Kuku wa 'kupandikizwa' wanaweza kukomesha uuaji wa mabilioni ya vifaranga

Watafiti wa Israel wanasema wametengeneza kuku waliobadilishwa vinasaba ambao hutaga mayai ambayo ni vifaranga wa kike pekee huanguliwa.

Hatua hiyo inaweza kuzuia uchinjaji wa mabilioni ya kuku majogoo kila mwaka, ambao huchinjwa kwa sababu hawatagi mayai.

Vifaranga wa kike, na mayai wanayotaga yanapokomaa, hayana alama yoyote ya mabadiliko ya awali ya jeni. Kikundi cha ustawi wa wanyama, Compassion in World Farming, kimeunga mkono utafiti huo.

Dk Yuval Cinnamon kutoka taasisi ya Volcani karibu na Tel Aviv, ambaye ni mwanasayansi mkuu wa mradi huo, aliambia BBC kwamba maendeleo ya kile anachokiita ''kuku wa dhahabu'' yatakuwa na athari kubwa chanya kwa ustawi wa wanyama katika sekta ya kuku.

“Nimefurahi sana tumetengeneza mfumo ambao nadhani unaweza kuleta mapinduzi ya kweli katika tasnia, kwanza kwa manufaa ya kuku lakini hata sisi sote, kwa sababu hili ni suala linalomgusa kila mtu hapa duniani,” alisema.

Wanasayansi hao wamehariri vinasaba au DNA katika kuku wa Golda ambayo inaweza kuzuia ukuaji wa viinitete vyovyote vya kiume kwenye mayai wanayotaga.

DNA huwashwa wakati mayai yanapowekwa kwenye mwanga wa bluu kwa saa kadhaa. Viinitete vya vifaranga vya kike haviathiriwi na mwanga wa bluu na hukua kawaida. Vifaranga hawana chembe za kijenetiki za ziada ndani yao wala mayai wanayotaga, kulingana na Dk Cinnamon.

“Wakulima watapata vifaranga sawa na wanavyopata leo na walaji watapata mayai yale yale wanayopata leo,” alisema. "Tofauti ndogo tu katika mchakato wa uzalishaji ni kwamba mayai yatakuwa yanaonekana kwa ndani kukiwa na mwanga wa bluu."

Timu ya Dk Cinnamon haijachapisha utafiti wao kwa sababu inapanga kutoa leseni kwa teknolojia hiyo kupitia kampuni yake ya spin out, Huminn Poultry, kwa hivyo wanasayansi wanaojitegemea kutoka kwa kikundi cha utafiti hawajaweza kutathmini madai hayo.

Lakini timu ya Israel imefanya kazi kwa kushirikiana na shirika la ustawi wa wanyama lenye makao yake nchini Uingereza Compassion in World Farming (CIWF) ambalo wafanyakazi wake wametembelea kampuni hiyo na kufuatilia utafiti kwa miaka mitatu.

Mshauri wake mkuu wa sera Peter Stephenson alisema kuwa mafanikio hayo yanaweza kuwa "maendeleo muhimu sana" kwa ustawi wa wanyama. "Kwa kawaida ninahofia sana kutumia uhariri wa vinasaba vya wanyama wa kienyeji. Lakini hii ni suala la kipekee na mimi, na wenzangu kutoka CIWF tunaunga mkono," alisema.

''Hatua muhimu inayofuata ni kuona kama kuku na vifaranga wa kike wanaowazalisha, ambao watataga mayai kwa ajili ya matumizi ya binadamu, wanaweza kupitia maisha ya kibiashara bila masuala yoyote ya ustawi yasiyotarajiwa kutokea.''

Sheria kwa sasa inapitishwa katika Bunge la Uingereza ambayo itaruhusu uhariri mdogo wa jeni kwa kilimo cha kibiashara nchini Uingereza. Inafikiriwa pindi mswada huo utakapopitishwa mapema mwaka ujao, kwamba kanuni zingepunguzwa hatua kwa hatua, na kuruhusu teknolojia hiyo kutumika kwa mimea tu kwa kuanzia.

Uhariri wa jeni (GE) unachukuliwa na serikali kuwa unaokubalika zaidi hadharani kuliko mbinu ya zamani ya urekebishaji jeni (GM). GE kwa kawaida huhusisha kudhibiti jeni kwa kuondoa DNA , ambapo GM kwa kawaida huongeza DNA, wakati mwingine kutoka kwa spishi nyingine.

CIWF inakadiria kuwa karibu vifaranga wa kiume bilioni saba huuliwa (huchinjwa) na sekta ya kuzalisha mayai kila mwaka muda mfupi baada ya kuzaliwa kwa sababu hawana thamani ya kibiashara.

Serikali ya Ujerumani ilipiga marufuku mauaji ya halaiki ya vifaranga wa kiume mwanzoni mwa mwaka huu. Na Wafaransa wana mapendekezo sawa ya kuanza mwanzoni mwa mwaka ujao.

Mataifa mengine mengi ya Umoja wa Ulaya yameelezea wasiwasi wao kuhusu kitendo hicho na mengi yametaka kuwepo kwa sheria ya Umoja wa Ulaya nzima. Serikali ya Uingereza bado haijatoa maoni yoyote kuhusu msimamo wake kuhusu kitendo hicho.

Dk Enbal Ben-Tal Cohen, ambaye aliongoza utafiti huo, aliambia BBC kwamba mfumo huo uko katika hatua ya juu ya maendeleo na timu inashirikiana na wafugaji ili kuboresha mchakato huo.

"Kwa miaka mingi ya tafiti, kulikuwa na changamoto nyingi ngumu ambazo tulifanikiwa kuzishinda, na hatimaye sasa tunapokuwa na suluhisho linalowezekana, ninatumai kuwa tasnia itaipitisha hivi karibuni," alisema.