Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kuminywa kwa mtandao wa intaneti kunavyoathiri sekta tofauti Tanzania
Mitandao ya kijamii — Facebook, X (zamani Twitter), YouTube, WhatsApp, TikTok na Instagram — haipatikani kabisa. Wale wanaoendelea kuunganishwa wanalazimika kutumia VPN.
Hadi sasa muunganisho wa intaneti unaendelea kuminywa nchini Tanzania tangu uchaguzi mkuu wa tarehe 29 mwezi Oktoba mwaka huu.
Athari zake hazijaishia katika kutopata taarifa sahihi kuhusu hali ya kiusalama zimeathiri sekta nyingi ikiwemo upatikanaji wa bidhaa za kimsingi na hata biashara.
Kwa mujibu wa serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania uminyaji wa intaneti ni kuhakikisha kuwa inazuia wahalifu mtandaoni ambao kulingana na serikali hiyo walitumia mitandao kueneza habari za uchochezi na kusababaisha maandamano ya viurugu ambazo zimekuwa zikishuhudiwa nchini humo.
''Wakati tulipowasha mtandao wa intaneti ilileta shida kwa watu wachache wahuni ambao walikuwa wakitumia mtandao kuleta vurugu. Sasa kwa mujibu wa sheria za mamlaka ya kusimamia mawasiliano Tanzania kuna sheria ambazo zinatumiwa wakati kuna wasiwasi wa usalama wa kitaifa kuhusu mtandao wa intaneti ndani ya nchi,'' Thabit Kombo alipoulizwa na BBC hatua ya kuminya intaneti.
Pia ni moja wapo ya kichocheo cha maandamano ya sasa nchini Tanzania vijana waliozungumza na BBC walisema kufungiwa intaneti kunahujumu haki zao na baadhi wao wakitaka serikali itengeze mazingira mazuri ya uhuru wa kujieleza.
Lakini serikali ya Tanzania haijachukulia hatua hiyo kama vile vijana wa Tanzania wanavyoiona.
''Kuminya intaneti si mambo ya haki au ukosefu wa haki, tunazungumzia maisha ya watu, mali ya watu na usalama wa nchi yetu'' aliongezea waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Thabit Kombo.
Wataalamu wa usalama wa kidijitali wanatahadharisha kwamba kufungwa kwa mitandao kunazidisha uwezekano wa upotoshaji wa habari.
Mtaalamu George Musalama ameiambia BBC: "kukosekana kwa intaneti kunazidisha taharuki na kutoa nafasi kwa propaganda kuenea bila uthibitisho wowote."
Kuzima au kuminya intaneti kumedhihirisha ni kwa kiasi gani Tanzania sasa inategemea mtandao.
Kile kilichokuwa badiliko la kisiasa la kudhibiti habari kimekuwa kichochezi cha kiuchumi - ambacho kinaweza kuzima mara moja pesa za simu, benki, vifaa, huduma za afya na maisha ya kila siku katika mojawapo ya uchumi wa kidijitali unaokuwa kwa kasi zaidi Afrika Mashariki.
Huduma za benki na miamala za simu
Takriban siku tano, Watanzania walikatiwa huduma za mtandao, na hivyo kuwafanya maelfu ya watu kushindwa kupokea fedha kutoka kwa ndugu zao nje ya nchi.
Huduma za benki na miamala ya simu ziliripotiwa kukwama.
Mamilioni ya shilingi yamekwama kwa sababu malipo hayawezi kuthibitishwa.
Benjamin Fernandes, mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Nala, alisema kufungwa kwa jukwaa la Nala kuna madhara makubwa kwa mamilioni ya Watanzania wanaotegemea jukwaa hilo.
"Kwa saa 18, familia nchini Tanzania hazikuweza kupokea pesa kutoka kwa wapendwa wao ng'ambo. Kwa nini? Kuzimwa kwa mtandao," Fernandes aliandika kwenye X. "Hii haihusu teknolojia - inahusu chakula, dawa, na maisha."
Kupitia mtandao wake wa X Fernandes alisema alipokea simu kutoka kwa watu nje ya nchi wakijaribu kutuma pesa za bili za hospitali, lakini hawakuweza kwa sababu ya kukatika.
Wazazi vijijini wanaotegemea fedha kutoka mijini pia wameripoti hawawezi kupokea wala kutuma pesa.
Pia wafanyabiashara wadogo, wauzaji wa mtandaoni, na vijana wanaofanya kazi za kidigitali kama washawishi au wauzaji wa bidhaa wamepoteza kipato.
Licha ya msemaji wa serikali kuwataka wafanyakazi wa umma kuendelea kufanya kazi wakiwa majumbani, vijana walioamua kufuata maagizo hayo hawangeweza kufanya kazi nyumbani kutokana na intaneti kufungwa.
Paul Boniface kupitia mtandao wa kijamii amekasirishwa na kuminywa kwa intaneti nchini humo kufuatia ghasia akisema amepata hasara kubwa.
"Natumia VPN kwa sababu internet tumezimiwa na hili swala linaathiri sana mfumo mzima wa ukiutendaji kwa sasa tunaotegemea internett kwenye kazi zetu za Kila siku lakini kazi zimesimama kwa sababu ya ukosefu wa internet iliyo imara" alieleza.
Biashara za nje na ndani zimetatizika
Kuminywa kwa intaneti pia kumesababisha kusitishwa kwa shughuli zote za kibiashara katika mji wa mpaka wenye shughuli nyingi.
Namanga, kitovu muhimu cha biashara kati ya nchi mbili za Afrika Mashariki Tanzania na Kenya iliona ofisi zake za forodha na njia za usafirishaji zikiwa zimefungwa huku machafuko yakienea.
Shughuli za forodha zilisitishwa baada ya Serikali ya Tanzania kutekeleza kuzimwa kwa mtandao wa intaneti, jambo lililosababisha usumbufu mkubwa wa mawasiliano na kusimamisha usindikaji wa vibali vya kuuza nje na kuingiza bidhaa.
Madereva wa malori wa usafirishaji wa umbali mrefu na wafanyabiashara wameripoti hasara zinazofikia mamilioni ya shilingi baada ya kushindwa kuhamisha bidhaa kuvuka mpaka.
"Tumezuiliwa hapa siku nzima; hatuwezi kupata kibali cha kusafirisha kwa sababu mfumo umezimwa. Parachichi zetu zinakoromoka, hakuna atakayenunua," alisema dereva mmoja upande wa Kenya.
Kwa mujibu wa Seatrade Maritime, Alhamisi ya wiki jana shughuli katika Bandari ya Dar es Salaam lango kuu la biashara ya ukanda wa Afrika Mashariki zilisimama.
Mizigo ya chakula, mafuta, na bidhaa za viwandani ilikwama njiani kuelekea DRC, Zambia, Malawi, Rwanda, Burundi na Uganda.
Mipaka ya Kasumulu, Namanga na Tunduma imeripoti kusitisha shughuli kwa muda baada ya mifumo ya mawasiliano kushindwa kufanya kazi.
Ukosefu wa mafuta na usafiri unakwamisha usafirishaji wa bidhaa muhimu kama chakula.
Hali ya maisha kwa raia wengi wa Tanzania imezorota.
Kwa sasa mafuta yamepanda bei mara nne kwenye soko la magendo, vituo vya mafuta vimefungwa, na usafiri wa umma umesimama.
Sekta ya utalii, injini kuu ya mapato ya taifa sasa inadorora.
Kuzimwa kwa intaneti, ambayo ilisababisha muunganisho kushuka hadi chini ya asilimia 15% ya viwango vya kawaida, ilianza siku ya uchaguzi, Jumatano, Oktoba 29 hii ni kwa mujibu wa shirika la Netblocks.
Hali hiyo iliathiri safari za ndege ambazo hutegemea zaidi intaneti.
Kutokana na hilo tahadhari ya ubalozi wa Marekani na Uingereza zimeeleza kwamba ndege kadhaa za kimataifa zilishindwa kutua au kuruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere wiki jana kutokana na hitilafu za mawasiliano.
Tanzania bara na visiwani Zanzibar ina vivutio vya utalii na watalii wengi wa ndani na nje walilazimika kusubiri kwa muda mrefu katika uwanja wa ndege wa Zanzibar kutokana na hitilafu hizo.
Usumbufu huu kwa watalii kulingana na wataalam wa uchumi unasema huenda ukachora picha hasi kwa mazingira ya utalii na kuathiri sekta hiyo ambayo inajumuisha asilimia 18 ya mapato ya GDP nchini humo.
Kuminywa kwa intaneti pia kumezidisha taharuki kiasi ya kuwa ubalozi wa Marekani ulishauri raia wake kutosafiri Tanzania isipokuwa ni dharura.
Hilo huenda likaathiri idadi ya watalii wanaoingia nchini humo kwani mtazamo wa kimataifa wa Tanzania kama mahali salama umepungua.
Si uchumi pekee hasara ya kuzimwa intaneti imevuruga misingi ya familia hasa jamii.
Familia nyingi zimekatiza mawasiliano, zikibaki kwenye hofu na upweke.
Kwa wengi, ukimya huu wa kidigitali ni kama kifungo kisicho na minyororo kinacholea hofu, hasira, na kukata tamaa