Putin apendekeza sheria mpya za kutumia silaha za nyuklia

m

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rais wa Urusi aliwahi kutishia kutumia silaha za nyuklia lakini pendekezo lake jipya linapanua tishio hilo
    • Author, Frances Mao
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Vladimir Putin anasema Urusi itachukulia shambulio kutoka katika taifa lisilo na silaha za nyuklia ambalo linaungwa mkono na taifa lenye silaha za nyuklia kuwa "shambulio la pamoja," kauli inayoweza kuzingatiwa kuwa ni tishio la kutumia silaha za nyuklia katika vita vya Ukraine.

Katika hotuba yake ya Jumatano usiku, rais wa Urusi alisema serikali yake inafikiria kubadilisha sheria na masharti ambayo Urusi itayatumia ili kutumia zana zake za nyuklia.

Ukraine ni taifa lisilo na silaha za nyuklia ambalo linapata usaidizi wa kijeshi kutoka Marekani na nchi nyingine zenye silaha za nyuklia.

Kauli yake inakuja wakati Kyiv inatafuta idhini ya kutumia makombora ya masafa marefu ya nchi za Magharibi dhidi ya maeneo ya kijeshi ndani ya Urusi.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesafiri kwenda Marekani wiki hii na anatazamiwa kukutana na Rais wa Marekani, Joe Biden mjini Washington siku ya Alhamisi, ambapo ombi hilo la Kyiv linatarajiwa kuwa ajenda kuu.

Ukraine imeingia katika ardhi ya Urusi mwaka huu na inataka kushambulia ngome ndani ya Urusi, ambazo ndizo zinatumika kurusha makombora nchini Ukraine, amesema.

Akijibu matamshi ya Putin, Mnadhimu Mkuu wa Zelensky, Andriy Yermak anasema Urusi "haina kitu kingine zaidi ya hadaa ya nyuklia ili kutisha Ulimwengu."

Vitisho vya Nyuklia

Putin aliwahi kutishia kutumia silaha za nyuklia huko nyuma. Ukraine inasema ni vitisho vya nyuklia ili kuzuia washirika wake kutoa msaada zaidi.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mshirika wa Urusi, China imetoa wito wa utulivu, huku kukiwa na ripoti kuwa Rais Xi Jinping amemuonya Putin dhidi ya kutumia silaha za nyuklia.

Lakini siku ya Jumatano, baada ya mkutano na Baraza lake la Usalama, Putin alitangaza kuongezwa kwa kanuni kali.

Kanuni mapya za nyuklia "zitaweka wazi masharti kwa Urusi ya kutumia silaha za nyuklia," alionya - na kusema masharti hayo yatajumuisha mashambulio ya kawaida ya makombora dhidi ya Moscow.

Alisema Urusi itazingatia "uwezekano" wa kutumia silaha za nyuklia ikiwa itagundua kuanza kwa urushwaji mkubwa wa makombora, ndege na droni katika ardhi yake, ambao utaleta "tishio kubwa" kwa uhuru wa nchi.

Aliongeza: "Kanuni inapendekeza kuwa uvamizi dhidi ya Urusi na nchi yoyote isiyo ya nyuklia, lakini kwa ushiriki au msaada wa nchi yenye nyuklia, litahesabiwa kuwa ni shambulio lao la pamoja dhidi ya Shirikisho la Urusi."

Silaha za nyuklia za nchi hiyo ni "dhamana muhimu zaidi ya usalama wa serikali yetu na raia wake," alisema kiongozi huyo wa Kremlin.

Tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, mataifa yenye silaha za nyuklia yamejiwekea sera za kujizuia kutumia silaha za nyuklia, kwa wazo kwamba ikiwa mataifa yanayopigana yataanzisha mashambulizi makubwa ya nyuklia - yatasababisha uharibifu mkubwa.

Lakini kuna silaha za kimkakati za nyuklia ambazo ni vichwa vidogo vilivyoundwa ili kuharibu shabaha bila kueneza mionzi.

Mwezi Juni, Putin alitoa onyo kwa nchi za Ulaya zinazoiunga mkono Ukraine, akisema Urusi ina "silaha nyingi za kimkakati za nyuklia kuliko zilizoko katika bara la Ulaya, hata kama Marekani italeta zake."

"Ulaya haina mfumo wa onyo la mapema," aliongeza. "Kwa maana hii wana ulinzi mdogo."

Wakati huo alikuwa amedokeza kuhusu mabadiliko ya kanuni za nyuklia za Urusi - hati ambayo inaweka masharti ambayo Moscow itayafuata ili kutumia silaha za nyuklia.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah