ziada kwa akina mama wanane katika jamii yake, wakiwemo marafiki wa muda mrefu na hata marafiki wapya waliomtafuta baada ya kuona video zake mtandaoni.
"Niliona video zake za TikTok za maziwa kwenye friji na nikasema… wow," anasema Maryann Kibinda, mmoja wa walionufaika na maziwa ya Chelimo. "Nilimtafuta tu na kusema, 'Habari, ukoje? Nahitaji maziwa.' Ilikuwa hivyo tu." Siku yake ya mwisho ya kutoa maziwa, Chelimo alikabidhi lita 14.
Uzoefu wa Chelimo wa kunyonyesha haukuanza vizuri. Mwanawe alihangaika kushika ziwa, na ilimbidi atumie vifaa maalumu vya kushikia chuchu ili kutoa maziwa. Lakini hivi karibuni, maziwa yaliendelea kutoka haraka na kwa wingi kuliko kawaida .
"Katika kilele cha safari yangu ya kutoa maziwa, nilikuwa na maziwa ya kutosha kulisha watoto 50 katika kitengo cha watoto wachanga (neonatal unit)," anasema.
Alianza kuchapisha video kwenye TikTok, akieleza kuhusu changamoto za kihisia na kimwili za kunyonyesha, na kutoa vidokezo juu ya kuhifadhi maziwa na usafi. Mwanzoni, video zake zilionekana na watu wachache tu. Sasa zinafikia zaidi ya watu 16,000. Baadhi ya watazamaji ni wazalishaji wenza wa maziwa mengi. Wengine ni wazazi waliokata tamaa wanaotafuta msaada.
"Kuna akina mama wengi wanaotaka kusaidia maziwa ya mama. Lakini pia tuna wengine wengi sana wanaotaka kuyapokea," anasema. Kenya ina benki moja rasmi ya maziwa ya mama, iliyoko Hospitali ya Uzazi ya Pumwani jijini Nairobi. Lakini inakubali tu kupokea michango ya maziwa kutoka kwa akina mama ambao wamelazwa hospitalini, na maziwa hayo hutumiwa tu kwa watoto waliolazwa hospitalini.
Hali hii inawaacha wanawake kama Chelimo wakiwa na machaguo machache rasmi za kusaidia kutoa maziwa. "Hatuna hifadhi ya maziwa ya mama inayokubali maziwa kutoka kwa akina mama wanaozalisha maziwa kupita kiasi," anasema.

Benki ya taifa ya maziwa ya mama
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mkurugenzi wa Lishe wa Kaunti ya Nairobi, Esther Kwamboka Mogusu, anasema mpango ni kupanua uwezo wa Hospitali ya Uzazi ya Pumwani kuwa kituo cha ubora. "Tutajenga benki mbili zaidi za maziwa ya mama jijini ili tuweze kusaidia watoto wengine zaidi ya hospitali," anasema. Wizara ya Afya kwa kushirikiana na serikali ya Kaunti ya Nairobi na PATH inasema imefanya tathmini ili kuongeza upatikanaji wa maziwa salama ya mama yaliyotolewa na wafadhili kote nchini.
"Kama sehemu ya juhudi za kuweka rasmi mpango wa rafiki wa mama na Mtoto Plus (MBFI+), ikiwemo benki ya maziwa ya mama, Wizara imeanzisha uundaji wa Sera mpya ya kitaifa ya lishe," anasema Veronica Kirogo, Mkurugenzi wa Huduma za Lishe kutoka Wizara ya Afya, Kenya.
"Sera hiyo itatambua benki ya maziwa ya mama kama hatua muhimu ya kuboresha matokeo ya lishe ya watoto wachanga na kutoa mwongozo wa ujumuishaji wake katika mfumo mpana wa huduma za afya ya watoto wachanga na watoto."
Mkunga na mtaalamu wa unyonyeshaji Mary Mathenge anakubali kuwa kuna pengo katika utoaji wa huduma lakini pia anahimiza tahadhari. Akiwa amefanya kazi na akina mama wanaonyonyesha kwa zaidi ya miongo minne, anaamini Kenya inahitaji mfumo wa kitaifa wa kusimamia utoaji wa maziwa ya mama kwa usalama. "Mtoto yeyote anaweza kupokea maziwa ya mama kutoka kwa binadamu yeyote," anasema.
"Lakini chochote kinachoweza kupita kupitia damu kinaweza pia kupita kupitia maziwa ya mama. Mama lazima apimwe." "Kunapaswa kuwepo mifumo ya kuchunguza, kufuatilia, na kuhifadhi maziwa yaliyotolewa. Kwa njia hiyo, watoto wengi zaidi wanaweza kunufaika kwa usalama."

Chelimo anasema ametumia baadhi ya maziwa yake yaliyobaki kwa njia za ubunifu, kama vile kwa ajili ya kuogesha watoto (milk baths), ambayo huaminika kutuliza ngozi ya mtoto. Lakini mengi yameenda kwa familia ambazo, kwa sababu mbalimbali, zinahangaika kuwalisha watoto wao.
Juhudi zake zimesherehekewa mtandaoni, na amepewa jina la utani "Malaika wa dhahabu ya kimiminika" (The Liquid Gold Angel).
Lakini Chelimo haraka anawakumbusha watu kuwa hii si safari yake pekee. "Hii si safari ya Chelimo tu," anasema. "Kuna akina mama wengi kama mimi."
Anapofunga mlango wa friji yake kwa mara ya mwisho, anatumai mazungumzo kuhusu utoaji wa maziwa ya mama yataendelea kukua na kwamba akina mama wengi zaidi watapata mifumo salama na rasmi ya kutoa na kupokea maziwa.
"Na ujumbe wangu kwa akina mama wengine wanaonyonyesha huko nje ni endeleeni kujitahidi."















