Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsia 'haipaswi kuwa kizuizi' katika kuwafundisha wanaume soka
- Author, Kelvin Kimathi
- Nafasi, BBC Sport Africa
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Jackline Juma anaweka historia kama mwanamke wa kwanza kufundisha timu ya wanaume katika ligi kuu ya Kenya - lakini bado anatakiwa kukabiliana na ubaguzi wa kijinsia pembezoni mwa uwanja .
Akiiongoza FC Talanta katika msimu mpya wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), haikumchukua Juma muda mrefu kutambua kwamba si kila mtu aliona uteuzi wake kuwa mzuri.
"Kuna baadhi ya maneno yalisemwa kutoka kwa benchi nyingine kama 'Hatuchezi soka ya wanawake'," Juma aliambia BBC Sport Africa, akizungumzia mchezo wake wa pili akiwa kocha mkuu dhidi ya Sofapaka.
"Na nikajiambia 'Ah, sawa. Lakini acha dakika 90 ziamue'."
Kikosi cha Juma kiliibuka na ushindi wa i 1-0 ili kuwanyamazisha wakosoaji wake.
"Baada ya mechi, bila shaka, hatukupeana mikono," alisema.
"Kupata pointi tatu dhidi ya kocha mwenye uzoefu kulinipa motisha ambayo ninahitaji kuendelea."
Afisa wa Sofapaka hakujibu ombi la maoni yake kuhusu tukio hilo.
Juma- Mama wa watoto wawili mwenye umri wa miaka 38, alianza kufundisha soka zaidi ya miongo miwili iliyopita na sasa ana leseni A ya Shirikisho la Soka la Afrika - hadhi ya pili ya juu zaidi barani humo.
Anamtaja mkufunzi wa Real Madrid Carlo Ancelotti na kocha wa Arsenal Mikel Arteta kama wanaompa nguvu na kielelezo dimbani, na analenga kutekeleza mtindo wa kumiliki mpira.
Ingawa amekuwa mwanzilishi kwa wanawake wengine kufuata, mwanzoni hakuchukulia kuteuliwa kwake mnamo Agosti kupitia msingi wa jinsia.
"Kwangu, nilidhani ni kawaida," alisema.
"Haikuwa hadi walipozungumza juu ya kuwa historia ndipo niligundua kuwa hii ni kubwa.
"Jinsia isiwe kikwazo. Nilijiambia wataamua uwezo wangu kulingana na kile nitakachotoa, sio kwa sababu mimi ni kocha wa kike."
Kupata imani ya wachezaji
Juma alianza safari yake ya kufundisha soka akiwa na umri wa miaka 16 na, baada ya kufanya kazi katika kozi kadhaa, pia anafanya kazi kama mkufunzi mkuu wa makocha.
Alipata uzoefu mkubwa na vilabu kadhaa vya wanawake na timu ya Kenya ya wachezaji walio na umri wa chini ya miaka 20 kabla ya simu kutoka kwa Talanta yenye makao yake Nairobi kuja.
Kazi yake ya kwanza ilikuwa kuishawishi familia yake, ambayo ilikuwa na shaka kuhusu yeye kuchukua kazi hiyo na kuhoji ikiwa angeweza kukabiliana na shinikizo hilo.
"Pia walikuwa na wasiwasi kuhusu wakosoaji lakini niliwaambia 'Hakuna jambo gumu. Hebu tujaribu'," alieleza.
Kisha kikaja kikosi cha Talanta chenyewe.
“Kuna mchezaji alinitumia ujumbe ‘Kocha nichukue nafasi hii kukupongeza na kukukaribisha katika timu kabla hata hujaja.
"Hii ilinipa mwanzo mzuri'
Nahodha Augustine Kuta anakiri uteuzi wa Juma ulikuwa "mshtuko" kwa wengi katika kikosi, lakini alifaulu kuwateka nyoyo haraka uwanjani.
"Baada ya kikao chake cha kwanza, jinsi alivyoshughulikia, tulihisi kwamba alikuwa amehitimu sana kwa kazi hiyo," Kuta aliambia BBC Sport Africa.
"[Kulikuwa na] mazoezi mapya ambayo wachezaji wengi hawakutarajia kutoka kwa kocha wa kike. Baada ya kikao cha kwanza kila mmoja alikuwa tayari kufanya kazi na kumsaidia kufikia malengo yake."
Hata hivyo, Kuta anasema wachezaji waliompinga wametilia shaka uwezo wa Juma.
"Wengi yamkini wanasema 'Je, mtaweza kucheza ligi mkiwa na kocha wa kike? Ligi ya Premia ni ngumu. Inahitaji kocha mwenye uzoefu'," kiungo huyo mwenye umri wa miaka 32 alieleza.
"Lakini hiyo ndiyo inatusukuma - kujaribu kuwaonesha kwamba inawezekana'
"Hawapaswi kumdunisha kwa sababu ni kocha wa kike. Tumeona anachoweza kufanya."
Kuonyesha ustahimilivu
Safari ya Juma hadi KPL haijawa moja kwa moja.
Alikabiliwa na pingamizi kutoka kwa familia yake alipoanza kucheza soka akiwa na umri wa miaka tisa, kwani waliona mchezo huo kama "mchezo wa mvulana".
"Niliendelea, bila kujali ilikuwa vigumu kiasi gani, hadi hatimaye wakaanza kuniunga mkono," alisema.
Alikuwa amepata nafasi kwenye timu ya taifa kabla ya kulazimika kuacha kucheza na kujikita katika ukocha mwaka wa 2016.
Talanta ilimaliza katika nafasi ya 15 katika ligi kuu ya timu 18 msimu uliopita na makocha kadhaa wa kiume waliokuwa na sifa zinazofanana walionyesha nia ya kuchukua usukani.
Lakini makamu mwenyekiti James Theuri alisema klabu ilikuwa tayari kwenda upande mwingine.
"Tulitaka kocha sio tu kwa matokeo ya haraka lakini ambaye anaweza kukua na wachezaji wetu," aliambia BBC Sport Africa.
"Jackline amethibitisha kuwa anaweza kuwa mshauri mzuri na ana mvuto wa kuwanoa wachezaji wachanga.
"Haukuwa uamuzi rahisi, lakini Jackline alikuwa amefuzu na tulitaka kuwapa changamoto wavulana."
Kupigania haki za kijinsia
Uteuzi wa Juma pia umempa jukwaa kubwa zaidi la kutaka kuwepo kwa usawa kati ya jinsia na malipo sawa.
"Ni soka. Sio kama tunacheza dakika 60 na wao (wanaume) wanacheza dakika 90," alisema.
"Tunaweka juhudi nyingi. Motisha inapaswa kuwa sawa kwa wanaume na wanawake."
Katika hali inayoonyesha kuwa mambo yanabadilika, Juma sio kocha mkuu pekee wa kike aliyeongoza timu kubwa Afrika Mashariki msimu huu.
Mnamo Oktoba, Oliver Mbekeka alipewa jukumu la kuinoa Lugazi ya Ligi Kuu ya Uganda kwa muda, na kushinda mchezo wake pekee wa bao 1-0 dhidi ya Giants kabla ya kurejea kwenye nafasi yake ya kawaida kama kocha msaidizi.
Lakini Juma anasema kuwa ni wazi kwamba huu ni mwanzo tu wa kile kinachohitajika kuwa harakati pana zaidi, baada ya kushuhudia uonevu wa kijinsia wakati wa kupanda kwake kupitia mchezo.
"Hili lilikuwa moja ya mambo ya kuudhi sana kwangu katika kazi yangu - wachezaji wa kike [kutendewa visivyo] kwa kutoheshimiwa sana ikilinganishwa na wanaume."
Kuhusu matamanio yake uwanjani, Juma analenga kuiongoza Talanta kumaliza katika nafasi sita bora katika KPL msimu huu.
Kwa sasa wako katika nafasi ya 15, wakiwa na sare mbili na kushindwa mara mbili sambamba na ushindi wao dhidi ya Sofapaka, wapo nyuma kwa pointi nne na Tusker walio katika nafasi ya sita wakiwa na michezo miwili ya ziada.
Chochote msimu utakacholeta, Juma anatumai simulizi yake itawatia moyo wanawake na wasichana ambao wana ndoto ya kuwa na taaluma ya soka.
"Nataka kuwatia moyo na kuwaonyesha kuwa inawezekana sana," alisema.
"Wanachohitaji kwanza ni kujiamini, kupata maarifa yanayohitajika, na kila fursa wanayopata wanapaswa kuitumia vyema."
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah