Wanandoa wanaoomba moyo wa mtoto wao kuacha kupiga

Andrea na Jay

Chanzo cha picha, Jay Weeldreyer

Maelezo ya picha, Andrea na mpenzi wake Jay wakiwa katika likizo Malta

Andrea na Jay hawakuwahi kufikiria wangekuwa katika hali kama hii: wakiomba kwamba moyo wa binti yao uwache kupiga kabla Andrea hajapata maambukizi mabaya.

Wanandoa hao wa Marekani walikuwa likizoni huko Malta wakati Andrea Prudente, mwenye ujauzito wa wiki 16, alipoanza kuvuja damu. Madaktari walimwambia kuwa kondo lake la nyuma lilikuwa limejitenga kwa kiasi na mimba yake haikuwa na uwezo tena wa kuishi.

Lakini moyo wa mtoto ulikuwa bado unapiga, na huko Malta hii ina maana kwamba, kwa sheria, madaktari hawawezi kuangamiza ujauzito.

Kwa wiki, wanandoa walisubiri, wakiwa wamejifungia katika chumba kimoja cha hospitali.

"Tumeketi hapa tukifikiria kwamba iwapo leba itaanza, hospitali itaingilia. Ikiwa moyo wa mtoto utasimama, watatusaidia kwa hilo. Lakini zaidi ya hayo, hawatafanya chochote," Jay Weeldreyer ananiambia kwa simu.

Sauti yake imechoka na ina hasira. Ana wasiwasi kwamba hali ya Andrea inaweza kubadilika haraka na wakati wowote.

Andrea na Jay

Chanzo cha picha, Jay Weel Dreyer

Andrea na Jay wanatumai kuwa wataweza kusafiri hadi Uingereza, ambapo utaratibu wa matibabu unaruhusiwa.

"Kwa kuvuja damu na kutenganishwa kwa kitovu na kizazi , huku ukiwa utando umepasuka kabisa na kitovu cha mtoto kionekana kutoka nje ya kizazi chake, Andrea yuko katika hatari kubwa ya maambukizi licha ya kwamba kila kitu kinaweza kuzuiwa," anasema.

"Mtoto hawezi kuishi, hakuna kinachoweza kufanywa kubadili hilo. Tulimpenda, bado tunampenda, tunatamani angeishi, lakini hawezi. Na hatuko tu katika wakati ambapo tunapoteza binti tuliyempenda, lakini hospitali inaongeza muda wa Andrea kuwa hatarini," anaongeza.

Matumaini yake pekee ni kuhamishwa kwa dharura kwenda Uingereza kulipiwa na bima yake ya usafiri.

Mnamo 2017, mtalii mwingine alilazimika kuhamishwa hadi Ufaransa ili kutoa mimba kwa dharura. Lakini hii sio chaguo mbadala kwa wanawake huko Malta.

Uavyaji mimba ni haramu Malta

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kisiwa hicho kina mojawapo ya sheria kali zaidi barani Ulaya linapokuja suala la utoaji mimba: kuangamiza mimba ni kinyume cha sheria kabisa, hata wakati kijusi hakina nafasi ya kuishi, kama ilivyo hapa.

Dk Lara Dimitrijevic, mwanasheria nchini Malta na rais wa Wakfu wa Haki za Wanawake, amekuwa akipigania sheria hii kwa miaka mingi.

"Hapa, wanawake mara chache huongea," ananiambia.

"Tabia ya jumla ni kwamba madaktari wanaruhusu mwili kukiondoa kijusi peke yake, au ikiwa mgonjwa atakuwa mgonjwa sana na kupata maambukizi yanayohatarisha maisha ya mama , wataingilia kati kuokoa maisha yake."

"Tunajua kwamba kwa wastani kuna kesi mbili au tatu kama hizi kila mwaka, lakini baada ya Andrea kuweka hadithi yake hadharani kupitia mitandao ya kijamii, tulianza kuona wanawake wengi zaidi wakijitokeza na kusema wanachopitia."

Dimitrijevic anasema sheria lazima ibadilike, kwa sababu tabia kama hiyo haiwakilishi tu hatari ya kiafya kwa wanawake, lakini pia kiwewe cha kisaikolojia kwao na familia zao.

BBC iliuliza serikali ya Malta na usimamizi wa hospitali kwa majibu, lakini haikupata jibu.

Jay ananiambia kwamba yeye na mke wake wamechoka baada ya kusubiri kwa siku sita kwa moja ya mambo mawili ya kutisha kutokea.

"Utaratibu huu uliweza kufanyika kwa saa mbili, bila kumweka Andrea katika hatari, na kuturuhusu kuhuzunika," anasema.

"Badala yake, hali hii imeendelea mbele ambapo unaishia na mawazo mabaya sana, ukijiuliza haya yataishia vipi."