Yanga yamaliza utata, yaitungua Simba 2-0 na kutwaa ubingwa Tanzania

Chanzo cha picha, yanga
- Author, Yusuph Mazimu
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Muda wa kusoma: Dakika 2
Utata na sintofahamu vimehitimishwa rasmi leo. Yanga SC imemaliza msimu kwa kishindo, ikiibuka na ushindi mnono wa mabao 2-0 dhidi ya wapinzani wao wakubwa, Simba SC, katika dabi ya Kariakoo iliyosubiriwa kwa hamu.
Ushindi huu unaifanya Yanga kutawazwa rasmi mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara msimu wa 2024/25, ikifikisha alama 82 na kuiacha Simba ikiwa na alama zake 78. Ni ubingwa wa nne mfululizo.
Mchezo huu wa 184, ambao umekuwa gumzo la msimu kutokana na kuahirishwa mara mbili na kujaa maswali mengi, hatimaye umepigwa na kutoa majibu yote yaliyokuwa yakisubiriwa. Licha ya ukimya na kutokuwepo kwa shamrashamra za kawaida zilizotangulia dabi hii, Yanga wameonyesha ubabe wao uwanjani na kuthibitisha ubingwa wao.
Kabla ya mchezo, ulimwengu wa soka ulitawaliwa na maswali mengi kuhusu hatma ya dabi hii, kutokana na historia yake ya kuahirishwa na malalamiko ya "ukulwa na doto" katika ligi. Hata hivyo, baada ya vikao vya ngazi za juu vilivyojumuisha viongozi wa timu zote mbili na Rais Samia Suluhu Hassan, mambo yalianza kubadilika.
Mabadiliko pia yameshuhudiwa ndani ya Bodi ya Ligi (TPLB), yaliyohusisha kujiuzulu kwa Mwenyekiti wa TPLB, Steven Mnguto, na kusimamishwa kazi kwa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almasi Kasongo.
Mchezo ulivyokuwa
Kipindi cha kwanza cha mchezo kilishuhudia sare tasa ya bila kufungana, huku Yanga wakionekana kushambulia zaidi na kutengeneza nafasi kadhaa. Simba walianza kwa tahadhari, na kuanza kuchangamka zaidi katika kipindi cha pili baada ya kufanya mabadiliko.
Dakika ya 59, Ellie Mpanzu wa Simba alipiga shuti kali lililogonga mwamba, na dakika moja baadaye, Jean Ahoua, mmoja wa waliokuwa wanawania kiatu cha dhahabu, alipiga shuti lililotoka juu ya lango. Hata hivyo, mambo yalibadilika ghafla dakika ya 63, pale mlinda mlango wa Simba, Moussa Camara, alipomchezea vibaya Pacôme Zouzoua ndani ya eneo la hatari. Mwamuzi kutoka Misri, Amin Mohamed Amin Omar, hakusita kuamua penati.
Pacôme Zouzoua mwenyewe alienda kupiga mkwaju huo kwa ujasiri na kuujaza wavuni, akifunga bao lake la 12 katika Ligi Kuu msimu huu na kuiweka Yanga mbele kwa bao 1-0. Baada ya bao hili, Yanga waliongeza kasi ya mashambulizi, wakishambulia kama nyuki.
Dakika ya 71, mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize, alipoteza nafasi ya wazi baada ya kubaki yeye na kipa Camara, akipiga mpira nje ya lango. Dakika ya 76, Pacome aliikosesha Yanga bao la wazi baada ya kupaisha mpira juu akiwa ndani ya eneo la sita, badala ya kutoa pasi kwa wachezaji wenzake wawili waliokuwa katika nafasi nzuri zaidi.
Hata hivyo, Yanga hawakukata tamaa. Katika dakika ya 86, Clement Mzize aliweka kimiani bao la pili la Yanga, akimalizia pasi safi kutoka kwa Pacôme Zouzoua. Bao hili lilihakikisha ushindi wa 2-0 kwa Yanga, na hivyo kuwapa rasmi taji la Ligi Kuu Tanzania Bara.














