Kuna nini ndani ya mkahawa wa miaka 5,000 uliogunduliwa hivi karibuni nchini Iraq?

Chanzo cha picha, Lagash Archeological project
Mita moja na nusu chini ya ardhi, wanaakiolojia wamepata mabaki ya mgahawa wa zama za kale ambao unaaminika kuwa wa 2,700BC.
Mkahawa huo ulipatikana katika jiji la kale la Lagash, katika nchini ya Iraq.
"Ulijumuisha eneo kubwa la kawaida ambalo pengine lilikuwa mahali ambapo chakula kililiwa," Sara Pizzimenti kutoka Chuo Kikuu cha Pisa aliiambia BBC.
Yeye ni mmoja wa watafiti ambao wamekuwa wakilichunguza jiji la zamani kwa miaka mitano sasa kama sehemu ya Mradi wa Akiolojia ya Lagash.
Lagash ilikuwa mojawapo ya miji mikubwa na kongwe zaidi kusini mwa Mesopotamia na mojawapo ya vituo vya mijini vya mapema zaidi duniani.
Ilikuwa sehemu ya ustaarabu wa Sumeri, mkusanyiko wa majimbo ya miji karibu na mito ya Tigris na Euphrates, ambayo ilidumu kutoka kipindi cha zama za Neolithic hadi Enzi ya shaba ya kale.
Madawati, oveni na jokovu la miaka 5,000

Chanzo cha picha, Lagash archeological project
Kwa kutumia mbinu mpya, kama vile picha za ndege zisizo na rubani na uchanganuzi wa sumaku, njia ambayo inaruhusu wanaakiolojia "kuona" ardhini bila kuchimba, timu iliweza kuchimba kwa usahihi zaidi.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mkahawa huo ulipoonekana , walifukua madawati, aina ya jokofu la udongo, tanuri, na mabaki ya vyombo vya kuhifadhia chakula, vingi vikiwa bado na chakula.
"Shukrani kwa ufinyanzi wa aina fulani uliopatikana kwenye tovuti na sanaa ya nakshi au michoro kwenye vito vya thamani), hakuna shaka mkahawa huo uliokuwa na umri wa takriban miaka 5,000," Holly Pittman, mkurugenzi wa mradi, aliiambia BBC.
Lakini kifaa cha kupozea kilifanyaje kazi bila umeme?
Kipoezaji cha chungu cha udongo au jokofu la chungu kilikuwa na sufuria mbili.
Chungu cha nje, kilicho na mchanga ulio majimaji , kilikuwa na sufuria ya ndani, ambayo ilikuwa imewekwa kuzuia maji kuingia ndani na hapo ndipasa chakula kiliwekwa. Mvuke wa unyevu wa chungu cha nje uliondoa joto katikia chungu cha ndani .Chochote kinaweza kupozwa kwenye sufuria hizi.
Ukiwa kwenye mto Tigri kaskazini mwa mahali mto huo unapokutana na Euphrates, Lagash ilikuwa kitovu cha biashara chenye shughuli nyingi wakati wa Enzi ya Utawala wa kale, ambao ulidumu kutoka 3,200 hadi 2,900 KK, wakati baadhi ya miji ya kwanza duniani ilianzishwa.
"Tunajaribu kuelewa jinsi jiji hili lilivyokua kutoka eneo dogo ambalo lilikuwa na sifa ya eneo hilo katika nyakati za zamani hadi mtandao mkubwa zaidi na uliounganishwa zaidi," mwanaakiolojia Reed Goodman kutoka Chuo Kikuu cha Pennsylvania aliiambia BBC.
Mabaki ya miaka 5000

Chanzo cha picha, Lagash archeoligical project
Karibu na tanuri na jokofu la udongo,wanaakiolojia walipata chumba kingine na bakuli za chakula, glasi na mitungi.
Na hazikuwa tupu.
"Tulikuta mabakuli zaidi ya 100 yakiwa na mabaki ya chakula, jambo ambalo lilitufanya tuamini kuwa hapa ni mahali pa watu wa wakati huo kupita na kupata chakula au kinywaji," Pizzimenti alisema.
Mahali hapo hapangeweza kuwa jiko la nyumbani, alisema "kwa sababu ya kiasi kikubwa cha chakula kilichoandaliwa".
Mabaki ya chakula yanaonyesha watu ambao walitembelea mkahawa miaka 5,000 iliyopita walikula samaki.
"Ndani ya kila kontena hizi tulipata idadi kubwa ya mifupa ya samaki, iliyohifadhiwa vizuri," Pittman alisema.
Kinachowashangaza wanaakiolojia ni kwa nini chakula hakikuliwa.
"Vitu vyote tulivyopata viliachwa tu hapo, kwa hivyo kuna kitu pengine kilitokea, lakini hatujui ni nini na hilo ni jambo tunalotaka kugundua," Pizzimenti alisema.
Kipande cha fumbo kinachokosekana

Chanzo cha picha, lagash archeological project
Pia wanataka kujua wageni wa mkahawa huo walikuwa akina nani na hali yao ya kijamii ilikuwaje.
Uchimbaji wa hapo awali kwenye tovuti ulifunua kuwa jiji la Lagash lilikuwa nyumbani kwa majengo matatu ya mahekalu, ambapo watu wa tabaka la juu waliishi.
Lakini wanaakiolojia wanafikiri mikahawa hiyo hiyo haikuwa katika sehemu ya kifahari ya jiji.
"Mtaa ambao mikahawa hiyo hiyo ilipatikana haionekani kuwa katika eneo la wasomi. Inaonekana ni sehemu ambayo ilikuwa ikitembelewa na watu wa kawaida," Pizzimenti alisema.
Wanaamini kuwa mikahawa hiyo ilikuwa mahali ambapo watu waliokuwa wakifanya kazi mbali na nyumbani wangeweza kula milo yao ya kila siku.
"Tunachohitaji kugundua ni ikiwa watu hawa walikuwa wakifanya kazi katika utengenezaji wa kauri," Pittman alisema.
Timu ina hamu ya kujua zaidi kuhusu maisha ya watu wa kawaida huko Lagash.
"Tunatumai kutoa uwiano mzuri kwa masimulizi ya aina hii ambayo yamekuwa yakisimama kwa muda mrefu katika maeneo haya ya awali kama nafasi za matajiri na maskini tu, kukiwa na tofauti ndogo sana kati yao," Goodman alisema.












