Kampuni ya dawa ya India inavyochochea matumizi ya dawa za kulevya Afrika Magharibi

EFDCX
Maelezo ya picha, Akirekodiwa kwa siri, Vinod Sharma amesema dawa ya kampuni ya Aveo ina "madhara sana," na kuongeza "hii ni biashara".
Muda wa kusoma: Dakika 6

Uchunguzi wa BBC Eye umebaini kuwa kampuni ya dawa kutoka India inatengeneza dawa zisizo na leseni, zinazolevya na kuzisafirisha kinyume cha sheria hadi Afrika Magharibi ambako zinasababisha tatizo mkubwa kwa afya ya umma katika nchi zikiwemo Ghana, Nigeria na Cote D'Ivoire.

Kampuni ya Aveo Pharmaceuticals, iliyoko Mumbai, hutengeneza aina mbalimbali za vidonge ambavyo huvipa majina na chapa tofauti na kuviweka kwenye paketi ili kuonekana kama dawa halali. Lakini dawa zote hizo ni mchanganyiko huo huo wa tapentadol (dawa inayolevya) na carisoprodol (dawa ya kutuliza misuli ambayo ina uraibu na imepigwa marufuku Ulaya.)

Mchanganyiko huu wa dawa haujaidhinishwa kutumiwa popote duniani na unaweza kusababisha matatizo ya kupumua na kifafa. Ukiitumia sana inaweza kukuua. Licha ya hatari hizo, dawa hizi za kulevya ni maarufu mitaani katika nchi nyingi za Afrika Magharibi, kwa sababu ni nafuu sana na zinapatikana kwa wingi.

BBC ilipata pakiti zake, zikiwa na nembo ya Aveo, zinazouzwa katika mitaa ya miji ya Ghana, Nigeria, na Ivory Coast.

Baada ya kufuatilia dawa hizo katika kiwanda cha Aveo nchini India, BBC ilituma shushushu ndani ya kiwanda hicho, akijifanya kama mfanyabiashara Mwafrika anayetaka kusambaza dawa za kulevya nchini Nigeria. Kwa kutumia kamera iliyofichwa, BBC ilimrekodi mmoja wa wakurugenzi wa Aveo, Vinod Sharma, akionyesha dawa hiyo hatari ambayo BBC ilikuta ikiuzwa kote Afrika Magharibi.

Katika video iliyorekodiwa kwa siri, shushushu huyo anamwambia Sharma kwamba mpango wake ni kuuza tembe hizo kwa vijana nchini Nigeria "ambao wote wanapenda bidhaa hii."

Sharma hakusita, akajibu. "Sawa," kabla ya kueleza kwamba ikiwa watumiaji watachukua vidonge viwili au vitatu kwa wakati mmoja, wanaweza "kupumzika" na anakubali wanaweza "kulewa." Kufikia mwisho wa mkutano huo, Sharma anasema: "Hii ni hatari sana kwa afya," na kuongeza "siku hizi, hii ni biashara."

Pia unaweza kusoma

Afrika Magharibi

FC
Maelezo ya picha, Kikosi kazi huko Tamale kinaamini kuwa mtu huyu alikuwa ametumia Tafrodol, ambayo waliipata katika uvamizi huo

Ni biashara ambayo inaharibu afya na kuharibu uwezo wa mamilioni ya vijana kote Afrika Magharibi.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika mji wa Tamale, kaskazini mwa Ghana, vijana wengi wanatumia dawa haramu na kupelekea mmoja wa machifu wa jiji hilo, Alhassan Maham, kuunda kikosi kazi cha hiari cha wananchi wapatao 100 ambao dhamira yao ni kuwavamia wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kuchukua tembe hizi.

"Dawa hizo huteketeza akili za wale wanaozitumia vibaya," anasema Maham, "kama moto unavyowaka wakati mafuta ya taa yanapomwagwa juu yake."

Mraibu mmoja huko Tamale anasema, dawa hizo "zimepoteza maisha yetu."

Timu ya BBC uliungana na jopo kazi hilo waliporukia pikipiki, kufuatia kujulishwa kuhusu dawa hizo, jopo hilo lilianza uvamizi katika mojawapo ya vitongoji maskini zaidi vya Tamale. Wakiwa njiani walimkuta kijana mmoja amelala hajielewi. Kwa mujibu wa wenyeji wanasema alikuwa ametumia dawa hizo.

Walipomnasa mfanyabiashara mwenyewe, walimkuta amebeba mfuko wa plastiki uliojaa vidonge vya kijani vilivyoandikwa Tafrodol. Pakiti hizo zimegongwa muhuri wa nembo ya Aveo Pharmaceuticals.

Sio tu huko Tamale ambapo vidonge vya Aveo vinasababisha taabu. BBC iligundua dawa kama hizo, zilizotengenezwa na Aveo, zimekamatwa na polisi nchini Ghana.

Pia tulipata ushahidi kuwa vidonge vya Aveo vinauzwa katika mitaa ya Nigeria na Cote D'Ivoire, ambapo vijana huviyeyusha katika kinywaji cha pombe ili kuongeza nguvu yake.

Taarifa zinaonyesha Aveo Pharmaceuticals, pamoja na kampuni dada inayoitwa Westfin International, husafirisha mamilioni ya vidonge hivi hadi Ghana na nchi nyingine za Afrika Magharibi.

Nigeria, yenye idadi ya watu milioni 225, ni soko kubwa zaidi la tembe hizi. Inakadiriwa kuwa takriban Wanigeria milioni nne wanatumia aina fulani ya dawa za kulevya, kulingana na Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Nigeria.

Mwenyekiti wa Shirika la Kupambana na Dawa za Kulevya na Utekelezaji wa Sheria nchini Nigeria (NDLEA), Brig Jenerali Mohammed Buba Marwa, aliiambia BBC, dawa za kulevya "zinaharibu vijana wetu, familia zetu, ziko katika kila jamii nchini Nigeria."

Mchanganyiko hatari

F
Maelezo ya picha, Pakiti za Tafrodol zenye chapa ya Aveo zilinaswa katika uvamizi huko Tamale, nchini Ghana.

Mwaka 2018, kufuatia uchunguzi wa BBC Africa Eye kuhusu uuzaji wa dawa za kulevya mitaani, serikali ya Nigeria ilijaribu kuzuia dawa ya kulevya ya kutuliza maumivu inayoitwa tramadol.

Serikali ilipiga marufuku uuzaji wa tramadol bila agizo la daktari, iliweka vizuizi vikali, na kuharibu mtandao haramu wa uagizaji wa tembe hizo. Wakati huo huo, serikali ya India iliimarisha kanuni za usafirishaji wa tramadol.

Muda mfupi baadaye, Aveo Pharmaceuticals ilianza kuuza kidonge kipya cha tapentadol, dawa yenye nguvu zaidi, iliyochanganywa na dawa ya carisoprodol ya kutuliza misuli.

Maafisa wa Afrika Magharibi wanaonya kwamba wauzaji wa dawa za kulevya wanaonekana kutumia tembe hizi mpya kama mbadala wa tramadol na kukwepa vizuizi vya serikali.

Katika kiwanda cha Aveo kulikuwa na katoni za dawa, katoni hizo zinakaribia kugonga dari. Juu ya meza yake, Vinod Sharma alikuwa na pakiti za tembe za tapentadol-carisoprodol ambazo kampuni hiyo inaziuza kwa majina mbalimbali ikiwa ni pamoja na Tafrodol, maarufu zaidi, pamoja na TimaKing na Super Royal-225.

Alimwambia shushushu wa BBC kwamba "wanasayansi" wanaofanya kazi katika kiwanda chake wanaweza kuchanganya dawa tofauti ili "kutengeneza bidhaa mpya."

Dawa mpya ya Aveo ya tapentadol ni hatari zaidi kuliko tramadol, kulingana na Dk Lekhansh Shukla, profesa msaidizi katika Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Akili na Sayansi ya mfumo wa fahamu huko Bengaluru, India,

Anasema "tapentadol pekee ina athari kama dawa ya kulevya, hukupa usingizi mzito sana. Inaweza kusababisha shida ya kupumua, ikitumiwa kupita kiasi" alielezea. "Na mchanganyiko huu wa tapentadol na carisoprodol hukupa usingizi mzito. Huu ni mchanganyiko hatari sana."

Dawa ya carisoprodol imepigwa marufuku barani Ulaya kwa sababu ina uraibu. Imeidhinishwa kutumika Marekani lakini kwa muda mfupi tu wa hadi wiki tatu. Ukiacha kuitumia unapata wasiwasi, kukosa usingizi, na maono.

Anasema hakuna majaribio ya kimaabara yamefanyika kuhusu mchanganyiko huo. Tofauti na tramadol, ambayo ni halali kwa matumizi katika dozi ndogo. Lakini tapentadol-carisoprodol "hauonekani kuwa ni mchanganyiko salama," anasema. "Hiki si kitu ambacho kimeidhinishwa kutumika katika nchi yetu."

Nchini India, makampuni ya dawa hayawezi kutengeneza na kuuza nje dawa zisizo na leseni isipokuwa dawa hizi zikidhi viwango vya nchi inayoagiza. Aveo husafirisha Tafrodol hadi Ghana, ambapo mchanganyiko huu wa tapentadol na carisoprodol, kulingana na Wkala wa Kitaifa wa Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Ghana, hauna leseni na ni kinyume cha sheria. Kwa kusafirisha Tafrodol hadi Ghana, Aveo anavunja sheria za India.

Majibu ya wahusika

D
Maelezo ya picha, Serikali ya Nigeria huhifadhi dawa haramu ambazo wamezikamata katika ghala huko Lagos - nyingi zikiwa ni za kulevya

Tumewasilisha maswali kwa Vinod Sharma na Aveo Pharmaceuticals, lakini hawakujibu.

Idara ya udhibiti wa dawa ya India, CDSCO, imetuambia serikali ya India inatambua wajibu wake kwa afya ya umma duniani kote na imejitolea kuhakikisha India ina mfumo wa udhibiti wa dawa.

CDSCO imesema inashughulikia suala hilo na nchi nyingine, zikiwemo zile za Afrika Magharibi, na imejitolea kufanya kazi nao ili kuzuia hilo. CDSCO imesema itachukua hatua za haraka dhidi ya kampuni yoyote ya dawa inayohusika na utovu wa nidhamu.

Aveo sio kampuni pekee ya India inayotengeneza na kuuza nje dawa zisizo na leseni. Taarifa zinaonyesha kampuni zingine za dawa hutengeneza dawa kama hizo, zenye chapa tofauti na zinapatikana kote Afrika Magharibi.

Akizungumzia kuhusu mkutano wake na Sharma, shushushu wa BBC, ambaye utambulisho wake unafichwa kwa usalama wake, anasema: "Waandishi wa habari wa Nigeria wamekuwa wakiripoti kuhusu tatizo hili kwa zaidi ya miaka 20."

Huko Tamale, Ghana, timu ya BBC ilifuata kikosi kazi cha wenyeji kwenye uvamizi wa mwisho kwa siku hiyo ambapo walipata tafrodol zaidi za kampuni ya Aveo. Jioni hiyo walikusanyika katika bustani ya eneo hilo ili kuchoma dawa walizokamata.