Yanga v Simba: Mbivu na mbichi kujulikana leo

- Author, Yusuph Mazimu
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Uwanja wa Benjamin Mkapa leo unafungua milango kwa pambano la mwisho la ligi kuu Tanzania Bara msimu wa 2024/25 (Kariakoo Dabi) ya mzunguko wa pili kati ya Simba na Yanga.
Ni mchezo wa namba 184, mechi iliyohairishwa mara mbili, ikijaa sintofahamu, ukimya na utata, na sasa inaonekana kama mzaha wa soka unaobeba hatima ya bingwa na hata hatma ya soka la Tanzania.
Upekee katika ukimya ni kwamba kwa mara ya kwanza katika historia ya Ligi Kuu Tanzania bara kwa mundo uliopo umepewa waamuzi kutoka mataifa matatu:Mwamuzi wa kati: Amin Mohamed Amin Omar (Misri) Mwamuzi mtathimini: Alli Mohamed (Somalia) na Kamishna wa mchezo: Salim Omary Singano (Tanzania)
Hatua hii huenda imelenga kudhibiti malalamiko ya upendeleo, lakini bado haijaziba utata wa kiusimamizi unaoendelea kuligubika pambano hili.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pamoja pia na utamu wa vita ya kusaka mfungaji bora wa ligi kuu ambapo Jean Ahoua wa Simba (mabao 15), Clement Mzize (Yanga) – mabao 13, Steven Mukwala na Leonel Ateba (Simba) – mabao 13 kila mmoja wanawania kiatu cha dhahabu, bado msisimko wa mchezo huu ni mdogo.
Ni pambano lisilo na mbwembe, tambo wala makeke ya kawaida. Ukipita mitaani, kwenye mitandao ya kijamii au hata kwenye tovuti ya Simba hutaona dalili ya moto wa dabi unaowaka. Ni kama mechi haipo.
Yanga SC wamekuwa wakijibizana na wanahabari, wakijivunia hali yao, lakini Simba wao kimya. Tangu kocha hadi nahodha wao walikosekana kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi, kama kanuni zitafuatwa huenda wakatozwa faini ya Shilingi 500,000 kutokana na kutofika kwenye kikao hicho.
Ofisa Habari wa Bodi ya ligi kuu Tanzania (TPLB), Karim Boimanda alisema "Tumejitahidi kuwasiliana na Simba, wamekosa kupatikana, hili lililotokea litaamuliwa kwa mujibu wa kanuni."
Kanuni kwa 'Kulwa na Doto'?

Chanzo cha picha, yanga
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Simba na Yanga ni kama Kulwa na Doto katika soka la Tanzania. 'Watoto' pendwa wanaolelewa na kukua watakavyo. Ukitaka ugombane na mzazi wa watoto hawa, jaribu kuwachapa kwa 'kanuni' ama vyovyote, utakiona cha mtema kuni.
Kwa kuwa watoto pendwa, haishangazi mchezo huu uliopangwa kupigwa machi 8, umepigwa danadana na kuhairishwa mara mbili mpaka leo, tena kwa hati hati. Simba alianza kugoma kuingiza timu Machi 8, yanga akaeleza wazo kuwa haingizi timu uwanjani Juni 15
Leo Juni 25 bado hakuna mwenye uhakika wa asilimia 100 kwamba mchezo utakuwepo. Angalau matumaini pekee unaweza kuona tovuti ya Simba wameweka ratiba ya mechi hiyo na muda utakaopigwa, zaidi ya hapo hakuna kitu kingine.
Kanuni ya 31 ya Ligi Kuu inaeleza bayana adhabu kwa timu inayokosa kufika uwanjani bila sababu: faini ya milioni 5, kupokwa alama 15, na kulipa fidia ya maandalizi. Michezo miwili kuahirishwa kwa sababu zisizoelezwa kwa kina, na kama Simba haitofika uwanjani kama tetesi zinavyosemwa, kanuni hii inapaswa kuwa rungu. Itakapofanyika hivyo, kwa sababu ya Ukulwa na doto wao, matokeo yake, yataleta dunia nyingine kubwa ya soka.
Bodi ya ligi (TPLB) kwa kushirikiana na Shirikisho la soka Tanzania (TFF), wapo kwenye kona ngumu ya kisiasa ya mpira, wakikumbwa na lawama kuwa wanabembeleza "watoto pendwa" wa ligi (Kulwa ama Doto).
Tumefikaje hapa?

Chanzo cha picha, Simba
Awali, mechi hii ya Yanga na Simba ilipangwa kuchezwa Machi 8, 2025. Yanga walikuwa tayari kucheza , lakini Simba ikaingia mitini, mpaka leo hakuna sababu rasmi iliyotolewa. Mchezo ukasogezwa mbele hadi Juni 15, ambapo safari hii Yanga wakagoma kucheza hadi baadhi ya viongozi wa Bodi ya Ligi wajiuzulu. Hakuna aliyejiuzulu wakati huo, hivyo mechi ikapigwa tena chini.
Hali ilianza kubadilika baada ya picha ya pamoja ya viongozi wa Yanga na Simba kuonekana Ikulu wakiwa pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan, na baadaye kutangazwa rasmi kuwa mechi itapigwa Juni 25.
Muda mfupi baada ya hapo Mwenyekiti wa Bodi ya ligi kuu Tanzania (TPLB), Steven Mnguto alijiuzulu huku Rais wa TFF, Wallace Karia, akamsimamisha kazi Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almasi Kasongo.
Pamoja na kuondoka kwao kwenye kuongoza bodi ya ligi, kama moja ya takwa la Yanga walilolitoa ili wacheze mchezo, lakini bado, hisia za mchezo hazipo. Simba anaonekana kama kusuasua na kuufanya mchezo kuonekana usio na mvuto uliozoeleka nje ya uwanja.
Katika hali ya kawaida, mchezo huu ungebeba kila aina ya mvutano, makelele yangepigwa wiki nzima. Huu ndiyo mchezo wa kuamua bingwa wa Ligi Kuu msimu huu. Yanga wanaongoza kwa alama 79 dhidi ya Simba wenye 78. Timu zote zimecheza mechi 29. Yanga wanahitaji sare tu kutwaa ubingwa, wakati Simba ni lazima washinde.
Lakini ni kama mchezo wa mchangani, kimya, kizunguzungu, hakuna hekaheka. Badala ya mjadala wa mbinu, safu za ushambuliaji, au miiko ya ulinzi, mijadala imejikita kwenye swali moja: Je, mchezo upo au haupo? majibu ya mbivu na mbichi yatapatikana leo. Mbivu na mbichi si tu kwa Simba na Yanga, bali hata pia kwa TPLB na TFF wenyewe.














